Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haji Kombo Mdowe (2 total)

MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukipandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kutokana na ukuaji wa mji huo kiutalii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi na kuuagiza kwamba unapaswa kuwasilisha hoja yao ya kutaka kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja, ambayo itashauri na kutoa mapendekezo yake kwenda Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo na ushauri wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar yatawasilishwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji wa kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi iwapo vigezo vya kiulinzi, kiutawala na miundombinu vinavyotakiwa vitakuwa vimekamilika.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga ukuta katika Fukwe za Bahari ya Nungwi Kiungani ili kuzuia bahari kuingia katika makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mmonyoko wa fukwe unaosababisha bahari kuingia katika makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hili, Serikali imefanikiwa kupata ufadhili kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) ambapo jumla ya dola za Marekani 500,000 sawa na takribani shilingi bilioni 1.3 za Kitanzania zimetolewa na mfuko husika kwa ajili ya kutekeleza mradi katika mwaka wa fedha 2025/2026 na 2026/2027 wa kuimarisha utayari wa Kisiwa cha Zanzibar kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu utaanza mara baada ya tathmini ya athari hizo kukamilika. Ninaomba kuwasilisha.