Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Johnston Johansen Mutasingwa (3 total)

MHE. ENG. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninapenda kuuliza swali la nyongeza kuhusu barabara zangu za Jimbo la Bukoba Mjini. Barabara ya kutoka Chemba kwenda Rugambwa, yenye urefu wa kilometa 1.4 na Barabara ya kutoka Kashai kwenda Mngeza, yenye urefu wa kilometa 7.41 zitaanza kujengwa lini kwa kiwango cha lami, kama ilivyoainishwa kwenye IIani ya Chama Cha Mapinduzi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, barabara hizi za Bukoba Mjini zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, kama ambavyo imeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi, mara tu baada ya Serikali kupata fedha na kutenga, kwa ajili ya shughuli hiyo.
MHE. ENG. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tuna vijana wengi sana wamejiajiri hasa upande wa garage. Kwa mfano pale Jimbo la Bukoba Mjini, tuna vijana zaidi ya 250 wako kwenye garage ya Mnyonge, lakini wako barabarani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuwatengea maeneo maalumU ya kufanyia shughuli zao hizo za garage ili waweze kwanza kuwa na uhakika wa shughuli zao, lakini waweze kuwa na sifa za kupata mikopo ya Serikali? Ahsante
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa swali la Mheshimiwa Mutasingwa na bahati nzuri nilishafanya ziara katika jimbo lake na nilipita katika maeneo ya garage na tulikuwa naye pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba vijana hawa kwanza tunawarasimisha ili kupata urahisi wa wao kupata fursa ambazo Serikali inazitengeneza. Mpaka sasa kupitia programu ya urasimishaji ambayo inafanyika kupitia VETA, mwaka huu pekee yake malengo ni kurasimisha vijana 14,400. Ninaamini vijana mojawapo watakaopata fursa hii ni vijana wanaopatikana katika jimbo lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupitia TAMISEMI kumekuwa na utaratibu wa kupanga maeneo rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanapata maeneo ambayo hawatabugudhiwa. Nimhakikishie, Serikali itaendelea kuratibu zoezi hilo na vijana wataendelea kupata nafasi na fursa za kufanya kazi katika maeneo ambayo ni rasmi. Ahsante sana.
MHE. ENG. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda niishukuru Serikali kwa majibu mazuri iliyoyatoa na sasa naona changamoto ya umeme kupungua au low voltage katika Jimbo letu la Bukoba Mjini linaenda kutoweka. Sasa ninapenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Je, ni lini Serikali sasa itamlipa huyu mkandarasi ili aweze kumaliza hiyo kazi kwa wakati na kama Serikali ilivyoahidi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika Jimbo letu la Bukoba Mjini tuna Kata kama nane ambazo zinapakana na Jimbo la Bukoba Vijijini ambazo ni Ijuganyondo, Tendagulo, Kibeta, Kashai hasa maeneo ya Rwomwe, Ijuganyondo, Kahororo na Buhembe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi hawa umeme wa REA kwa shilingi 27,000 ili waweze na wenyewe kupata huduma ya umeme kwa uhakika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba kumpongeza Engineer Mutasingwa, Mbunge wa Bukoba Mjini kwa jinsi ambavyo amekuwa mtetezi wa dhati wa mahitaji ya msingi ya wapigakura wake wa Jimbo la Bukoba Mjini. Engineer huyu kwa kweli anapenda wapigakura wake wajue kwamba hawakukosea kumleta katika Bunge lako Tukufu, maana ni mtetezi wa kweli wa mahitaji ya watu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la msingi, ni lini huu mradi utakamilishwa wa kuongeza hiyo transfoma ya kuongeza umeme ambao umeshatekelezwa kwa 65%, ninapenda kukuhakikishia kwamba, kwa kuwa IPT imeshapelekwa Wizara ya Fedha, mkandarasi huyu atalipwa na mradi huu unakwenda kukamilika ndani ya muda uliopangwa ambao ni kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu Kata na Vijiji alivyovitaja anavyoviombea vipewe umeme wa REA, hizi bila shaka ni vile vijiji vinavyopakana na Miji, tunaviita Peri-urban areas ambavyo kuna siku Waziri amesimama hapa katika Bunge lako Tukufu akatoa ufafanuzi kwamba vijiji hivyo vinavyopakana na miji yenye hadhi ya vijiji, vyote vitakwenda kupatiwa umeme wa REA kwa bei ya shilingi 27,000. Ahsante sana. (Makofi)