Supplementary Questions from Hon. Dr. Yahaya Esmail Nawanda (4 total)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga minara katika Kata za Mtunguru, Mkwedu, Chilangala pamoja na Mikumbi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Nawanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Wizara inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Minara 280 katika bajeti hii na katika bajeti ijayo tutatekeleza tena mradi wa kujenga minara mingine 280 ambayo katika mradi huo Kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge nazo tutazipatia kipaumbele. (Makofi)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Mfuko wa Barabara umekuwa unagharamia zile barabara ambazo ziko rasmi na umekuwa unajenga Barabara kutoka Mkoma Sokoni hadi Lihanga. Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha maalum kwa ajili ya kumalizia sasa kutoka Lihanga mpaka Chikalule, ambayo ni kama kilometa moja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Barabara ya Mchemo hadi Mahuta imekuwa ina changamoto kubwa sana. Je, ni lini Serikali sasa itapandisha hadhi ya barabara hii kutoka udongo kwenda kutengenezwa kuwa barabara changarawe ili wananchi wa maeneo haya waweze kupita kwa usalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninatambua kuwa jiografia ya Mji wa Newala Vijijini ina miinuko mikali na barabara hii ambayo imetajwa na Mheshimiwa Mbunge, Barabara ya Chikalule kwenda Makao Makuu ya Kitangali wananchi wetu kwenye maeneo yale wakati mwingine wamelazimika kupitia Lindi ili kufika makao makuu ya wilaya. Kwa kutambua umuhimu huo pia zipo taasisi kwenye eneo hilo, ikiwemo Shule yetu ya Msingi Chikalule ambayo inafanya vizuri sana; na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wale.
Mheshimiwa Spika, Serikali itakwenda kuijenga barabara hii kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Tumepanga, kwenye Mwaka wa Fedha unaofuata wa 2026/2027 tutaweka fedha kwa ajili ya barabara hii.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, kwenye swali lake la pili ameitaja Barabara ya Mchemu hadi Mahuta na Mheshimiwa Nape wakati ameanza kuuliza alitaka kuitaja barabara hii. Tunatambua kuwa barabara hii imebeba uchumi mkubwa wa zao la korosho kwenye maeneo ya Newala pamoja na Tandahimba na ina urefu wa kilometa 17.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha ujao ninawaelekeza mkoa waiangalie barabara hii vizuri ili waihuishe kwenye mipango yetu ya kitaifa na hatimaye iweze kujengwa na kuinua uchumi na kufungua uchumi wa Wananewala pamoja na Wanatandaimba.
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara zote zilizopo katika Mji wa Kitangari? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara za lami kutoka katika Kijiji cha Maputi hadi Ndanda, na pia, katika Kijiji cha Chiwonga, Pacha Nne, hadi Nanganga? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshaanza kujenga barabara zilizopo katika Mji wa Kitangari. Tumeanza na barabara ya kutoka kwa Mzee Lada mpaka kwa Mzee Twalibu, ambayo ina urefu wa kilomita moja, na siyo tu kwamba tumeishia kuijenga, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amehakikisha barabara hiyo imewekewa taa pia, na inatumika.
Mheshimiwa Spika, kadiri fedha zitakavyoendelea kupatikana tutaendelea na ujenzi wa barabara za mji huo. Barabara ya kutoka Msikiti Mkubwa kwenda kituo cha afya karibu na stendi, na vilevile Barabara ya Mnakute hadi Halmashauri na Barabara ya VETA hadi Nachirindima.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Barabara ya Maputi – Ndanda, Chuonga – Pacha Nne kwenda Mkongi hadi Nanganga njia panda ya kwenda Ruangwa, Serikali itatekeleza kama ilivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025/2030. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia barabara hizi kwa umakini mkubwa. (Makofi)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mradi wa Makonde ni mradi mkubwa sana ambao Serikali imekubali yenyewe kwa kusema jumla ya watu 600,000 wanakwenda kunufaika katika Wilaya za Newala, Tandahimba pamoja na Mtwara. Hivi tunapozungumza mkandarasi hayupo site, na alishawasilisha certificate za madai ya jumla bilioni 11.2. Je, ni Serikali italipa fedha hizo ili mkandarasi aendelee na shughuli yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika mradi huo wa Makonde kuna miradi miwili pacha, Mradi wa Lukohe pamoja na Mradi wa Malatu, miradi hii yote kandarasi CTC Construction Company amefanya kazi na amewasilisha jumla ya certificate tatu zenye jumla ya shilingi 6,000,000,000 na hayupo site. Je, Serikali ina kauli gani ya kuhakikisha mkandarasi anarudi ili miradi hii iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Yahya Esmail Nawanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika jimbo la Newala Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kabisa, kwamba mradi huu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, ni mradi mkubwa na ni wa kimkakati. Asili yake ni mradi uliojengwa mwaka 1954, ambapo ukarabati wake ulianza mwaka 2022. Kuna zaidi ya matenki manne ambayo yatajengwa Newala Mjini, Newala Vijijini, Tandahimba pamoja na Nanyamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tayari fedha ambazo mkandarasi ameshalipwa zaidi ya bilioni 20.7 ambapo mradi umefikia 40% kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu pia kwamba, mkandarasi anadai takribani bilioni 10.8 ambazo tayari zipo kwenye mchakato na zitakapokamilika mkandarasi atalipwa, ambaye ni ECC. Tunaamini kwamba mradi huu unatakiwa ukamilike na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mradi wa pili ambapo mkandarasi pia naye anadai; kama ambavyo nilijibu hapa kuwa uwepo wa madai ya wakandarasi ni ishara tosha kwamba Serikali ina dhamira ya kweli kuhakikisha kwamba inatatua changamoto za wananchi na ndiyo maana tumeamua kuwekeza miradi mingi ili kuhakikisha kwamba wananchi wanatatuliwa changamoto zao, wakiwemo wananchi wa Newala Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, hizi bilioni sita tutahakikisha kwamba mkandarasi analipwa ili arudi site na kuhakikisha kwamba anaendelea na mradi na kuukamilisha kwa wakati, ahsante sana.