MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, niwashukuru sana wizara hii kwa kutupatia mnara katika Kata ya Tandangongoro. Tandangongoro sasa inazungumza; je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Jimbo la Lindi, hususan katika maeneo ya Kata ya Chikonji, Kitumbikwela, Mbanja na Rasbura?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Lindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yetu tunatekeleza mpango wa miaka mitano wa kujenga minara katika mikoa na wilaya zote nchini ikiwemo Jimbo la Lindi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wetu huu tutafika katika jimbo lake na tutafanya kama anavyoomba kujenga minara ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF kutuma wataalamu katika jimbo hili kufanya tathmini ya uhitaji wa minara katika jimbo lake ili tuingize katika mpango wetu wa miaka mitano wa ujenzi wa minara nchi nzima. Nakushukuru.