MHE. CHRISTINA S. MNDEME aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo wa huduma za Watoto Njiti katika Vituo vya Afya vya Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya kibali alichonipatia kusimama mbele hapa. Kwa moyo wa dhati kabisa nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua ili niweze kumsaidia katika nafasi hii ya Unaibu Waziri. Pia, niwashukuru wananchi wa Muhambwe kwa kuendelea kuniamini ili niweze kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho siyo kwa umuhimu, ninaishukuru familia yangu ambayo imeendelea kunipa ushirikiano mkubwa kwa kipindi chote cha safari yangu ya siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Christina Mndeme, Mbunge Viti Maalum, kutokea Tabora.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za watoto njiti kwa Mkoa wa Tabora ambapo Hospitali ya Kitete imetengewa shilingi bilioni 4.5, Nzega TC shilingi milioni 460, Urambo DC shilingi milioni 460, na ujenzi huu unatarajiwa kuanza mapema Februari, 2026.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imepanua wigo wa huduma za watoto njiti katika Mkoa wa Tabora kwa kutenga vyumba maalum katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambavyo vimewekewa vifaa kwa ajili ya kutoa huduma za watoto njiti kutoka vituo sifuri mwaka 2018 hadi kufikia vituo 33 mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CHRISTINA S. MNDEME aliuliza: -
Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inawafikia Wanawake wote wenye uhitaji wa Mikopo katika Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Solomon Mndeme, Mbunge wa viti maalumu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba wanawake wenye sifa katika Mkoa wa Tabora wanafikiwa na mikopo ya 10% kwa kuongeza fedha zinazotengwa kwa vikundi vya wanawake. Katika Mkoa wa Tabora, kiasi cha mikopo kwa wanawake kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.54 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 4.80 mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika halmashauri za Mkoa wa Tabora Serikali inaendelea kuwasaidia wanawake kuunda na kusajili vikundi, kupata mafunzo ya ujasiriamali na kuandaa miradi yenye tija ili waweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo. Kutokana na hatua hizo, vikundi vya wanawake vilivyosajiliwa na kupewa mikopo vimeongezeka kutoka vikundi 234 mwaka 2020/2021 hadi vikundi 532 mwaka 2024/2025, huku vikundi vilivyopatiwa mafunzo vikiongezeka kutoka 1,718 hadi 5,907 katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inaendelea kutumia mfumo wa WEZESHA Portal katika usajili na usimamizi wa mikopo. Aidha, Serikali imezielekeza halmashauri zote kutangaza fursa hizo kwa uwazi kupitia mbao za matangazo, mikutano ya hadhara na vyombo vya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuongeza uhamasishaji na kuwajengea uwezo wanawake wanufaike zaidi na mikopo hiyo.