Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi uliyonipa ya kuweza kuhitimisha hoja baada ya michango mizuri sana ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza kwa kuwashukuru kwa namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwa umakini mkubwa sana na kila mchango uliokuwa unatolewa ulikuwa unaona kabisa inatoka moyoni, nikimaanisha kwamba Bunge hili lina dhamira njema na limeweka vijana katikati ya ajenda za muhimu katika mijadala yetu. Kwa hiyo, niwapongeze sana na niwashukuru sana pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi ambayo yamezungumzwa, yamegusia ushauri, na ninapenda kukiri kwamba yale yote ambayo yametolewa kama sehemu ya ushauri, sisi kama Wizara pamoja na watendaji tunayachukua, tutayafanyia kazi pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo masuala kadhaa ambayo ninaomba niyatolee ufafanuzi ili kuendelea kuwa pamoja katika namna ya uelewa, lakini pia kupata ufahamu mpana katika maeneo ambayo nilieleza katika hotuba yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa, ninaamini kwamba sisi wote kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunakubaliana kwa pamoja na dhamira ya Mheshimiwa Rais kuhusiana na kuwawezesha vijana wa nchi hii. Dhamira hii ameionesha hata kabla ya kuiunda Wizara hii ya Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anatoa ahadi kipindi cha kampeni katika ahadi zake hasa zile ahadi za siku 100 hadi 13 Wizara ilikuwa haijaundwa bado, lakini ulikuwa unaona kwamba Mheshimiwa Rais alikuwa na lengo mahususi kuhusiana na uwezeshaji wa vijana. Katika ahadi zake 13, ahadi sita ziligusa moja kwa moja maisha ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuja akihutubia Bunge, wakati analifungua Bunge hili, tutakumbuka alizungumza mambo mengi sana yanayohusiana na vijana. Ukipitia katika kile kitabu chake cha hotuba utagundua kuna mambo kama 13 mahususi ambayo aliyagusia yanahusiana na uwezeshaji wa vijana kiuchumi, kijamii, kisiasa, na pia katika nafasi za uongozi na maamuzi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hilo, ningependa kwa mara nyingine tena niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na vijana wa Tanzania kwa ujumla kwamba Mheshimiwa Rais anayo dhamira ya dhati ambayo hajaifanya tu kwa maneno, lakini ameendelea kuitekeleza kwa vitendo kwenye masuala ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kumekuwa na sera ambazo zinaongoza masuala ambayo yanahusiana na vijana. Tumekuwa na Sera yetu ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 ambayo kupitia Sera hiyo Serikali imekuwa na mkazo mkubwa sana katika masuala mbalimbali ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumesikia katika baadhi ya michango ambayo imetolewa hapa kwamba ipo sheria iliyopitishwa ya Manunuzi ya Umma (PPRA) inayotaka taasisi kutenga 30%, na katika hizo, 10% ni kwa ajili ya vijana. Sheria hii ilitungwa kwa sababu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba Serikali inapoweka sera, inakuwa na nia ya dhati kuingiza utekelezaji katika vitendo. Leo ninapozungumza, mwaka 2025 peke yake vijana walioingia katika Mfumo wa NeST wameweza kupata tender za thamani ya shilingi bilioni 13.2. Hii yote ni kumaanisha kwamba Serikali haizungumzi tu uwezeshaji wa vijana, lakini pia inatoa fursa katika maeneo hayo pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, leo tunazungumza mikopo ya 10%, mikopo hii pia ni matokeo ya Sera ya Maendeleo ya Vijana. Ilipotengenezwa sheria ya kutoa mikopo hii katika Serikali za Mitaa, ni kwa sababu ya uboreshaji ambao umetokana na uundwaji wa sera ya maendeleo ya vijana. Ndiyo maana, Mheshimiwa Rais alitoa agizo alipoingia madarakani, turejee Sera ya Maendeleo ya Vijana ili kuiboreshsa zaidi. Sasa hivi tunayo sera ya mwaka 2007, na toleo jipya la mwaka 2024 ambalo limelenga maeneo mahsusi ya kuwezesha vijana wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwamba, pamoja na mambo ya jumla tunayoyazungumza, lakini tunao utekelezaji mahususi ambao tunautekeleza kwa kutumia sera hii. Sera hii uzuri wake pia, imetengeneza mkakati wa utekelezaji kati ya mwaka 2024 mpaka 2034.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati huo wa utekelezaji, yapo masuala ambayo yanahusisha sekta binafsi, sawasawa na maono yetu na mpango wetu wa mwaka 2050 ambao unataka sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi ambao wanahusiana na masuala ya vijana pia wachangie maendeleo ya vijana katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, katika utekelezaji wa afua za vijana, pamoja na juhudi ambazo Serikali inazifanya, tunayo mahusiano mazuri na sekta binafsi kwa kupitia miongozo ambayo Serikali imeweka na tutahakikisha pale ambapo bado kuna gaps, tutatumia mikakati hiyo ambayo tumeweka ili kutekeleza masuala yanayohusiana na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la pili ambalo limezungumzwa kwa mapana sana, na nikiri kwamba limetolewa ushauri mwingi sana, na sisi tumeupokea, ni eneo la mikopo. Limezungumzwa kwa mapana na hoja nyingi zinazungumzia juu ya uboreshaji wa vigezo vya mikopo, juu ya urahisi wa vijana kupata mikopo na masuala yanayofanana na hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe maelezo machache kwenye eneo hili. Kwanza, ningependa kuwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba, kuna mabadiliko na maboresho makubwa sana yamefanyika katika utoaji wa mikopo hasa inayotolewa katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Kupitia mwongozo mpya ambao ninao hapa, unaitwa Youth Development Fund Operation Guidelines, tumeboresha maeneo kadhaa ambayo ningependa niyataje kwa ufupi ili pia tuweze kuyafahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo vijana walikuwa wakilalamikia lilikuwa eneo la riba, kwamba ilikuwa ni kubwa. Kupitia mwongozo huu kwa sasa, riba imeshuka sana, na hata hatuiti riba, tunaita administrative costs, kwa sababu, asilimia ambayo wanachajiwa kwa muda wote wa mkopo, hata kama amekopa miaka mitatu yote, ni asilimia tano, siyo kwa mwaka ni kwa miaka yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia tatu ni kwa ajili ya taasisi ya kifedha ambayo inatusaidia kutoa mafunzo na usimamizi, asilimia moja ni kwa ajili ya bima, asilimia moja inayobakia ni kwa ajili ya kurudisha kwenye mfuko ili ule mfuko uwe ni revolving. Kwa maneno mengine ni sawa na kusema kwamba, masharti ya riba yamekuwa ni madogo sana kwa ajili ya mikopo ambayo inatolewa na Serikali kwa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo lilikuwa linazungumzwa sana ni eneo la ukopaji wa mtu mmoja mmoja badala ya kukopa kwa vikundi. Mwongozo wetu wa sasa hivi unaturuhusu kufanya hivyo. Hivi ninavyozungumza, katika ripoti ambayo niliisoma hapa, vikundi ambavyo tumewapa na wapo watu binafsi ambao tayari pia tumewapatia mikopo hii ambayo inatokana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ili pia kuthamini vijana ambao wana kampuni binafsi au wameanzisha juhudi zao wenyewe binafsi za kuweza kutekeleza malengo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limeboreshwa ni eneo la grace period. Nilizungumza katika hotuba yangu pia kwamba, sasa hivi kijana akikopeshwa fedha hii ambayo inatoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, anapewa miezi mitatu kabla hajaanza kulipa deni lake. Anapewa miezi mitatu ya kuboresha biashara yake, hata kama biashara inaendelea, Serikali imesema tunakupa miezi mitatu kwanza, uongeze mtaji wako wa uzalishaji, baada ya miezi mitatu ndiyo utaanza kulipa deni lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara nyingine tumezipa miezi sita, na nyingine kama za uzalishaji kwa mfano, kama samaki, visima vya samaki au kwenye kilimo, wanalipa mpaka baada ya miezi minane, hawadaiwi chochote na hawatakiwi kulipa jambo lolote lile. Jambo hili pia tumelifanya kama sehemu ya kuboresha mikopo hii kwa ajili ya vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo lilikuwa linalalamikiwa ni dhamana, kwamba kijana akienda anahitaji kupewa dhamana. Ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tumezungumza katika hii ripoti, katika muda mfupi tangu Wizara hii imeundwa, tumetoa zaidi ya shilingi milioni 400, na hakuna kijana yeyote aliyepata fedha hizo ambaye ameombwa dhamana ya aina yoyote katika mkopo ambao tumempatia. Dhamana tunayohitaji sisi kwa walio katika vikundi, kikundi chao ndiyo kilikuwa dhamana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunampa asset, kama ni pikipiki, au guta, ama truck la kufanyia biashara, ile asset tunayompa ndiyo inafanyika kuwa dhamana, haiitaji nyumba, haiitaji kiwanja, shamba wala kitu chochote kile, kwa sababu, hayo ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba turahisishe upatikanaji wa mikopo kwa vijana wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie, huo ndio mwelekeo wa Wizara. Katika fedha ambazo tutaendelea kuzitoa za mikopo, hayo ndiyo masharti ambayo tumeyaweka, ambayo ni masharti nafuu ambayo tunaamini mtu yeyote na kijana yeyote yule mwenye nia ya dhati anaweza pia kuyakamilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tumeboresha ni eneo la usimamizi. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza hapa kwamba, vijana wanapewa mikopo lakini baada ya hapo pia inakuwa ni changamoto wao kuweza kurejesha, kwa sababu ya ufahamu na ujuzi wa biashara na elimu ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeingia makubaliano na baadhi ya taasisi za kifedha tayari, ambazo zenyewe kazi yake mojawapo ni kutoa mafunzo kwa vijana kabla hawajapata mkopo, lakini pia kipindi chote wakati wanahudumia ule mkopo, taasisi hizi za kifedha huwa zinaendelea kutoa mafunzo kwa ajili ya hawa vijana ili kuhakikisha wanafanyiwa mentorship ili wawe na uwezo wa kukuza biashara zao pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia pia kuondoa defaulters wengi katika hii mikopo kwa kuzingatia kwamba mikopo hii dhamira yake ni kwamba, akirudisha waweze kukopeshwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo pia cycle ya mkopo tumeipunguza sana. Kwa sasa hivi, akisha-apply tuna siku 14 za uchambuzi, baada ya hapo tuna siku 10 nyingine za kufanya uhakiki, na baada ya hapo kuna siku 10 zinazofuata kwa ajili ya kufanya disbursement. Kwa hiyo, ndani ya mwezi mmoja, tunakuwa tuna uwezo wa kufanya uhakiki unaojitosheleza na kuweza kutoa hiyo mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mikopo tuliyoitoa Mwanza, walikuwa wameomba mwezi wa 12 na mwezi wa Kwanza tuliweza kuwapatia pale vikundi viwili. Kikundi kimoja shilingi milioni 100 kwa ajili ya ufugaji wa Samaki, na kikundi kingine cha Buswelu tuliwapatia shilingi milioni 100 ambao wanafanya shughuli za usafirishaji wakiwa na maguta pamoja na pikipiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, maboresho makubwa sana yamefanyika katika suala zima la mikopo na ninaomba mwendelee kuiunga mkono Serikali na dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwezesha vijana wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ambalo Waheshimiwa Wabunge wameliongea kwa dhamira ya dhati sana kwamba, bado fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni chache sana. Ninakubaliana na mawazo hayo kwa kuangalia wingi na mahitaji ambayo tunayo katika sekta mbalimbali za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kukumbusha kwamba, Mfuko huu wa Maendeleo ya Vijana kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwake, umekuwa ukitengewa shilingi bilioni moja. Kuna baadhi ya miaka fedha hiyo pia ilishindikana kutoka kwa sababu za kibajeti. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, bajeti hii, tumeleta mezani shilingi bilioni tano, mara tano zaidi ya fedha ambayo ilikuwa inatengwa kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea kwenye ripoti yangu, katika mwaka wa fedha uliopita tulitengewa shilingi bilioni moja. Leo ninavyozungumza, Serikali haijaweka tu shilingi bilioni moja, tayari imeweka shilingi bilioni 2.5 zaidi ya ile ambayo mwanzoni ilikuwa imetajwa pale. Maana yangu ni nini? Pamoja na uchache na uhaba tunaouona katika fedha hizi ambazo zimetengwa sasa hivi, lakini ukweli ambao hatuwezi kuupinga ni kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa zaidi katika fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kwamba, kwa sababu tunaanza, baadaye zitaendelea kuongezeka kadiri mipango inavyokuwa inaendelea. Kwa hiyo, ningeomba Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono katika hili ambalo tumeliweka mezani, ili tuanzie hapa tukiwa tunaendelea kujenga zaidi na kuongeza wingi wa fedha hizi ambazo zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo zimetolewa kwenye Mfuko huu wa Maendeleo ya Vijana siyo fedha pekee za vijana ambazo wanazi-access katika nchi hii. Ninashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wameongea, na wametoa mawazo mazuri sana ya namna bora ya ku-manage fedha hizi katika namna ambayo wameitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba vijana wa nchi hii, bado ukiacha shilingi bilioni tano ambazo tumeziomba hapa, yapo maeneo mengine mengi ambayo, kama ambavyo Wabunge wamechangia, vijana wanaendelea kuwezeshwa katika namna mbalimbali na nitatoa mifano michache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumekuwa tukizungumzia hata 10% ya uwezeshaji hapa, kwa mwaka jana pekee tuliona shilingi bilioni 130 zilienda kwa ajili ya hawa vijana. Hiyo ni kwa ajili ya vijana peke yao katika ile asilimia nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya tatizo ambalo tumekuwanalo ambalo ndiyo tunajaribu kulitibu sasa ni kwamba, pamoja na utokaji wa fedha nyingi kwa makundi ya vijana, zile zinazorudi ni chache. Sasa mfuko usipokuwa ni revolving fund, zisiporudi maana yake zinatukosesha uwezo. Nitatoa mfano kidogo, katika shilingi bilioni 130 ambazo zimetolewa kwenye asilimia nne kwenye Serikali za Mitaa, zimerudi shilingi bilioni 49 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata leo sisi kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuna shilingi bilioni 3.9 ambazo zipo nje, ambazo vijana wameshindwa kuzirudisha bado. Ndiyo maana katika mkakati wetu, tumeona pamoja na kutoa fedha kama Mwalimu Nyerere alivyosema, kwamba fedha siyo engine ya maendeleo peke yake, tunahitaji uwekezaji katika ufahamu, tunahitaji uwekezaji katika tabia, tunahitaji uwekezaji katika nidhamu ya hawa vijana pia, ili waweze kuwa na uwezo wa kurudisha hizo fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na uchache unaoonekana, lakini bado naweza nikasema kwamba, Serikali imeongeza nguvu na kasi kubwa zaidi katika uwezeshaji wa vijana katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningeomba nilizungumzie kwa sehemu, ni kuhusiana na kufikisha taarifa kwa vijana. Nakubaliana na michango mizuri sana ya Waheshimiwa Wabunge, ambayo wameitoa kwamba bado tunahitaji kuongeza nguvu na mbinu zaidi za kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali. Ninapenda kusema mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba, tutaendelea sisi kama Wizara, tumetumia mbinu mbalimbali kama ambavyo tumeeleza katika ripoti yetu kuwafikia vijana physically kwa maana ya uso kwa uso, kutumia teknolojia na tunaamini bado lipo kundi lingine ambalo linakosa taarifa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaahidi Waheshimiwa Wabunge, Serikali ina mtandao mpana mpaka ngazi ya kata, na bado tunaendelea kujipanga vizuri hasa tunapoendelea kuimarisha Muundo wa Wizara yetu, ili kuhakikisha kwamba vijana walioko mpaka ngazi ya chini kabisa na wenyewe pia wanafaidika na kupata taarifa kwa wakati ili na wenyewe waweze kutumia fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kujifunza, kutokana na yale ambayo tumeanza kuyafanya sasa, na kutokana na masomo tunayoyapata na michango yenu, tutaendelea kuboresha namna bora ya kuwafikia vijana wa nchi hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea ushauri mzuri sana kutoka kwa Mheshimiwa Yunus, hasa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu. Ninapenda kukiri sera yetu ya maendeleo ya vijana kipengele cha 3.13 kinazungumza katika ukurasa wa 33 kuhusiana na eneo mojawapo la msingi ni kushughulika na makundi maalum hasa ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea maoni aliyoyatoa, tutaenda kuyaboresha na kuaona namna bora ya kuwashirikisha kwa karibu sana katika kuhakikisha kwamba nao pia wanakuwa sehemu ya msingi na ya muhimu katika shughuli zinazohusiana na mambo ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni la kuhusiana na ukuzaji wa ujuzi kwa vijana. Ninashukuru kwa maoni ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kwamba changamoto nyingi za vijana ziko katika ujuzi ambao unaendana katika ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoeleza katika hotuba yetu, tutashirikiana na kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inashughulika na mambo ya ajira na maoni ambayo mmeyatoa, tunayapokea na sisi kama Serikali tutayafanyia kazi, tutayachakata na mwisho wa siku tutaona namna bora pia ya kuweza kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni mingi sana, nami niseme kwamba michango hii mingi mliyoitoa inaenda kutujenga na kutufanya tuwe bora zaidi katika utekelezaji wetu. Kama tulivyokuja hapa katika Bunge lililopita, maswali na maoni ya Waheshimiwa Wabunge waliyoyatoa tulikwenda kuyafanyia kazi na leo tumefika hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba yale ambayo mmeyasema pia tutaenda kuyafanyia kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha vijana na nchi hii, sawasawa na maneno ya Mheshimiwa Rais, wanaachiwa tabasamu kwa maendeleo ambayo watayapata na uwezeshaji ambao atawapatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa shukrani za mwisho, ningependa niseme jambo moja. Ni kweli kwamba changamoto za vijana ni nyingi, lakini ninaamini ni uamuzi wetu sisi kuamua, tunaziona kwa namna gani, na tunazitafsiri vipi? Kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu, vijana wa nchi hii ni asset kubwa sana katika kuhakikisha nchi hii inasogea hatua nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, katika majimbo yetu, katika shughuli zetu, tuendelee kuwafanya vijana kama sehemu muhimu pia ya kuhakikisha wanashiriki katika mambo tunayoyafanya, lakini pia tunaruhusu ujuzi wao, nguvu yao na ubunifu wao uwe sehemu ya muhimu sana katika shughuli zetu za kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni moja ilituma watu wawili kwenda kutafuta soko la viatu kwenye kisiwa. Walivyokwenda siku wamerudi kutoa ripoti, wa kwanza alivyorudi kutoa ripoti akawaambia management kwamba nimekuta katika kisiwa kile watu hawavai viatu kabisa, ina maana hakuna soko kabisa katika kisiwa kile, tuachane na habari za kwenda kupeleka viatu kuuza. Mtu wa pili alipoingia kutoa taarifa yake, akasema, naomba tujipigie makofi, kwa sababu nimeenda nimekuta hakuna watu wanavaa viatu, ina maana sisi ndiyo tutakuwa kampuni ya kwanza kuuza viatu katika kisiwa kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana na Tanzania tunapowaangalia na udhaifu walionao na changamoto walizonazo, tuwaangalie upande kama asset kwa ajili ya nchi yetu. Tutumie ujuzi wao, tutumie ubunifu wao na ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Nasi kama Wizara tunasema, changamoto zote zilizopo tutazigeuza, tutazifanya kuwa ni fursa ili kuhakikisha vijana wa Tanzania wanakuwa ni sehemu muhimu ya kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ambao wametoa mchango wao mzuri na ushauri wao wa mara kwa mara ambao umetusaidia pia kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuboresha kazi zetu pia. Pia, kwa namna ya kipekee ninawashukuru Wabunge hasa wanaotokea katika kundi la vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri wa mara kwa mara, wakichangia, na pia kutoa maelekezo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, ninaomba nichukue fursa hii kuwashukuru Mawaziri wenzangu ambao nao pia wamekuwa ni nguzo muhimu ya kunishauri na kunisaidia pale ambapo ninahitaji kuongozwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee sana, ninaomba nitoe shukrani zangu kwa Wabunge wote ambao tumejadili bajeti hii, wale waliozungumza, wale waliotuma michango yao kwa maandishi, wale waliotuma message na wale ambao hata wataongea na kunishauri baada ya hapa, nimepokea michango yenu, nimeielewa michango yenu na nitaifanyia kazi kwa maslahi mapana ya nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaomba kutoa hoja. (Makofi)