Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Daniel Godfrey Chongolo (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza kuchangia ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniamini na kunipa heshima ya kusimamia sekta muhimu ya kilimo nchini. Nimhakikishie imani hii itazaa imani.

Mheshimiwa Spika, pia niwashukuru Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa miongozo ambayo wanaendelea kutupatia sisi wasaidizi wao. Nitakuwa ni mchoyo wa fadhila nisipokushukuru wewe binafsi kwa namna unavyotuongoza ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja. Ninaunga mkono hoja kwa nini? Kwa sababu, kwanza Waziri Mkuu ameonesha kwa kina katika mapendekezo ya bajeti inayohusu ofisi yake kuwa, dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, ninasema ameonesha kwa kina kwa namna gani? Kwanza, kabla ya kuiwasilisha kwa muda mfupi amefanya kazi kubwa sana, ameshatembea katika mikoa mbalimbali nchini na huko ametufundisha wasaidizi wake namna ya kuwajibika na changamoto za wananchi moja kwa moja kwa wananchi kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, leo ukienda kwenye maeneo ambayo tayari Waziri Mkuu amepita na sisi askari wake wa mwavuli Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao tuliambatana naye kwenye maeneo kadhaa unaona tabasamu ambalo Rais aliliahidi kwa Watanzania likianza kuonekana.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wabunge 27 walitoa hoja mbalimbali zinazohusu sekta ya kilimo nchini, nami ninawashukuru sana Wabunge wote kwa michango yenu. Tumeichukua michango yote na niwahakikishie kwamba kupitia bajeti ya Wizara ya Kilimo nitaonesha namna yale ambayo wameyachangia hapa yanavyokwenda kutafutiwa majawabu.

Mheshimiwa Spika, maeneo makubwa yaliyokuwa yamegusiwa ni manne, eneo la kwanza kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni kuhusu pembejeo za kilimo, kwa maana ya mbolea, mbegu na viuatilifu. Eneo la pili lilikuwa ni umwagiliaji na tatu lilikuwa ni masoko na uongezaji wa thamani ya mazao, eneo la mwisho ni ushirika na mitaji inayotokana na vyama vya ushirika, lakini pia benki zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa pembejeo za kilimo, ushauri wa Wabunge tumeuzingatia sana, niwahakikishie tutaendelea kuimarisha utoaji wa ruzuku za pembejeo za kilimo nchini na kuweka mifumo itakayowezesha pembejeo za kilimo kuwafikia wananchi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pembejeo za kilimo ndiyo zinazojenga msingi wa kutafuta matokeo ya kilimo chenyewe na wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakisema kilimo ni uti wa mgongo, lakini ukiangalia uti wa mgongo ni sehemu ya mgongo, kuita kilimo ni uti wa mgongo ni kupunguza ukubwa wa kilimo chenyewe, kwa sababu uhalisia kwa kweli kilimo ndiyo mgongo wenyewe.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ijayo ya Wizara ya Kilimo maeneo ya msingi ambayo tumeyapa kipaumbele na tutayapa kipaumbele ni kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Pia, kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya fedha za ruzuku ambazo zimekuwa bado hazijakamilika kulipwa kwa mawakala, lakini pia na kwa suppliers wa mbolea na pembejeo nyingine. Pia kupanua wigo wa upatikanaji wa pembejeo karibu na wananchi, kwa sababu tukiwasogezea karibu tutawasaidia kupunguza usumbufu wa kufuata kwenye maeneo ya mbali na kuongeza gharama.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ni kuhakikisha tunawekeza kwenye upatikanaji wa mbegu ili kupunguza changamoto ya mbegu feki. Katika hili moja ya kazi kubwa ambayo tumefanya ni kuimarisha na kuiongezea uwezo taasisi yetu ya mbegu ya ASA ili iweze kutumia mashamba yake kwa kiwango kikubwa kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Spika, katika hili tumetengeneza mfumo wa contract farming. Mwanzo ASA alikuwa anatafuta fedha kwa ajili ya kwenda yeye mwenyewe kulima na changamoto alikuwa akilima mvua ikiwa chache au kukiwa na changamoto yoyote, mavuno yakiwa machache matokeo ya mbegu yatakuwa hivyo hivyo mwishoni. Ili kuepukana na hilo sasa tumejielekeza kuisukuma ASA kutoa mashamba kwa wakulima binafsi na kuingia nao mkataba, wao walime halafu waingie mkataba wa kuuziana mbegu na ASA, ili ASA kwa bajeti yake ya mbegu aweze kupata asilimia 100 ya mbegu alizozipangia kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, hilo linalenga kuhakikisha matokeo yake ya upatikanaji wa mbegu kwa wananchi, tena mbegu bora yanaongezeka na kuwaondoa wananchi kwenye changamoto ya kupata mbegu maarufu feki.

Mheshimiwa Spika, moja ya eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge waligusia ni kuhusu nafaka, ununuzi wa nafaka na hasa mahindi ambapo kila msimu tumekuwa tukinunua kupitia taasisi yetu ya NFRA. Tuwahakikishie mwaka huu tumefanikiwa kununua mahindi yenye thamani msimu uliopita shilingi bilioni 95.3 na mpaka sasa tumeshafanikiwa kulipa shilingi bilioni 93.1 bado bilioni mbili kasoro kidogo ambayo mpaka mwezi huu mwishoni tarehe 30 tutakuwa tumekamilisha kulipa ili wakulima waendelee kujibidiisha kwenye kilimo na siyo vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, kikubwa niwahakikishie Wabunge kwamba dhamira ya Wizara ya Kilimo na Serikali ni kuhakikisha inaendeleza kilimo kuwa mgongo kamili lakini kuwa ndiyo sehemu ya msingi ya watanzania walioamua kujielekeza kwenye shughuli za kilimo kunufaika na kujikwamua na umaskini.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo tutahakikisha kila linalotustahili kulifanya tunalifanya ili kutafuta matokeo yanayokusudiwa, kwa yote ambayo nilisema mwanzo yanahitaji kuingia kwenye bajeti yakiwemo ya masoko na hasa masoko ya mipakani ambayo kwetu ni muhimu, yakiwemo maeneo ya kukusanyia na vituo vya kukusanyia nafaka pamoja na matunda, nitayaonesha kwa kina kupitia bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijaanza kujibu hoja za msingi sana ambazo zimezotolewa na Waheshimiwa Wabunge; mtakubaliana nami kwamba hali ya hewa jana na leo ilikuwa inaonesha dhahiri kwamba inasindikiza shughuli ya kilimo humu ndani. Tumepata mvua ya kutosha jana na tumepata mvua ya kutosha leo. Dalili njema kwamba Mwenyezi Mungu ameweka mkono wake kwenye kilimo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa leo tena kutekeleza majukumu yetu ya Kibunge. Nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi na Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2026/2027 ambao tunauhitimisha leo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee ninaishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo na Mifugo kwa maoni na ushauri wao ambao umelenga kuboresha utekelezaji wa shughuli za kilimo kwenye eneo la umwagiliaji, huduma za ugani, masoko ya mazao ya kilimo, vituo vya huduma za zana za kilimo, utafiti na uzalishaji wa mbegu bora na ulinzi wa mbegu za asili. Vilevile kujenga miundombinu ya uhifadhi pamoja kuimarisha maendeleo ya ushiriki. Wizara itazingatia maoni na ushauri wao kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji. Aidha, ninaahidi kuwa nitaendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge wote katika kutekeleza malengo ya Taifa ya kuendeleza kilimo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kutoa hoja nzuri sana zinazolenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Kilimo na kujenga Sekta ya Kilimo endelevu na yenye ushindani ili kukuza uchumi shirikishi, kuboresha maisha ya mkulima na Taifa lenye utajiri. Hii inaonesha wazi umuhimu mkubwa wa Sekta ya Kilimo katika uchumi wa nchi hususani katika kuimarisha usalama wa chakula, lishe, maendeleo ya viwanda, ajira na kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa David Ernest Silinde, kwa kuchangia hoja hii na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizojitokeza wakati wa majadiliano. Wakati anazungumza wote watakuwa mashahidi watafikiri ndiyo amekaimu kabisa na nafasi yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Geofrey Mweli, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Athumani Juma Kilundumya anayeshughulikia umwagiliaji na zana za kilimo, pamoja na Profesa Peter Laurence Makenga Msofe anayeshughulikia maendeleo ya mazao na usalama wa chakula kwa kuendelea kunisaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Vilevile ninawashukuru Wakuu wa Idara Na Vitengo, Wakuu wa Taasisi, Bodi, Wakala zilizo chini ya Wizara, na watumishi kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ninaomba nirudie kusema maneno niliyoyasema jana wakati ninatoa hoja kwa sababu ndiyo msingi wa bajeti hii na mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, lakini pia ndiyo msingi wa mwelekeo kwenda 2030. Maneno haya yalisemwa na mzee mmoja aliyekuwa akitoa urithi wakati anakaribia kufariki kwa wanawe alisema, “Kama mnataka mali mtaipata shambani”.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ninaomba sasa niwatambue Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuongea na kwa maandishi. Hoja yangu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 70. Ninapenda kuwahakikishia kuwa majibu ya hoja zote zilizotolewa kwa kauli na maandishi yataandaliwa na kuwasilishwa kwa Waheshimiwa Wabunge kabla ya kuhitimisha Mkutano huu wa Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yafuatayo: Hoja ya kwanza ni eneo la Jenga Kesho Iliyo Bora kwenye program ya BBT.

Mheshimiwa Naibu Spika, Afrika na Dunia kwa miaka mingi tumekuwa na maswali mengi ya namna ya kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana. Kwa mfano Afrika ambayo ina zaidi ya 60% ya ardhi inayofaa kwa kilimo hilo swali tumekuwa nalo kwa muda mrefu sana. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan iliamua kuja na mpango wa kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuanzisha Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora hivyo hiyo program haikuwa na haijaja kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutambua kwamba vijana waliopo wana jukumu la pamoja la kutengeneza kesho yao iliyo bora kupitia kilimo. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa nia ya dhati aliamua kuwezesha vijana na wanawake kupata ajira zenye staha, kuwezesha upatikanaji wa mitaji, ardhi, ujuzi na masoko kupitia programu hii ya BBT.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia BBT wengi wanaichukulia kama ni project na siyo program na hili ninataka angalau kwa dakika mbili nilieleze kwa kina. Tukisema BBT ni project tutaangalia mashamba ya Ndogoye na tutaangalia mashamba ya Chinangali kwa sababu watu wote wanaamini hapo ndipo mwisho wa programu hii muhimu ya BBT, lakini ukienda kwa upana BBT ni zaidi ya miradi ambayo tunaizungumzia (miradi miwili mikubwa) ambayo ndiyo inayobeba sura nzima ya project pana ya Jenga Kesho Iliyo Bora kwa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge programu hii imefanyika kwenye haya maeneo mawili kama pilot study kwa sababu kwa uhalisia ukiangalia Afrika hamna project au program kubwa ambayo ilibeba dhamira ya kujielekeza kuhamasisha vijana kwenda kuingia kwenye kilimo na kutafuta fursa na kutumia fursa za kilimo kujikwamua na umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania sisi ndiyo tumeanza tutafute programu nyingine ambayo iko Afrika ambayo inatekelezwa kwa vijana ambayo imefikia hata kuwa na uwezo wa kutambulika na vijana na Watanzania na wananchi kama ilivyo program ya BBT kwa Watanzania. Baada ya majaribio ya maeneo hayo mawili kwetu tumejifunza kwanza tumefanikiwa, lakini pia kuna changamoto ambazo zimetupa nguvu ya kutengeneza mazingira ya kuweka msukumo wa kwenda mbele tukiwa imara zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakwenda kwenye wilaya na majimbo yetu nchini. Kwa kuanza tunaanza na halmashauri 18 na nitazitaja ya kwanza ni Chemba, Bahi, Kisarawe, Kibaha, Kilolo, Njombe, Manyoni, Musoma, Ikungi, Kaliua, Kakonko, Nkasi, Muleba, Missenyi, Njombe Mji, Manispaa za Geita na Mpanda. Lengo ni kuhakikisha tunawapa vijana kule kule kwenye maeneo wanakoishi sasa nyenzo za msingi za kuwafanya waendeshe kilimo kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaanza pia ujenzi wa miundombinu kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 20,000 katika Halmashauri ya Chunya kwa ajili ya vijana kama inavyofanyika katika mashamba ya Kapunga na Highland Estate. Lengo ni kuhakikisha vijana wanapata ardhi ya kilimo ambayo ilibainishwa kuwa ni hitaji kubwa wakati wa tathmini ya kuanzishwa kwa programu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo BBT imefanikiwa sana kwenye upande wa majaribio na changamoto chache zilizojitokeza ni sehemu ya kujifunza. Niwahakikishie huko tunakokwenda sasa tutaona tunavyogusa vijana. Lakini niseme hatutaishia kwenye hiyo tu tuna mradi wa visima, tuna magari 19 ya visima sasa hivi tunayo. Tuna vijana ambao sasa hivi wanalima kwenye maeneo wanayolima wana changamoto ya uhaba wa maji, wana changamoto ya uhaba wa miundombinu ya umwagiliaji. Waheshimiwa Wabunge wakitusaidia kuwapata tukawatambua tukawatengenezea miundombinu ndiyo jenga kesho iliyo bora itakuwa inatekelezwa kwa utaratibu huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mazao ya kimkakati. Tuna mazao ya kipaumbele 13 ambayo yapo katika ajenda 10/30 au ten thirty na mpango kabambe wa maendeleo ya kilimo 2050. Baadhi ya mazao hayo tumeshaanza kuyafanyia kazi na katika mwaka wa fedha 2026/2027 tumepanga kuendelea na mazao matano ya alizeti, chikichi, ngano, tufaa (apple) na viazi mviringo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii haimaanishi kwamba mazao mengine hatuendelei nayo au hatutaendelea nayo. Tutaweka nguvu kwenye mazao hayo ili kupunguza uingizaji wa mafuta ya kula, kupunguza uingizaji wa ngano na kuhakikisha tunaongeza ajira na kuwa na usalama wa chakula nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uzalishaji wa mazao hayo ya kipaumbele, Serikali itaendelea kutumia vyama vya ushirika katika kuanzisha viwanda vidogo vya kukamua alizeti na usindikaji wa ngano badala ya kutegemea viwanda vikubwa pekee. Pia, kwa kipindi cha muda wa kati na mrefu, Serikali itaimarisha uzalishaji wa zao la Chikichi ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viazi mviringo Waheshimiwa Wabunge wanafahamu zao hili ni moja ya mazao muhimu kwa ajili ya chakula na mhimili mkubwa wa uchumi wa vijana hususan katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini, hata hivyo kumekuwa na tatizo kubwa la uhaba wa mbegu. Sasa eneo tunaloliwekea msukumo ni kuhakikisha tunaweka msukumo kwenye utafiti wa mbegu na upatikanaji wa mbegu za uhakika kupitia taasisi yetu ya utafiti ya TARI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa TFC. Mwaka 2021 wakati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TFC ilikuwa imekufa. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuipatia TFC mtaji wa shilingi bilioni 116 ambao umeiwezesha kuwa miongoni mwa kampuni kubwa katika biashara ya mbolea nchini ikishika nafasi ya nne kati ya kampuni 32.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kufufuliwa kwa kampuni hiyo imeweza kuuza jumla ya tani 299,787 zenye thamani ya shilingi 544,000,180,000. Katika msimu wa 2025/2026 unaoendelea mathalani Oktoba, 2025 ilipojitokeza changamoto kubwa ya mbolea ya DAP katika maeneo ya uzalishaji, TFC ndiyo kampuni pekee iliyonunua na kusambaza mbolea ya DAP tani 50,000 kwa kipindi ambacho kampuni nyingine binafsi hazikuleta na kuwasaidia wakulima kuwa na mbolea ya kupandia na tukavuka salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua kuna maeneo ilichelewa na hayo ndiyo malalamiko makubwa ya Waheshimiwa Wabunge lakini kwa sababu tumejifunza tutahakikisha msimu ujao wa kilimo tunawahisha mbolea kwa sababu tumejua kutegemea kampuni binafsi pekee tunaweza tukakwamisha jitihada za wananchi wetu kwenye kilimo hasa kwa kukosa pembejeo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hilo tumelichukua na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tutaliwekea msukumo mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa hoja ya ushirika mwaka huu Waheshimiwa Wabunge wanafahamu, tumeuza mazao ya kahawa, korosho, tumbaku, chai, pamba, ufuta, kakau, soya, mbaazi, dengu, mkonge, choroko, pareto, maharage na miwa tani 1,719,219.77 kwa thamani ya shilingi trilioni 4.048 kupitia ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ushirika kuna watu wema na wabaya kama ilivyo kwenye maeneo yote ya kazi. Ninakiri na ninafahamu kuhusu mnada Na.6 wa Tandahimba ambao ulitokea changamoto ambayo tayari imetatuliwa pamoja na kwamba hiyo ni chini ya 0.01% ya jumla ya biashara iliyofanyika kupitia ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, ushirika unafanya vizuri na unaendelea kuimarishwa. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuboresha ushirika kuwa nyenzo muhimu ya kuleta mageuzi ya kiuchumi. Sisi ambao tumepewa dhamana ya kusimamia Wizara ya Kilimo tutaweka udhibiti mahususi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana kupitia program ya “Linda Ushirika Chagua Uadilifu” sasa kuwa na chombo kitakachohusisha vyombo vyote vinavyohusika na enforcement, udhibiti na mambo kama hayo ikiwemo Polisi, TAKUKURU, DPP na ofisi nyingine za udhibiti ili kwenda kufanya ufuatiliaji kwenye maeneo yaliyofanyiwa ufujaji au ubadhirifu, lakini kubwa kutengeneza udhibiti ili pesa ya mwanaushirika isiliwe tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masoko kwa kiasi kikubwa tumefanyia kazi changamoto zilizokuwepo huko nyuma. Tumefungua masoko mapya, tumevutia wanunuzi na kuimarisha mifumo ya uuzaji wa mazao ya kilimo. Kwa upande wa mazao mbalimbali imebainika kuwa pale bei inaposhuka wakulima wanaona kama ni changamoto ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua kuingia kwenye biashara ya Kimataifa. Kama wanavyofahamu kwenye kufanya biashara kuna kupanda na kushuka kwa bei kutegemea nguvu ya soko. Mazao mengi ya biashara yanategemea soko la nje na Tanzania siyo nchi pekee inayozalisha mazao hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa sababu tunaendelea na jitihada za kufungua masoko, tutakuwa tukifuatilia bei ya masoko kama walivyoshauri kwa sehemu kubwa huko huko ambapo yapo masoko husika ili wakulima wetu wapate uhakika na wapate bei ya uhakika tofauti na kuruhusu watu wa katikati kuendelea kutumia mwanya wa kutojua bei halisi ya soko kwa bidhaa tunazolima nchini kuwanyonya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa hoja ya bima ya afya kwa wakulima wa zao la korosho, ushauri umepokelewa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote wanaotoka kwenye eneo tunalolima zao la korosho tutafanya tathmini ya kina kujua namna gani tunaweza tukafanikisha hili kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapokamilisha tutakaa na kuwashirikisha wote ili tuone namna bora ya kulitekeleza. Hili hatutalifanya kwa korosho tu, tutalifanya kwenye maeneo ya mazao mengine kama pamba, tumbaku na maeneo mengine ambayo yana mazao yanayolimwa kwa ukubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa zao la chai ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya kiwanda cha DL kwa muda mrefu nyuma, lakini hivi leo tunavyozungumza tumefanya majadiliano ya pamoja na mwekezaji pamoja na financier wa mwekezaji ambaye ni CRDB Bank. Mwekezaji huyo ameonesha nia na ninawaahidi ndani ya miezi sita kama DL hataweza kutekeleza tuliyokubaliana tutatafuta mwekezaji mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba katika hili uruhusu baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa maeneo ya chai pamoja na Kamati inayosimamia Sekta ya Kilimo kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja tufanye ziara kule uwandani kwenye eneo la mradi. Twende wote tusikilize tuone lakini tujiridhishe na kile ambacho kinazungumzwa kwamba ni uwekezaji wenye lengo la kuanza uzalishaji wa chai bila usumbufu kwa wakulima lakini na kwa wadau wote wanaozunguka mashamba husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini tukienda tukarudi wote kwa pamoja tukijadiliana tutakuwa na jambo la msingi la kushauriana ili kutafuta hoja pana. Hiyo ni pamoja na kwenye uwekezaji wa kiwanda cha WATCO, (Wakulima Tea Company Limited) lakini pia na yale mashamba yaliyopo na uwekezaji unaoendelea kule East Usambara pamoja na Korogwe na Bumbuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kiwanda cha Mbolea kujengwa Tabora msimamo wa Serikali haujabadilika. Hata hivyo, mwekezaji ambaye tunamkusudia au tulimkusudia ajenge kiwanda husika ni mwekezaji binafsi na Wizara inatamani uwekezaji huo ufanyike nchini na ukifanyika Tabora ingekuwa baraka zaidi kwa sababu ni karibu na eneo ambalo uzalishaji mkubwa na watumiaji wakubwa wa mbolea hiyo wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mwekezaji ni mtu binafsi, sisi tungetamani. lakini na yeye ni lazima tumpe nafasi ya kuangalia namna anavyoweza kutengeneza biashara kupitia kile anachokusudia kukifanya. Hata hivyo, nisitize msukumo wa Wizara na msukumo wa Serikali ni kiwanda kijengwe Tabora ili kiwe karibu na wahitaji wa mbolea husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya pia vikao na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka kwenye maeneo yanayolima tumbaku, yanayolima pamba pamoja na korosho. Niwahakikishie yale yote tuliyokubaliana tutahakikisha tunayawekea msukumo kuyatafutia matokeo. Sasa nishukuru tena kwa kunipa nafasi ya kutoa ufafanuzi wa maeneo machache kuhusu hoja hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa kutoa hoja. (Makofi)