Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Adonis Alfred Bitegeko (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Hotuba ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hasa kuhusiana na utekelezwaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha na pia kwa ajili ya Mwaka ujao wa Fedha wa 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo inafanyika. Pia Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Tunamwona Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara zake amekuwa akipambana sana kuona kama miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa jinsi ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia kwamba kupitia hali ya uchumi, uchumi wetu umekua na pato halisi la Taifa limeongezeka hadi asilimia sita kutoka tano mwaka uliopita. Kwa hiyo pato limeongezeka hadi asilimia sita kutoka 5.5%. Pia mwenendo wa mapato nao umekuwa ni mkubwa. Tumeona kwamba hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu tumeweza kukusanya trilioni 26.63. Haya ni makusanyo makubwa ukilinganisha na ambavyo yalipatikana mwaka jana kipindi kama hiki, ya trilioni 25.68. Pia hata mapato ya Serikali za Mitaa nayo yameongezeka mpaka kufikia trilioni 1.8 ambazo zimekusanywa, ambazo ni sawasawa na 64.6% ya lengo ambalo lilikuwa limepangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima nipongeze vile vile jitihada ambazo zimefanywa na Mheshimiwa Rais wetu. Tumeona kwamba amewaza kuunda tume ya kufanya mapitio na maboresho ya mfumo wa kodi hapa nchini. Hili ni jambo jema sana katika kupanua wigo wa kukusanya kodi, lakini pia wa kuondoa upotevu wa makusanyo ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nijikite Ofisi ya Waziri Mkuu hasa Sera, Bunge na Uratibu. Kwa vile mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI nitachangia eneo hili zaidi, pamoja na upande wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu inasimamia Tume ya Kudhibiti UKIMWI. Ukiangalia ni kwamba Tume hii ina jukumu la kisheria ya kutoa uongozi wa kimkakati wa shughuli za kudhibiti UKIMWI hapa nchini. Kupitia jitihada za Serikali tumeona kwamba jitihada kubwa zimefanyika na zimesababisha mpaka kupungua kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kiasi kikubwa. Pia, kupitia jitihada za Serikali dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI zimekuwa zikipatika bure na kwa wahitaji wote, hizi ni juhudi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeenda mbele zaidi, ni kwamba, ili kuziba pengo ambalo linaenda kujitokeza kutokana na kujitoa kwa shirika la kimaendeleo inaanzisha Mfuko Maalum kupitia Sheria ya Fedha Na. 11 2025, Mfuko ambao ni wa udhamini wakidhibiti UKIMWI (ATF) ili kuona kwamba fedha zinazohitajika kwa ajili ya UKIMWI zinapatikana kwa uhakika na zinakuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona, kwamba Serikali pia imeamua kuwekeza zaidi katika kiwanda au kufufua kiwanda kile ambacho kilikuwa kinazalisha dawa za VVU, dawa za ARV, Kiwanda cha TPI – Arusha. Hizi ni jitihada kubwa sana kwa Serikali ili kuona kwamba tunaongeza upatikaji wa dawa hizo nchini, pia kuzalisha ajira na kupunguza gharama za kuagiza dawa kutoka nje ya nchi. Hili ni jambo kubwa sana. Ushauri kwa Serikali ni kuona kwamba kiwanda hiki kinazalisha dawa kwa kuzingatia sheria na kanuni za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ili kuona dawa ambazo zinazalishwa zinakuwa na ubora na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) hadi kufikia Februari mwaka huu matumizi yake ya fedha katika bajeti ambayo ilikuwa imeidhinishwa ya bilioni 29.14; kwamba matumizi yake au pengine fedha ambazo zimepokelewa ilikuwa ni 36% tu ya fedha ambazo zilikuwa zimetengwa au zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha bado ni ndogo, tunaishauri Serikali kwamba iongeze kasi katika utoaji wa fedha ili yale mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI yasirudi ili yaende mbele zaidi. Kwa hiyo, ninashauri sana Serikali katika hili iangalie umuhimu kuona kwamba zile jitihada zetu tunazozifanya basi hazirudi nyuma. Kwa hiyo tunashauri sana Serikali katika hili iongeze kasi katika kutoa fedha katika kipindi hiki kilichobaki kwa mwaka huu wa fedha ili kuona kwamba kazi kubwa inafanyika katika haya mapambano dhidi ya VVU pamoja na UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho tujifunze ni kwamba kazi za uratibu dhidi ya mapambano ya UKIMWI zinafanyika na TACAIDS, lakini pia ni vyema sana kwamba matumizi ya Ofisi za Kanda za TACAIDS yakafanyika kwa kuona kwamba tunapeleka zaidi rasilimali kwenye ofisi za kanda ili zishikane ndani ya halmashauri katika kuleta msukumo zaidi katika mapambano ya Virusi vya UKIMWI pamoja na UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili ni suala muhimu sana kwamba TACAIDS wakapeleka zaidi msukumo katika ofisi za kanda ili kuona kwamba fedha nyingi zinakwenda kule na rasilimali watu katika kusaidia katika shughuli za mapambano ya UKIMWI kwa kushirikiana na ofisi za halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa bajeti ya Mwaka huu wa Fedha 2025/2026. Katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 kwenye makadirio ya TACAIDS tumeona kwamba, TACAIDS imeleta mapendekezo ya jumla kwa fedha za ndani pamoja na za maendeleo ambazo zinafikia shilingi bilioni 12.7. Kama ukiangalia ukalinganisha na bajeti iliyopita, mwaka uliopita wa fedha ni kwamba fedha hizi zimepungua kwa 56%. Zile za mwaka uliopita wa fedha ambao ndio unaendelea zilikuwa ni shilingi bilioni 29.4, lakini sasa hivi tumeshuka hadi shilingi bilioni 12.6; ni upungufu wa 56%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho tunapaswa kupata maelezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ni kwamba katika mwaka ujao wa fedha, mapendekezo ya makadirio haya tulitegemea kuona zaidi kwamba kunakuwa na bajeti au makadirio ambayo yameainishwa ya matumizi ya zile fedha za mwitikio wa UKIMWI, hizo fedha hazijaainishwa mle ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunashauri kwamba ni vizuri sana katika makadirio yakawa wazi ili kuonyesha kwamba zile fedha ambazo zinaingia kwenye Mfuko wa ATF makadirio yake tukayajua kabisa ili tujue kwa ajili ya matumizi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa TARURA baada ya hapa tunaona kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana, lakini pia kulikuwa na changamoto ya mapokeo ya fedha kwenye mwaka huu fedha. Kwa mfano, katika Wilaya yetu ya Muleba kupitia TARURA mpaka sasa hivi tumepokea 16.4% tu ya fedha ambazo zimetengwa ambazo zilikuwa ni shilingi bilioni 4.3, tunaomba sana kuwe na msukumo zaidi ili fedha hizi zipatikane zaidi ili kusaidia athari za barabara ambazo zimeharibika kutokana na athari za mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa afya jambo lingine la msingi la ushauri ni kwamba kwenye Wilaya ya Muleba kulikuwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya. Ushauri ni kwamba hospitali hii tunashukuru mpaka sasa hivi ujenzi umefika hatua kubwa. Mkataba wa ujenzi wa hii hospitali ya wilaya ulikuwa na thamani ya shilingi bilioni 2.17, tuna upungufu wa shilingi bilioni 844.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tu Serikali itoe fedha hizi ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hii ya wilaya hasa ujenzi wa jengo la ICU pamoja na jengo la upasuaji pamoja na jengo la kutolea chanjo. Tunaomba pia Serikali itekeleze pengine katika bajeti hii ya mwaka huu kuona kwamba tunakamilisha ujenzi wa Zahanati ya Ilogero na Makongora katika Wilaya ya Muleba pamoja na Vituo vya Afya Izigo na Kamachumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Vituo vya Afya vya Kamachumu na Izigo vina upungufu wa wataalam hasa wataalam wa dawa za usingizi na radiolojia. Kwa hiyo, tunaishauri sana Serikali katika hili iangalie kwa sababu tayari majengo yapo tayari tunasubiri tu wataalam hao tuweze kukamilisha kufanya huduma hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho la kumalizia ni ushauri kwamba kwenye afya ya msingi ngazi ya wilaya tunashauri pia Serikali iangalie umuhimu wa kuongeza wataalam wa dawa (wafamasia) ili waweze kutoa huduma inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie kwa kuomba kwamba Serikali iweke kipaumbele katika kukamilisha ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya ili huduma ya afya iweze kutolewa kwa ubora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ambayo kwa dhahiri ameonesha kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona dhamira yake ya dhati kabisa kuwezesha wananchi wengi kupata huduma ya maji mpaka sasa hivi imefikia 85.2% kutoka 70.1% mwaka 2021 wakati anaingia madarakani. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa sisi wakazi wa vijijini kuona kwamba huduma hiyo imeimarika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri wake na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Mimi kama Mbunge wa Muleba Kaskazini nimekuwa nikipata ushirikano mkubwa sana kutoka kwao hasa pale ninapofuatilia miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana, kwa kuwa katika miaka mitano iliyopita Jimbo la Muleba Kaskazini lilipata miradi mitano ya maji ambayo yamesaidia sana kuimarisha huduma za maji na kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji mpaka kufikia 81% kutoka 74%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na mafanikio haya, sisi katika Jimbo la Muleba Kaskazini bado tuna miradi miwili mikubwa ya maji ambayo tunaisubiri. Tuliahidiwa katika mwaka huu wa fedha miradi hiyo itakuwa imetekelezwa (mradi wa maji wa Iroba na mradi wa maji wa Makongora).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miradi ambayo wananchi wa Jimbo la Muleba Kaskazini wamenituma niiombe Serikali iweze kuitekeza miradi hii, kwani itasaidia sana kuleta huduma za maji katika wakazi takribani 9,000 katika maeneo hayo na maeneo ya jirani ya vijiji hivyo. Pia tunatarajia kwamba katika mwaka ujao wa fedha tutapata visima vitatu ambavyo vitasaidia sana katika kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Muleba Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi ambalo ninaomba niliseme hapa leo ni kwamba katika miradi mitano ambayo imetekelezwa katika Jimbo la Muleba Kaskazini, tuna mradi mmoja wa Kagoma ambao utekelezaji wake umefikia 96% bado asilimia nne kukamilika, lakini bado mkandarasi anadai fedha shilingi milioni 119 ili kukamilisha mradi huo. Tunaomba sana Serikali isimamie ili mkandarasi huyu aweze kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali ya kuleta maombi hayo ya Jimbo la Muleba Kaskazini, ninapenda pia kushauri Serikali kwamba ukiangalia dira yetu ya 2050 imetoa kipaumbele sana katika sekta ya binafsi kuweza kuchangia katika kuleta mafanikio ya maendeleo. Ninaamini kwamba maji pia ni uchumi. Ninaamini kwamba ni wakati mwafaka sasa hivi Serikali ikafungua milango kuruhusu sekta binafsi iweze kushiriki katika kutoa huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la msingi sana, tumeona mafanikio kule Tanga kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge aliyetangulia kwamba imesaidia sana uuzaji wa hatifungani. Ninashauri kwamba sisi tufungue pia fursa zaidi kwa wawekezaji waingie kuwekeza katika sekta ya maji ili kusaidia sana katika kuongeza zaidi miradi mingine ya maji, lakini pia kufadhili miradi ya maji. Tumeona pia katika upande wa barabara, Samia Infrastructure Bond imesaidia sana katika kuongeza uwezo wa Serikali katika ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaamini kabisa sekta binafsi ikishirikishwa, basi tutaweza kufika mbali katika kufanikisha mipango yetu ambayo kimsingi itasaidia sana maendeleo yetu ya sekta ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili pengine ni jambo la jumla la Kitaifa, nimeona kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2025/2026 kwamba ilipangwa miradi 1,318 vijijini, lakini mpaka tunafikia mwezi wa nne ni miradi 54 tu imeshatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Serikali iongeze nguvu zaidi katika kukamilisha miradi mingine 992 ili tuweze kupata huduma zaidi ya maji na kufikia yale malengo kusudiwa ya kuona kwamba kila kijiji kinapata huduma ya maji ifikapo mwaka 2030. Ninaamini kabisa kwamba kwa mpango kabambe wa Serikali ambayo imeuandaa, tutaweza kufikia yale malengo tarajiwa ya kutoa huduma za maji kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninapenda kutumia fursa hii kwa kuwa ninahitimisha pia mchango wangu, ni kwamba ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Muleba Kaskazini kwa jinsi wanavyoniamini. Nami ninapenda kuwahakikishia kwamba chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi pamoja na madiwani tutapambania kuona kwamba wanapata maji ya uhakika na usalama katika vijiji vyote.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bitegeko, ahsante sana.

MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja.