Answers to Primary Questions by Hon. Switbert Zacharia Mkama (11 total)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:-
Je, upi mpango wa Serikali kupunguza gharama za vifurushi kwa Kampuni zote za simu?
WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa vile nami ni mara yangu ya kwanza, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa msaidizi wake kama Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ninapenda niahidi kwamba nitafanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa kwa weledi kwa nguvu zangu zote na akili yangu yote.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu kwa wananchi. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi zake za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha huduma za simu, intaneti na data zinakuwa rafiki kwa wananchi.
Mheshimiwa Spka, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na:-
(i) Kusimamia ushindani wa haki miongoni mwa Kampuni za simu ili kuchochea ubunifu na upatikanaji wa vifurushi vya gharama nafuu vinavyokidhi uwezo wa wananchi;
(ii) Kufanya mapitio ya gharama na tozo mbalimbali ili kuhakikisha utozaji unazingatia gharama halisi za huduma na kumlinda mlaji wa mwisho;
(iii) Kuhimiza matumizi ya miundombinu ya pamoja ili kupunguza gharama za uendeshaji;
(iv) Kuendelea na Ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, minara ya mawasiliano maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara pamoja na ujenzi wa vituo vya kuhifadhi data. Hatua hii inachangia kushuka kwa gharama za huduma, hususan intaneti ya faiba majumbani na maofisini.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko na kuchukua hatua stahiki za kisera na kikanuni ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu na sekta inaendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijiti nchini.
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga mnara wa mawasiliano katika Vijiji vya Kazamoyo, Imani na Kilimani katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Fadhili Sandali Chilombe, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka minne jumla ya minara 1,041 imejengwa na inatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi. Kati ya minara hiyo, minara 758 imejengwa kupitia Mradi wa Tanzania Kidigitali ambao ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais, tarehe 13 Mei, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na jitihada za kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyosalia ambapo tarehe 5 Desemba, 2025 mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 201 ilisainiwa na utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2027.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Serikali kupitia UCSAF imepanga kufikisha huduma hizo katika maeneo mengine 280, yakiwemo maeneo ya kimkakati kama vile reli ya kisasa, hifadhi za Taifa, barabara kuu na maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zake na makampuni ya simu, inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Miaka Mitano (2025 – 2030) wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu wenye lengo la kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Lukumbule ina minara minne ya mawasiliano iliyojengwa na Makampuni ya Simu ya VIETTEL (mnara mmoja) na TTCL (minara miwili) pamoja na mnara wa Helios Towers Tanzania ambao Vodacom, Airtel na Honora wanautumia kwa pamoja kwa kuweka vifaa vyao vya mawasiliano. Aidha, kutokana na changamoto ya mawasiliano katika Kata hiyo, Vijiji vya Kazamoyo na Imani vimejumuishwa katika mradi wa mawasiliano vijijini, awamu ya tisa unaotekelezwa na Wizara. Usanifu wa minara katika vijiji hivyo umekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema Februari, 2026 na kukamilika mwishoni mwa Mei, 2026, ambapo wananchi wataanza kunufaika na huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Kilimani kitapata mawasiliano kupitia mnara wa Kazamoyo mara utakapokamilika. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Je, lini changamoto ya Mawasiliano Jimbo la Tabora Mjini Kata za Ikomwa, Ndevelwa, Ntalikwa, Kabila, Kalunde na Itetemia itamalizika?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kupitia UCSAF na watoa huduma wa Mawasiliano ilifikisha huduma za mawasiliano katika Kata husika kama ifuatavyo: Kata ya Ikomwa (Airtel, Vodacom na Halotel), Kata ya Ndevelwa (Halotel), Kata ya Ntalikwa (Airtel), Kata ya Kabila (Honora, Airtel na Halotel), Kata ya Kalunde (Honora, Vodacom, Airtel na Halotel) na Kata ya Itetemia (Halotel).
Mheshimiwa Spika, Kata zote sita zimefikiwa na watoa huduma za mawasiliano kama nilivyotangulia kuwataja kwa kuzijengea minara ambayo imekamilika na inafanya kazi. Kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali lake kwa kuonyesha kuna tatizo la Mawasiliano, Wizara kwa kushirikiana na UCSAF na Watoa Huduma wa Mawasiliano itatuma wataalam katika Jimbo la Tabora Mjini ili kufanya tathmini ya kina ya hali ya mawasiliano kwa lengo la kujua tatizo lililopo.
Mheshimiwa Spika, upo uwezekano wa kutokea tatizo la kupatikana kwa mawasiliano ya uhakika katika baadhi ya maeneo hata kama minara ya mawasiliano ilishajengwa katika maeneo hayo kwa sababu kama vile ongezeko la watu, kukua kwa shughuli za kiuchumi pamoja na jiografia ya eneo husika. Pia, sababu nyingine ni kuanzishwa kwa makazi mapya katika maeneo ambayo awali hayakuwa na wakazi, hivyo kuongeza uhitaji wa kujengwa minara zaidi au kuboreshwa kwa minara iliyopo.
Mheshimiwa Spika, tathmini itakayofanyika itatoa suluhisho sahihi, kama ni kuongeza nguvu ya mitambo katika minara iliyopo au kujenga minara mipya. Iwapo suluhisho ni ujenzi wa minara mipya, Kata husika zitajumuishwa katika miradi itakayotekelezwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Aidha, kupitia Mradi wa Awamu ya 11 utakaotangazwa mwishoni mwa mwezi Februari, Kata ya Ndevelwa, Kijiji cha Itulu utajengwa mnara wa mawasiliano.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga minara ya simu katika Kata za Kikolo na Kagugu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu nchini, ilifanya tathimini katika Kata ya Kikolo inayojumuisha Vijiji vya Kikolo, Njomlole, Uzena na Luhehe na kukijumuisha Kijiji cha Kikolo katika Mradi wa Mawasiliano vijijini awamu ya tisa unaosimamiwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambapo mtoa huduma ambaye ni Shirika la Mawasiliano Tanzania - TTCL anajenga mnara katika kijiji hicho na utekelezaji wa ujenzi wa mnara huo unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Kagugu inayoundwa na Vijiji vya Kagugu, Makunguru, Mtetema, Makatani na Maganagana, Serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote - UCSAF itafanya tathmini katika kata hii ili kupata mahitaji halisi ya huduma za mawasiliano na kuyaweka maeneo yatakayobainika kuwa na uhitaji katika mpango mkakati wa ujenzi wa minara kwa mwaka 2025/2030.
MHE. PROF. PIUS Z. YANDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Chuo cha TEHAMA Wilayani Buhigwe ili kutekeleza ahadi ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Pius Zebhe Yanda, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imewezesha upatikanaji wa eneo la ujenzi wa chuo lenye ukubwa wa ekari 155 katika Kijiji cha Songambele, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe. Pamoja na hiyo Serikali tayari imekamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya tathmini ya gharama ya ujenzi wa chuo ambapo inakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi bilioni 113 kitahitajika kukamilisha ujenzi husika. Kwa sasa Serikali inaendelea na utaratibu wa kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuanza ujenzi wa chuo husika.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: -
Je, upi mpango wa Serikali wa kuimarisha Mawasiliano ya Simu kwenye Vijiji vyenye changamoto ya huduma hiyo Mkoa wa Kaskazini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Tamima Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilitekeleza mradi wa kimkakati wa kufikisha mawasiliano katika Shehia 38 zilizokuwa na changamoto ya mawasiliano ambapo jumla ya minara 42 ilijengwa kwa kushirikiana na mtoa huduma Honora/YAS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya minara hiyo Mkoa wa Kaskazini Unguja ulinufaika kwa kujengewa Minara 12 ambapo mradi huu ulikamilika kikamilifu na kwa sasa wananchi wananufaika na huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zilizofanyika kama nilivyotangulia kuzitaja, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imebaini kuwepo kwa changamoto za Mawasiliano katika Shehia ya Mafufuni, iliyoko Wilaya ya Kaskazini “B” pamoja na Shehia ya Tazari iliyoko Wilaya ya Kaskazini “A” ambapo kwa upande wa Shehia ya Mafufuni tayari imejumuishwa katika Mradi wa Awamu ya Kumi ambao mikataba yake ilisainiwa tarehe 5 Disemba, 2025. Pia Kampuni ya YAS inatarajiwa kujenga mnara katika Shehia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Shehia ya Tazari pamoja na maeneo mengine ya pembezoni ya Mkoa wa Kaskazini Unguja yatajumuishwa katika awamu zinazofuata.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka Mawasiliano ya simu katika Vijiji vinne vya Kata za Nyamigogo na maeneo mengine yenye uhitaji Wilayani Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mhandisi Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imejenga Minara 11 ya Mawasiliano katika awamu mbalimbali (Awamu ya Kwanza A, Awamu ya Pili B na Awamu ya Nne B) katika kata kadhaa zilizopo katika Wilaya ya Biharamulo, ikiwemo Biharamulo Mjini, Kalenge, Kaniha, Lusahunga, Nemba, Nyabusozi, Nyakahura, Nyarubungo na Ruziba.
Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijiti Awamu ya Kwanza Minara 13 imejengwa katika kata 13 na tayari inatoa Huduma za Simu na data kwa teknolojia za 2G, 3G na 4G. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mnara mmoja katika Kata ya Lusahunga chini ya Mradi wa Mawasiliano Vijijini Awamu ya 10, unaotarajiwa kuhudumia Kijiji cha Kikoma na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto ya huduma za mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Biharamulo, hususan katika Kata za Nyamigogo, Runazi, Nemba na Nyakahura.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia UCSAF imebaini uwepo wa changamoto ya Huduma za Mawasiliano katika Vijiji vya Nyamigogo, Kagoma, Kasozibakaya, Songambele na maeneo mengine katika Vijiji vya Migango, Kaluguyu na Busiri. Kwa sasa, upembuzi yakinifu unaendelea ili kuyaingiza maeneo hayo katika Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Minara wa Mwaka 2025 – 2030.
MHE. DICKSON N. KUTEVELE K.n.y. MHE. JESCA J. MAGUFULI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vijana wanapata ujuzi sahihi na kunufaika kupitia Akili Mnemba (AI)?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca John Magufuli, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi na taasisi za Kimataifa kuhakikisha vijana wanajengewa ujuzi sahihi wa matumizi ya akili mnemba. Vilevile, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa matumizi salama ya Teknolojia ya akili mnemba unaolenga kukuza ujuzi kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi vyuo vikuu ili kujenga hazina ya wataalamu mahiri nchini. Aidha, Serikali kupitia Tume ya TEHAMA imepitia mitaala 110 ya vyuo vikuu 32 vyenye Mlengo wa TEHAMA ili kuhakikisha vyuo hivyo vinajumuisha Moduli za Akili Mnemba, hatua inayolenga kuendana na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kuzalisha vijana wenye ujuzi wa teknolojia ya kisasa ikiwemo akili mnemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Akili Mnemba utahusisha uanzishwaji wa vituo vya ubunifu nchini katika Mikoa ya Lindi, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, na Zanzibar. Sambamba na vyuo hivyo, Serikali inakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijiti katika eneo la Nala – Jijini Dodoma, ambayo itajikita katika utoaji wa mafunzo kwa teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili mnemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ubunifu, kuimarisha ushindani wa Kimataifa na kuhakikisha manufaa ya teknolojia ya akili mnemba na teknolojia nyingine zinawafikia wananchi wote kwa maendeleo jumuishi na endelevu.
MHE. THOMAS M. KITIMA aliuliza: -
Je, lini Serikali itahakikisha kila kijiji nchini kinapata mawasiliano ya kimtandao na kuwepo kwa minara ili kurahisisha mawasiliano hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Thomas Mngoto Kitima, Mbunge wa Jimbo la ikungi Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa huduma za mawasiliano ya uhakika katika kila kijiji nchini kama msingi wa kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hasa katika zama hizi za uchumi wa kidijiti. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Sekta Binafsi, imeendelea kupanua miundombinu ya mawasiliano ikiwemo ujenzi wa minara ya simu, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo bado kuna changamoto ya mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa Mpango Mkakati Mahsusi wa Ujenzi wa Minara kwa Kipindi cha Miaka Mitano (2025 – 2030). Mpango huu unalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vijiji vyote nchini vinapata huduma za mawasiliano mbadala ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya mawasiliano na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mpango huu, mwezi Disemba, 2025 Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, ilikamilisha Mradi wa Awamu ya Nane ya Ujenzi wa Minara 758 nchini. Utekelezaji wa awamu ya tisa ya ujenzi wa minara 636 unaendelea na utakamilika mwezi Disemba, 2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, UCSAF inaendelea na awamu ya 10 ya ujenzi wa minara 287 ambayo mikataba yake ilisainiwa Disemba, 2025. Hatua hii inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za Mawasiliano katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na kuboresha huduma kwa wananchi.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza changamoto ya Mawasiliano kwa kujenga Minara Kata za Heru Ushingo, Kagerankanda na Asante Nyerere - Kasulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Edibily Kazala Kinyoma, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote – UCSAF ilikamilisha ujenzi wa Mnara Mwaka 2014 kupitia Kampuni ya Honora au (Yas Tanzania) kwa ajili ya kuhudumia Vijiji vya Seruhemebe na Heru vilivyopo katika Kata ya Heru Ushingo. Aidha, katika Kata za Kagerankanda, UCSAF ilijenga Mnara mwaka 2021 katika Kijiji cha Mvinza kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika Kata ya Asante Nyerere, UCSAF ilikamilisha ujenzi wa mnara mwaka 2025 kupitia Kampuni ya Vodacom Tanzania katika Kijiji cha Sogeeni Kwiliba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada nilizozitaja awali, Serikali kupitia UCSAF itatuma wataalamu kwenda Kasulu Vijijini katika Kata husika kufanya tathmini ili kujua mahitaji halisi na hatimaye kuviingiza vijiji vyote vyenye changamoto ya mawasiliano katika miradi itakayotekelezwa na UCSAF hususan katika Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Minara wa Mwaka 2025 – 2030.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano Halmashauri ya Mji Ifakara hasa Ikwambi, Mang’ula B na Kanyenja?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza miradi ya kuboresha Huduma za Mawasiliano katika Jimbo la Kilombero. Katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, mnara wa mawasiliano wa mtoa huduma Honora (Yas) ulijengwa Kata ya Signal katika Kijiji cha Sagamaganga na unatoa huduma katika Vijiji vya Signal, Sululu na Sagamaganga. Aidha, kupitia awamu hiyo Kampuni ya Honora ilijenga mnara katika Kijiji cha Mhelule, Kata ya Mang’ula, unaohudumia vijiji vya Kanyenja, Mhelule, Mikoleko, Mang’ula A na Mang’ula B.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mnamo tarehe 8 Aprili, 2026, UCSAF ilifanya tathmini katika Vijiji vya Mang’ula B, Kanyenja na Kitongoji cha Ikwambi na kubaini kuwa Kijiji cha Kanyenja kilijumuishwa katika Mradi wa Mawasiliano ya Simu vijijini wa minara 636 ambapo mnara huo ulijengwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Kijiji cha Kanyenja na unatoa huduma za teknolojia ya 2G na 4G. Aidha, Kijiji cha Mang’ula B na Kitongoji cha Ikwambi vilibainika kuwa na changamoto za mawasiliano hivyo UCSAF itayajumuisha maeneo hayo kwenye miradi ya mawasiliano ya simu ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo katika Kijiji cha Mang’ula B na Kitongoji cha Ikwambi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.