Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Daniel Godfrey Chongolo (2 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Bwawa la Mayuyu na Skimu ya Umwagiliaji - Korogwe Vijijini?
NAIBU WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji nchini ikiwemo katika Wilaya ya Korogwe ambapo kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zinaendelea katika Skimu za Kwamngumi, Magoma, Mapangoni na Kwagunda ambapo usanifu huo unajumuisha Mabwawa ya Magoma na Mapangoni (Mayuyu) yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Usanifu wa mabwawa hayo umefikia wastani wa 40% kwa usanifu wa Bwawa la Magoma na 73.6% kwa usanifu wa Bwawa Mapangoni na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2026. Baada ya usanifu wa mabwawa hayo kukamilika utajumuishwa kwenye mpango wa ujenzi wa miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika Skimu za Mkomazi na Chekelei zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ikihusisha ujenzi wa Mabwawa ya Mkomazi na Chekelei ambapo utekelezaji wake umefikia 96.4% kwa Bwawa la Mkomazi na 10% kwa Bwawa la Chekelei. Ujenzi wa Bwawa la Mkomazi unatarajiwa kukamilika Septemba, 2026 na ujenzi wa Bwawa la Chekelei unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2027.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa miradi hiyo kutanufaisha wakulima 20,000 katika Vijiji vya Manga Mtindiro, Goha, Kwenangu, Magila, Mkumbara, Mazinde Mheza, Mazinde Bagamoyo, Mabogo, Kasiga, Mlembule, Magila Gereza, Mombo, Makuyuni, Kwasunga, Chekelei, Chepete, Madumu na Madala.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Je, lini Mradi wa Umwagiliaji wa Arusha Chini utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji nchini ikiwemo katika Mkoa wa Mtwara. Lengo la utekelezaji wa miradi hiyo ni kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuchangia kuongeza kipato cha wakulima kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo, hadi kufikia Machi, 2026 mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji wa Arusha Chini amepatikana na kukabidhiwa eneo la mradi kwa ajili ya ujenzi. Mradi huo una ukubwa wa jumla ya hekta 264 ambapo gharama za utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo ni shilingi bilioni 14.83.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wakulima 950 katika Vijiji vya Arusha, Arusha Juu, Mkomo, Ngorongoro, Chawi, Chawi Sokoni, Mchanje na Ngonja na hivyo kuwezesha wakulima kulima zaidi ya mara mbili kwa mwaka.