Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JESCA J. MAGUFULI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amenijaalia uhai na kuniwezesha kusimama hapa siku ya leo kwa niaba ya vijana wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninaanza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameweza kutekeleza dhima ya kuweza kuwainua vijana, hususan katika sekta ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo imeweza kudhihirishwa kutokana na mikopo na jitihada ambazo Mheshimiwa Rais amekuwa akizifanya kwa kusaidia kutoa mikopo kwa vijana. Kwa kweli, hili lazima tusimame kama vijana kumpongeza kwa jinsi ambavyo ameweza kuonesha na ameweza kusimama thabiti na vijana wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza pia Waziri wa Maendeleo ya Vijana, kaka yangu Mheshimiwa Joel Nanauka. Kwa kweli, amewasilisha hotuba yake leo asubuhi na tumeweza kuipitia, lakini kwa kuipitia huko tumeweza kutambua ni jinsi gani ambavyo amejikita zaidi katika kuwasaidia vijana, kuwainua, na kuleta mapinduzi makubwa, ambayo yanawalenga moja kwa moja vijana wa Kitanzania. Kwa hiyo, ninampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yameongelewa na vijana wenzangu, lakini kwa siku hii ya leo ninaomba nijikite kwenye mambo makuu mawili, nikianza na suala la mikopo. Kweli Serikali imejizatiti na imekuwa ikiendelea kutoa mikopo kwa vijana, lakini bado hatuwezi kutegemea mikopo tu. Ninajua ni ukweli mchungu, lakini lazima tuongee, kwamba hatuwezi kutegemea mikopo tu katika kuwezesha vijana hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo hii, ili kijana aweze kunufaika kibiashara, ili kijana aweze kuwa na consistency katika biashara, ili kijana aweze kutanuka zaidi katika biashara, ni lazima tuwe na mfumo jumuishi wa ujasiriamali wa vijana wetu wa Taifa hili la Tanzania. Tunapozungumzia mfumo huo wa ujasiriamali kwanza kabisa ni lazima tuwajengee uwezo (capacity building) vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajikita zaidi katika kutoa mikopo ambayo kweli imekuwa ikitusaidia, lakini lazima tuwajengee uwezo vijana hawa ili waweze kupata elimu au mwanzo mzuri wa kuweza kuitumia mikopo hiyo. Ninaposemea hapa katika capacity building, nitajikita zaidi katika suala la elimu ndogo ndogo tu kama ya utunzaji wa fedha na pia elimu ya kuweza kutambua kodi za Serikali na jinsi ya kuanza mwanzo wa biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itamwezesha kijana huyu hata anapoingia katika biashara kupitia mikopo ambayo imetolewa kuweza kutambua ni namna gani ataweza kutunza kumbukumbu zake za fedha na ni namna gani ataweza kukabiliana na kodi ambazo zitakuwa zinakuja. Anakuwa na uelewa wa kodi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nizungumzie kuhusu mafunzo ya kisekta (specific training). Kweli mikopo imekuwa inatolewa na vijana wamejikita waziwazi katika kuwekeza katika nyanja tofauti. Wengine wamejikita katika kuwekeza katika teknolojia, lakini wapo ambao wamejikita kuwekeza katika kilimo, na wapo ambao wamejikita kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo. Kusema kuwachukua hao wote na kuwapa training siku moja kwa ujumla ni uongo. Ni sawasawa na kutwanga maji kwenye kinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwatafute ma-professional. Uzuri, Wizara ya Vijana inaweza kushirikiana na Wizara nyingine kama ya teknolojia, Wizara ya Kilimo pamoja na Mifugo, ili kuwasaidia vijana hawa pale ambapo wamepewa mkopo huo na inapoambatana na mafunzo hayo, ambayo ni ya kimkakati yatakayotolewa, kuwekeza zaidi na kwa ufasaha na kwa ukubwa ambao Serikali inataka iwekeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhusu suala la addition of value, kuwajengea thamani vijana hawa. Mikopo inatolewa, lakini pia, lazima tuhakikishe kwamba tunawajengea thamani ya bidhaa zao ambazo vijana wamejikita zaidi katika kuziwekeza. Bidhaa hizi ni lazima ziambatane na soko la ushindani ambalo lipo Kitaifa na Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kuwapatia training, na pia, kuwasukuma kuwezesha kuzalisha bidhaa ambazo zinaendana na soko la kila siku. Tusije tukawa tunatoa mikopo, lakini mwisho wa siku mikopo hiyo ikawa vijana wana-produce products ambazo ni za hapa hapa tu, yaani haziendi sehemu yoyote, na hazina ukuaji. Kwa hiyo, ni lazima tufuatilie, na ni lazima tu-intensify hili kwa ajili ya kusaidia kumpatia kipato kijana huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu upatikanaji wa masoko. Ni kweli Serikali imejikita katika kuendelea kutoa mikopo hiyo, lakini je imewatafutia soko vijana au ndiyo tunatoa mikopo na tunawaacha tu waendelee ku-hang hang tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwatafutie masoko ya Kimataifa na ya Kitaifa pia. Kwanza utamjengea uwezo kijana huyo, na jambo la pili utamsaidia yeye mwenyewe kuongeza kipato, comfort ambayo anaipata pale ambapo anapata mkopo. Pia Serikali iwatafutie masoko kuweza kuuza bidhaa hizo ambazo wataweza kuzalisha kupitia mkopo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba Waziri niendelee kumshauri jambo la mwisho kuhusu kuanzisha maonesho ya vijana (youth expo).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imekuwa ikisifika kwa kuanzisha maonesho ya biashara kama Saba Saba ambayo kiuhalisia yamekuwepo kwa miaka mingi, lakini pia kuna maonesho ya wakulima Nane Nane. Kwa nini sasa isifike wakati nasi tuwe na maonesho yetu, kwa kuwa tumetoa mikopo na tumewawezesha vijana hawa, database tunayo, kwa nini tusiwajengee kuwepo na maonesho hayo ya vijana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca muda wako umeisha.
MHE. JESCA J. MAGUFULI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie.
MWENYEKITI: Malizia kwa kuunga mkono hoja.
MHE. JESCA J. MAGUFULI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)