Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Christina Solomon Mndeme (1 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi uliyonipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia ninaomba nianze kwanza kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uzima na kubwa kuruhusu mimi kuwa Mbunge na kuruhusu mimi kuwemo Bungeni leo hii. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wangu wa CCM na Halmashauri Kuu kupitisha jina langu, na mimi leo kuwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa alioupata; na ushindi huu alistahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee pia ninawashukuru wanawake wa Mkoa wa Tabora ambao walinipa kura ambazo ziliniwezesha leo kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Ahsanteni sana wanawake wote wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kinara mwongoza njia kwa kazi anazozifanya. Amegusa sekta zote, kila kijiji amegusa, kila mtaa amegusa, kila wilaya amegusa, kila mkoa amegusa na leo Tanzania ya leo, siyo Tanzania ya jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kuwapongeza walioshiriki wote kuandaa mpango huu. Hongereni sana. Wote mlioshiriki mpango huu ni mzuri ambao unaonesha dira ya wapi tunakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajielekeza kwenye ushauri, nianze na agenda ya nishati safi ya kupikia. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeye ndiye kinara namba moja nchini wa nishati safi ya kupikia, ndiye kinara namba moja wa Afrika na ndiye kinara namba moja wa ulimwengu wa nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona agenda hii imeleta mafanikio makubwa sana. Sasa hivi idadi ya watumiaji wa nishati safi ya kupikia wameongezeka kutoka asilimia sita nukta tisa mpaka 23.2%. Kazi kubwa imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana na ndugu zangu walioandaa mpango huu, wamegusia suala hili. Katika hili ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya 50% kwa mitungi 452,445 ya gesi ya kilo sita na kutoa ruzuku ya 85% kwa majiko banifu 200,000 kwa wananchi waishio vijijini na wanufaika wakubwa ni wanawake. Ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu, nishati safi ni uchumi, nishati safi ni afya, na nishati safi ni mazingira. Ninaomba sasa katika hili tuendelee kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi kama ilivyoelekezwa katika mkakati wa nishati safi ya kupikia aliyoizindua Mheshimiwa Rais mwezi Mei, mwaka 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika hili niwashauri tuongeze wigo wa upatikanaji wa majiko ya gesi na majiko banifu yenye ruzuku. Vilevile, nizipongeze taasisi 1,136 ambazo zimeitikia wito wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo zikiwemo Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa, baadhi ya vyuo vya elimu, hospitali zetu, shule na vyuo vingine vya kati, tunazipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu katika mpango huu ningeshauri, zipo taasisi ambazo bado hazijaunga mkono juhudi hizi za Mheshimiwa Rais. Agenda hii Mheshimiwa Rais ameileta kwa Watanzania kwa nia njema na nzuri akiwa yeye ni mwanamazingira namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke sheria, kanuni na miongozo mbalimbali na tuisimamie. Taasisi ambazo zinalisha watu zaidi ya 100 ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi ya kupikia zitumie. Isiwe sasa ni hiari, bali iwe ni lazima kwa mujibu wa sheria na taratibu ili mazingira yetu tuyatunze. Vilevile, sasa hivi kuna kaya takribani 2,000 zinatumia gesi asilia (natural gas) kwa ajili ya kupikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali hii inapatikana nchini kwa manufaa ya Watanzania. Ninashauri katika mpango wetu tuongeze wigo wa matumizi ya gesi asilia kwa matumizi ya kupikia majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninashauri tunahitaji uwekezaji katika nishati safi ya kupikia. Tunahitaji nishati safi, na teknolojia ya nishati safi. Tunamlenga mwanamke kwa sababu nishati safi ni Uchumi. Mama atatumia muda mfupi kupika na muda mrefu kufanya shughuli za uzalishaji mali. Tunamtaja mwanamke kwa sababu mwanamke ndiyo anatumia muda mwingi jikoni, yeye na mtoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kama ilivyoelekezwa kwenye mkakati wa nishati safi ya kupikia, tupunguze tozo na kodi kwenye nishati safi na teknolojia ya nishati safi ya kupikia na mashine za kutengenezea majiko haya ili sasa yapatikane kwa bei nafuu na wafanyabiashara wengi wawekeze katika nishati safi ya kupikia, na vilevile tuwe na teknolojia ya Pay As You Use. Unalipa kulingana na matumizi yako ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kutokana na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba Taifa hili linahama kutumia nishati isiyo salama na kutumia nishati iliyo salama, tuweke mazingira mazuri ili sasa wawekezaji waje kuwekeza zaidi na zaidi katika nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaomba kushauri ni suala la watoto njiti. Takribani watoto 300,000 huzaliwa njiti ndani ya nchi yetu. Tupanue sana huduma ya watoto hawa ili wasipotee kwa sababu wakipotea ni nguvu kazi inapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la Special Economic Zone. Haya maeneo ni muhimu sana kwa ukuaji wa Uchumi. Tupanue wigo ili sasa hizi Special Economic Zone zifanye kazi. Zikifanya kazi, wanawake wa Kitanzania watafanya biashara katika maeneo yao wanapopatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kongani (clusters) tuzipe umuhimu na kuzipanua, kongani za kilimo, za mifugo, za viwanda. Hizi kongani zikifanya vizuri uzalishaji ukaongezeka, mwanamke huyu wa Kitanzania atafanya biashara katika maeneo hayo na atatupatia fedha ya kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni viwanda kufufuliwa. Tufufue viwanda vilivyokufa. Kwa mfano, Kiwanda cha Nyuzi Tabora kimekufa, kiwanda cha Maziwa Mkoani Tabora kimekufa. Tufufue viwanda hivi ili wanawake hawa na vijana wetu wapate ajira na uchumi ukue, wazalishe ili pato la nchi liweze kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhakikisha kwamba wale waliopewa viwanda wameshindwa kuviendeleza wanyang’anywe wapewe wenye uwezo ili sasa vifanye kazi, uchumi ukue na watu wapate ajira wakiwemo akinamama; watafanya biashara ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda. Tujenge viwanda ili sasa maeneo ya kufanya biashara yawepo na ajira ikue ili uchumi wa wananchi wetu uweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mikopo kwa wanawake. Ninaomba tuongeze wigo wa utoaji wa elimu ya mikopo hii inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo ile inapotolewa tuhakikishe mazingira ya kufanyia biashara yanakuwa mazuri, na pia tutoe elimu, biashara za kuzalisha, wazalishe biashara zenye tija; TBS wafanye kazi, watembelee wanawake wawape elimu ya uzalishaji mali ili akinamama hawa waweze kukua katika bidhaa wanazozalisha. Pia wanapokwenda kwenye benki, wapate mikopo ya masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninaona muda wangu unakwenda, ni suala la mazingira…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia, Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwa na Taifa lenye kustahimili mabadiliko ya tabia ya nchi na himilivu, tutunze mazingira yatulinde na sisi tuyatunze sekta ya kilimo ikue ili sasa mwanamke afanye kazi maana mama ndiyo mkulima mkubwa nchini, kwa sababu sisi tupo wengi zaidi, takribani ya 51%. Tulime, tuzalishe, tutunze familia zetu na uchumi ukue kuanzia ndani ya familia na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa muda ulionipa, ninaunga mkono hoja. (Makofi)