Answers to supplementary Questions by Hon. Mohammed Mahmoud Ayoub (6 total)
MHE. IBRAHIM S. MZIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa vituo hivi vinahudumiwa na ndugu zetu wa polisi ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kulinda nchi yetu. Je, Mheshimiwa Waziri, yupo tayari kuambatana nami kwenda Jimbo la Mtambile kujionea hali halisi ya makazi ya polisi wetu hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Said Ibrahim; na ombi lake la kwenda Mtambile nimelipokea na nipo tayari kuambatana naye kwenda Mtambile.
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninashukuru kwa kunipatia fursa hii nami kuuliza swali langu la nyongeza. Pale Mkoani kwangu Kaskazini Pemba pana Kituo cha Polisi cha muda mrefu. Kituo kile kilizinduliwa tarehe 25 Juni, 1979. Kwa kuongezeka wananchi katika Mkoa ule wa Kaskazini Pemba. Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi katika Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na jengo la RPC wa Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Asha Omar, Mbunge wa Viti Maalum, Kaskazini Pemba, kwa swali lake zuri; na nimpongeze sana kwa kuwa karibu sana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi na kubaini pia changamoto zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleza katika majibu yangu ya msingi wakati nikijibu wiki iliyopita, kwamba kwa upande wa ujenzi wa vituo vya polisi vya mkoa tulikuwa tunakiri kwamba tuna mikoa mitano ambayo ilikuwa haina vituo vya polisi; lakini kwa upande wake alikuwa anaongelea zaidi kuhakikisha kwamba anafanya ukarabati wa jengo la RPC katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambalo hilo nalo lipo kwenye mpango wa ukarabati kama ambavyo tunaendelea nao. Kwa sasa tuna miradi 56 ya ukarabati nchi nzima katika ngazi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo ninaamini kwamba tukienda kwenye hatua ya pili ya mpango wa kukarabati jengo hilo nalo litaingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa yale majengo mawili ya wilaya kwa maana Wilaya ya Wete na Wilaya ya Michiweni Kaskazini Pemba nayo yapo kwenye majengo 75 ambayo kwa sasa ama yapo kwenye hatua ya ukarabati ama ujenzi upya kwa wilaya zetu 75 za nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Jeshi la Polisi tupo kwenye hatua ya kukamilisha mpango mkakati wa miaka mitano ijayo. Wakati tukiendelea na hatua hiyo, tunaendelea vilevile kutathmini hali ya majengo ya vituo vya polisi, makazi ya askari na maeneo mengine yakiwemo hospitali na majengo ya mazoezi ya vikosi vyetu vya Field Force na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue, wapo Wabunge wengi ambao wamehitaji ama kujengewa ama kufanyiwa ukarabati vituo vya polisi. Kwa ruhusa yako ninaomba niwatambue Mheshimiwa Florence George Samizi, Mheshimiwa wa Kigoma, Mheshimiwa Joseph Copriano Isack au Kadogo wa Monduli wamehitaji hilo, ninatambua pia hitaji lake, Mheshimiwa Anne Kilango Malacela naye na nimemwahidi nitakwenda pia kwenye eneo lake, pamoja na Mheshimiwa Ester Bulaya naye pia alihitaji pale Bunda Mjini, naye nimemwahidi pia nitakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nina swali dogo la nyongeza. Kama ikimpendeza Mheshimiwa Naibu Waziri atalijibu au atalichukuwa. Wilaya yetu ya Malinyi tumekuwa tuna shida ya gereza la mahabusu kwa muda mrefu sana. Eneo limepatikana lakini kumekuwa kuna ucheleweshwaji wa kukamilisha ambayo inawafanya wahusika kusafiri umbali mrefu sana kwenda Wilaya ya Ulanga. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimfahamu ili niweze kujibu vizuri; amekusudia mahabusu ya polisi au ya gereza?NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mahabusu ya gereza.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaongelea kuhusu suala la Jeshi la Polisi lakini kwa sababu Magereza na yenyewe ni sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini ninaomba tu nimjibu Mheshimiwa Kapoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo baadhi ya magereza yamekuwa na changamoto ya uchakavu wa majengo. Hata hivyo, moja ya eneo ambalo amelitaja la jimbo lake kwamba wilaya nzima ya Malinyi hakuna gereza na kupeleka eneo la pili; tunakuja na mpango na tutaueleza kwenye bajeti ya mwaka huu kwamba ni mpango gani kwa upande wa Jeshi la Magereza, tutaenda kuboresha magereza katika maeneo ambayo yana uhaba likiwepo eneo lake la Malinyi.
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa ruksa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Jimbo la Bumbwini, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewekeza nguvu kubwa sana katika uchumi wa nchi na maeneo mengine; je, haioni sasa kuna haja ya kujengwa kituo kikubwa cha polisi katika jimbo hilo kutokana na uchumi wa nchi ulivyokuwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mwinyi Jamal swali lake la nyongeza kuhusiana na jimbo lake la Bumbwini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba Bumbwini kwa sasa ni eneo la kimkakati hasa kwa uchumi wa Zanzibar, kwani Bumbwini inaenda kuelekea kujengwa uwekezaji wa bandari kubwa mpya; Bandari ambayo itakuwa na maeneo karibu matano. Katika bandari ile kwa bahati nzuri wakati nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa mkoa ule, niliwahi kupata fursa ya ushiriki kidogo wa maandalizi ya bandari hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango ulioandaliwa wa eneo lile la Bumbwini kumeandaliwa kujengwa miundombinu yenyewe ya bandari, miundombinu ya barabara za kisasa lakini pia kujengwa mji mdogo. Katika mpango uliowekwa wa mji mdogo ndani yake kuna ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi ambacho kitaweza kusaidia kuimarisha eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali imewekeza vituo vingi vidogo vidogo na sasa vituo hivyo vyote havifanyi kazi ikiwemo kituo changu cha Jimbo la Shaurimoyo na vituo vingine. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifufua vituo hivyo vikaanza kufanya kazi ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mattar swali lake la nyongeza ambalo linahusu vituo vidogo vya polisi kwa maana ya daraja C1 au police post.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri hasa kwa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, kulijengwa vituo vingi vya police post katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, ninaomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza siyo vituo vyote vidogo vidogo kuwa havitumiki, vipo baadhi yake vinatumika. Mfano wa vituo vidogo vidogo vinavyotumika ni Kituo cha Mkunazini, Kituo cha Vuga na vinginevyo. Kwa vile ambavyo kwa sasa havitumiki tumefanya tathmini kupitia Jeshi la Polisi kuona namna gani nzuri ya utumiaji wa vituo vidogo vile vya polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukiri vingi ya vituo hivyo vipo maeneo karibu karibu. Kwa hiyo Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeona haja ya kuwatumia Askari wa Ulinzi Shirikishi kwa kushirikiana na Polisi wa Shehia ili wafanye doria badala ya kuweka askari wengi kwenye kituo kimoja na kutoa huduma bila ya ufanisi kama ambavyo ingetarajiwa. Kwa hiyo, bado vituo hivyo tuna mpango wa kuvitumia, lakini kwa utaratibu mwingine kinyume na ule wa awali hadi hapo tutakapokuwa na askari wa kutosha wa kuweza kuwaweka vituoni na wengine kufanya doria.
MHE. TIMOTH G. ANYOSISYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tarehe 29 Oktoba, 2025 Jimboni Kawe vilichomwa Vituo vya Polisi vitatu. Kwetu sisi Wanakawe jambo hili tunalichukulia kama jambo la dharura. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivi ili kurejesha hali ya huduma ya kipolisi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba nimjibu swali lake Mheshimiwa Timoth kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tarehe 29 Oktoba, 2025 kulitokea uharibifu wa mali mbalimbali za Serikali ikiwepo baadhi ya Vituo vya Polisi katika baadhi ya maeneo. Ninaomba nimwambie Mheshimiwa Timothy kwamba Serikali inaendelea kukamilisha kazi ya tathmini na kuja na mpango wa dharura wa kuona namna gani ya kuweza kurejesha huduma kwenye maeneo husika. (Makofi)