MHE. JASMINE C. NG’UMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, swali langu ni kuwa; je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha skimu za umwagiliaji zinafika katika Mkoa wa Iringa, hususani katika majimbo yote saba, ili kuweza kuwasaidia vijana wa Mkoa wa Iringa kujiajiri, lakini pia kulima kilimo cha kisasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mbunge wa Vijana, Mheshimiwa Jasmine Ng'umbi kwa jinsi ambavyo anawapigania vijana wa nchi hii. Yeye na Wabunge wenzake ambao wanawakilisha vijana hapa Bungeni wamethibitisha umuhimu wa kuwa na vijana makini wanaofuatilia masuala ya maendeleo ya vijana, kwa maslahi ya Taifa leo na kesho.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake ambalo kimsingi anauliza kwa upande wa Mkoa wa Iringa kwamba ni lini skimu hizi zitakamilika.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa katika mkoa wetu wa Iringa, Wizara ya Kilimo inatekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu karibu kwenye majimbo yote saba katika mkoa wetu. Pili, tuna miradi takribani 24 ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali ya usanifu, lakini tatu, tunayo miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mradi wa Ruaha Mbuyuni, Mradi wa Mgololo, Mradi wa Mkombozi na Miradi mingine, ambayo kimsingi inatekelezwa. Serikali inampa uhakika Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote ambao wanataka kufahamu kuhusiana na Mkoa wa Iringa na maeneo mengine, itakwenda kuongeza kasi kuhakikisha kwamba maeneo hayo, au wananchi wa Mkoa wa Iringa hususani vijana ambao yeye anawawakilisha, wanakwenda kunufaika ili washiriki kwenye uzalishaji, wapate ajira, wajenge uchumi na waweze kusaidia shughuli mbalimbali katika familia zao.
MHE. JASMINE C. NG’UMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kumekuwa na tatizo kubwa la ajali za bodaboda kutokana na hawa vijana wetu. Sasa ningependa kujua, Serikali haioni haja ya kutenga dawati maalum au kitengo maalum katika hospitali zetu, kuwasaidia hawa vijana wanaopata ajali za bodaboda ili wawe wanapewa kipaumbele au wanapata huduma za haraka wanapopata ajali hizi, kwani hawa vijana vifo vyao vimekuwa ni vingi sana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Tunaelewa kama sasa Tanzania yetu imekumbwa na teknolojia, na vyuo vyetu vinavyotoa elimu juu ya udereva vimekumbwa na teknolojia. Sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia, ningetamani kujua, je, Serikali haioni haja ya kuwasaidia hawa wahitimu wanaomaliza kila siku kwenye vyuo vyetu, kuwapatia elimu ya kisasa zaidi ili wanapopata ajira baada ya kuhitimu katika vyuo vyao, kuweza kuwa madereva mahiri na kuweza kuutumia ujuzi huo walioupata kwa umahiri zaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Jasmine Chesco Ng’umbi kwa jinsi ambavyo amejitoa kuamua kuwasemea vijana wenzake wa nchi hii haswa kundi la bodaboda. Ninakubaliana na ushauri wake kuhusu umuhimu wa kuweza kuwa na mkakati maalum wa kuwatazama hawa vijana wanaopata ajali, kwa sababu ni nguvu kazi ya Taifa. Wanapata ajali wakiwa wanakwenda kuhangaika kutafuta riziki za familia zao na kujenga nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kupitia Wizara yetu ya Afya, ninaamini jambo hili wamelipokea, wataona namna bora ya kuweza kulifanikisha, na sisi kama Sekta ya Uchukuzi tutakuwa tupo tayari kwa ajili ya kulifanikisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusiana na teknolojia namna gani ambavyo tunaweza kushiriki kikamilifu kuhakikisha kwamba vijina wetu mafunzo tunayowapatia, yanakuwa yanakidhi teknolojia ya sasa. Ni kweli hata hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya madereva wakipelekwa nje ya nchi. Teknolojia waliyojifunzia hapa kwetu wakienda huko inakuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea ushauri huu, tunauingiza Serikalini kuanza kuuchakata. Nitumie nafasi hii kutoa maelekezo kwa Chuo chetu cha Taifa cha Usafirishaji ili waendelee kutoa mafunzo ambayo dereva au kijana akipata mafunzo huku kwetu, akienda mahali pengine popote duniani, aweze kufiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe rai na maombi kwa vyuo vingine na taasisi nyingine ambazo zinatoa mafunzo ya namna hiyo, ili kuweza kutazama mabadiliko ya teknolojia. Wahitimu mnaowatoa hapa waweze kuwa competitive mahali popote wanapokwenda duniani.