Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Haji Kombo Mdowe (2 total)

MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa ruhusa yako. Kwanza ninaomba niishukuru na kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya katika nchi yetu. Pia ninashukuru kwa majibu yao ambayo wamenipa, kwa sababu majibu haya yametoa mwongozo mzuri katika suala letu hili. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza katika jambo hili: -

(a) Je, ni vigezo gani vya kiulinzi, kiutawala na kimiundombinu vinavyotakiwa kukamilika ili kituo cha Polisi kiweze kupandishwa hadhi?

(b) Je, ni jukumu la nani hasa kukamilisha vigezo vya kiulinzi na kimiundombinu katika vituo vya Polisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Jimbo la Nungwi kwa maswali yake mawili ya nyongeza, ambayo ni muhimu sana. Ninapenda kumfahamisha Mheshimiwa Mdowe kwamba, vigezo vya kimiundombinu ni madaraja ya majengo ya Jeshi la Polisi ambayo yapo kwenye daraja la C1, C, B na E, kutegemeana na aina au eneo linalotaka kujengwa kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ombi ambalo wamewasilisha wao kwa Kituo cha Polisi cha Nungwi, kwa sasa kipo kwenye daraja C. Kwa hiyo, kinaomba kupandishwa hadhi kwenda kwenye daraja B. Ili kufikia kiwango cha daraja B, basi ni lazima miundombinu hiyo ya jengo la kituo cha Polisi iwe imekidhi vigezo vya daraja B la vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika vigezo vya kiulinzi ni kuangalia parameter za eneo ambalo linaombewa kupandishwa daraja la eneo hilo. Kwa mfano, hivi sasa Jeshi la Polisi linayo maeneo ambayo yamepewa hadhi ya mikoa, lakini kiutawala yapo hadhi ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano halisi ni kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambao umepewa kanda maalum, na ndani yake zile wilaya zimepewa hadhi ya mikoa. Hiyo inatokana na hali ya kiutawala, na pia mahitaji ya kiulinzi katika eneo la Mkoa husika wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa vigezo hivyo, watakapowasilisha maombi yao kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa maana ya Kamati ya Usalama ya Wilaya, itaweza kuchakata na kutathmini hali ya vigezo vyote vitatu kama vitakuwa vimefikiwa na kushauri ipasavyo kwenye ngazi inayofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kwamba, ni nani ambaye ana jukumu hilo, nilieleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, ninauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi kwamba uwasilishe pendekezo hilo kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa maana ya Kamati ya Usalama ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Nungwi wanataka kujua, ni lini tathmini hiyo itakamilika? Kwa sababu kuanzia mwaka wa fedha wa 2023/2024 majibu ya Serikali yalikuja kuhusu tathmini. Ninanukuu; Waziri wa wakati huo alijibu: "Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar imetenga fedha jumla ya shilingi milioni 650..."

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kombo, utakuwa kama unachangia, uliza tu swali.

MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa tathmini hiyo itakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuwa mbaya. Sasa tunataka kujua sisi kama wananchi wa Nungwi, ni zipi hatua za dharura ambazo Serikali zitaichukua kukabiliana na hali ile pale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ameshafika ofisini kwetu takribani mara tatu au mara nne kwa ajili ya kufuatilia jambo hili. Hata jana alikuwepo ofisini kwetu. Tayari imeshafanyika tathmini ya awali kwa Zanzibar yote, na tumebaini maeneo karibia 148 ambayo yameathirika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo maeneo 148, maeneo 123 yako Pemba na maeneo 25 yako Unguja. Serikali baada ya kufanya tathmini hiyo imeanza kutekeleza mradi wa mabadiliko ya tabianchi kukabiliana nayo katika ngazi ya jamii. Tayari tumeshaanza kwa awali na halmashauri 11 kule Zanzibar na halmashauri 54 Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayofuata baada ya tathmini hii kukamilika, tunakwenda kufanya tathmini ya kubaini gharama kwa kila eneo ambalo limeathirika yakiwemo maeneo anayotokea Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, ametaka kujua ni hatua za dharura ambazo Serikali inachukua. Kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge Wilaya ya Kati tumebaini maeneo matatu ambayo yameathirika zaidi kuliko maeneo mengine. Maeneo hayo ni Wadi ya Cheju, Wadi ya Chakwa, pamoja na eneo la Wadi ya Ubago.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii tunayokwenda kuitekeleza kwenye bajeti ambayo Bunge hili limetupitishia, tumetenga kwa nchi nzima kwa maana ya pande zote mbili kupitia Fungu 31, zaidi ya shilingi bilioni 31 ambazo zitatekeleza miradi hii ya mabadiliko ya tabianchi kwa awamu na awamu itakapofika tutajielekeza kwenye maeneo hayo ya Cheju, Chakwa na Ubago. Ninaomba kuwasilisha.