Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, ninaomba niungane na Mwenyekiti wetu, kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama kijana nimejua kwamba, vijana wote wanafarijika pale ambapo vijana wenzetu wanapata nafasi, wanazitumia vizuri na wanazitendea haki. Mheshimiwa Waziri Anthony Mavunde anaitendea haki sana nafasi yake, ambayo Mheshimiwa Rais amemwamini. Tunampongeza, sisi vijana wenzake na anazidi kutu-inspire katika maeneo mengine na tunamtakia kila la heri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tunajua kwamba, hakuna kijiji kisicho na wazee, kaka yetu pia, Naibu Waziri, tunampongeza sana kwa msaada mkubwa anaoutoa kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Menejimenti nzima ya Wizara. Baada ya pongezi hizo, sisi katika Jimbo letu la Ngara tuna Mradi wa Kabanga Nickel; kama ambavyo maeneo mengine yana dhahabu, mengine yana almasi, sisi katika Jimbo la Ngara na Wilaya ya Ngara Mwenyezi Mungu ametujalia tumepata nickel, lakini imekuwa ni story ya muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu ama kumbukumbu inaonesha kwamba, utafiti wa kwanza ulianza kufanyika mwaka 1976 pale Kabanga Nickel. Hii ni kwa mujibu wa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wakisaini mkataba na kampuni ambayo inatakiwa kuendesha huu mradi, alisema yeye mwenyewe kwamba, utafiti wa kwanza ulianza mwaka 1976.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chote hicho ambacho sisi watu wa Ngara tumekuwa tunasubiri kwa muda mrefu kuweza kunufaika na ile rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia, mpaka leo hakuna namna ambavyo tunaweza tukasema kwamba, tupo tumenufaika au tunaona dalili za kunufaika. Kwa bahati mbaya ni kwamba, hata jitihada zote ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais kwa sasa hivi, mimi Bahati nzuri nimekuwa ninazungumza na Mheshimiwa Waziri mara kwa mara, ameniambia jinsi ukweli ulivyo na ninauona mwanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo ninamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa mdomo wake, aongee na watu wa Ngara atuambie Mradi wa Kabanga Nickel ni lini unaanza? Kauli moja tu! Atuambie Mradi wa Kabanga Nickel ni lini unaanza? Hilo tu litakuwa limetosha; sisi hatuna kitu kingine ambacho tunataka kusikia kwa siku ya leo kutoka kwa Waziri zaidi ya kwamba, Mradi wa Kabanga Nickel unaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, siyo kwamba hatuamini, tunaamini kwamba ni kitu kinakuja kutokea, lakini kwa bahati mbaya sisi watu wa Ngara tulishang’atwa na nyoka huko nyuma, sasa hivi tukiona majani tunakuwa na wasiwasi. Kuanzia mwaka 1976 mpaka leo ambavyo tunaendelea, tumekuwa tunaona zinakuja kampuni; inakuja kampuni hii inatoka, inakuja kampuni nyingine inatoka, inakuja kampuni inatoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi uelewa wetu, wananchi wa kawaida, ni tunajua kwamba, tayari pale shughuli zinaendelea. Hayo mambo ya kitaalam wanayajua wao kwamba, sijui ni utafiti! Sijui ni nini, lakini sisi wananchi wa kawaida ambao tumezunguka eneo lile, ambao tunategemea tuwe tunanufaika na eneo lile, tunajua kwamba shughuli zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mwaka 2021 tunakumbuka ndipo mkataba ulisainiwa, kwa ajili ya kuanza huu mradi rasmi, miaka mitano iliyopita. Ninakumbuka kwenye ile hafla ya kusaini ule mkataba iliyofanyika Bukoba, mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano na miongoni mwa watu ambao walitufanya sisi watu wa Ngara tukapata faraja kwamba sasa tunaenda kunufaika ni Mheshimiwa Profesa Kabudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Kabudi wakati anaelezea manufaa ya ule mradi, item Namba 7 aliyoitaja, ninaomba niinukuu alisema: “Miongoni mwa faida za huo mradi ni kuendeleza biashara, uchumi na maisha bora kwa Wilaya ya Ngara na Wilaya ya Kahama na wananchi wake kwa ujumla”. Akamalizia kusema, “Ngara Oyee!”, akamalizia kusema “Kahama Oyee!”. Sasa, leo ni miaka mitano imepita tangu kauli zile za kututia matumaini za Mheshimiwa Profesa Kabudi, ambazo alizitoa jinsi ambavyo tunaenda kunufaika na Tembo Nickel, lakini mpaka sasa hivi watu wa Ngara wanaamini kwamba, ni story zinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu, tumepita katika vipindi mbalimbali vya kuambiwa hiki kitaenda hivi, hiki kitaenda vile, mpaka leo, hata angekuja nani leo akatuambia, mimi ninajua kwa sababu, pengine angalau nimepata nafasi ya kuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini, ninajua kwamba, kuna kitu kinakuja, lakini watu wa Ngara wanaamini ni story kwa sababu, story za hivyo wameambiwa kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, leo inawezekana ikawa ni siku ambayo wananchi wa Ngara watafurahi sana watakapomsikia Waziri. Kwa kipindi chote ambacho kimepita Mheshimiwa Waziri, tunaomba basi leo awafurahishe watu wa Ngara, awape matumaini, awaambie Mradi wa Kabanga Nickel utaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana wengi wa kule Ngara wameomba kazi katika huu mradi ambao wanaamini kwamba, unakwenda kuanza, sasa hata akipata kazi sehemu nyingine anaogopa kwenda kwa sababu, anategemea hapa kwa hiyo, kuna vitu vingi sana vime-stuck. Kuna watu wengine wameanza kutengeneza biashara zao, wameanza kubuni mawazo ya biashara, lakini kila siku kitakuja hiki, kesho kitakuja kitu kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ilitokea huko nyuma tukawa tunaamini kwamba hiki kitu kinaenda kutokea na kwa sababu hakijawahi kutokea, Mheshimiwa tunaomba atushangaze watu wa Ngara, basi tunaomba itokee. Sisi Ngara mambo ambayo huwa tunayaomba kwa Serikali, ni mengi. Wakati huu ambao tumekuja tumesema vitu vingine, wakitupa vitaenda kupunguza shida nyingine hata hawatapigiwa kelele.
Mheshimiwa Naibu Spika, watakapotupa Tembo Nickel kuna mambo mengine automatically yataanza kujipeleka. Sisi watu wa Ngara hatutalalamika kwa sababu, tunaamini tutapata ajira, tutapata uchumi kama ambao alisema Mheshimiwa Profesa Kabudi, lakini kama itaendelea kuwa story, kama miaka yote, sisi watu wa Ngara tutaendelea kuwa disappointed. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, mimi ninamjua vizuri sana, ninajua jinsi gani ambavyo yuko committed na mara kwa mara amekuwa akiniambia nenda kaa vizuri na Tembo Nickel, kitu kinaenda kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba, watu wa Ngara nimewaambia vitu vingi sana, vingine vinatokea vingine vitakuja kutokea, lakini vingine havitatokea. Hili wakilisikia kutoka mdomoni mwa Waziri leo, atapokuwa anahitimisha hapa, atuambie Tembo Nickel inaanza lini na Kabanga Nickel inaanza lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Ngara watamshukuru na sisi tunamwombea kila la heri, tunamtakia utekelezaji mwema wa bajeti yake, ili kuwa na mengi, lakini ninaomba nisichanganye hili la Tembo Nickel na na kitu kingine. Ninaomba leo libaki hilo hilo la Tembo Nickel peke yake, ili kama ananijibu, anijibu hilo peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na maendeleo ya vijana. Nami nikiwa kama kijana, basi ninashukuru angalau nimepata nafasi hii ya kuzungumza na Serikali, na vilevile kuzungumza na vijana wenzangu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sisi kama vijana tumekuwa tuna changamoto nyingi ambazo kwa bahati mbaya zilikuwa hazipati ufumbuzi wa haraka kwa sababu zilikuwa zinashughulikiwa na idara. Tulikuwa ni idara ya vijana ambayo ilikuwa katika ofisi ambayo inashughulikia matatizo mengine mengi. Kwa hiyo, sisi vijana tulikuwa ni kama idara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa mara ya kwanza katika uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi vijana tumetolewa kuwa kama idara, sasa tumekwenda kupewa Wizara rasmi ya kwenda kushughulikia matatizo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunampongeza sana kwa sababu tunaamini kwamba pamoja na matatizo mengi tuliyonayo sisi kama vijana, lakini hili la kutupa Wizara ambayo ita-deal na vijana pekee yake, angalau inatoa mwanga kwamba yapo mazuri mengi ambayo yanakuja kwa ajili ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso kaka yangu huwa anasema kwamba “Asiyeshukuru kwa kidogo, hata kwa kikubwa hawezi kushukuru.” Kwa hiyo, vijana tunashukuru angalau kwa hili tu la kutupa visa. Sisi vijana, hili tu peke yake, tunashukuru, tunajua mambo mengine mengi yanakuja, Mheshimiwa Rais atakwenda kuyamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Waziri, ameeleza katika hotuba yake mambo ambayo ameyafanya tangu amekabidhiwa hii Wizara. Ni Wizara mpya, lakini ameeleza mlolongo wa mambo mengi sana ambayo yamefanyika ndani ya kipindi kifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunampongeza yeye pamoja na watendaji wake. Tumekuwa tukiona vilevile ambavyo anaenda katika maeneo mbalimbali, anakunywa chai na bodaboda, anakula maandazi na mamalishe. Hii inaonyesha jinsi gani ambavyo Mheshimiwa Rais hakukosea kumpa Mheshimiwa Joel kuwa msimamizi wa sekta yetu sisi vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zote ambazo zinahusu vijana, mwisho wa siku zinaongea katika eneo moja. Vijana inawezekana tunaambiwa tunahitaji vitu vingi, lakini tunahitaji kitu kimoja tu, fedha. Tunahitaji fedha, siyo kitu kingine chochote kile. Sasa fedha inapatikana kupitia njia mbalimbali; kuna ajira, kuna ujasiriamali, na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata mipango mingine yote ambayo tutakuwa nayo, kama kijana hatakuwa na fedha ina maana hatuna uhakika kama vijana tutakwenda kuridhika, kwa sababu changamoto nyingine kubwa sana ambayo inatajwa ni ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama vijana tukitendewa haki katika eneo hili kwenye hii Wizara yetu ya Vijana, vijana tukapata yale ambayo tunahitaji, ina maana hata tatizo la ajira kwa nchi yetu litakwenda kupungua kwa kiasi kikubwa sana, kwa sababu vijana wengi ndiyo ambao wanahitaji ajira. Ni kwa bahati mbaya kwamba ukiangalia jinsi ambavyo mambo yanaenda, hatuoni kama kuna mwanga wa tatizo la ajira kumalizika kwa siku za karibuni. Kwa hiyo, ambacho kinaweza kikafanywa na Serikali ni kutuwezesha sisi vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Waziri amekuja na jambo zuri kuhusiana na Benki ya Vijana, tunapongeza sana kwa hili, lakini kabla Benki ya Vijana haijaanza, sisi vijana hapa katikati tunaishije?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tulipewa shilingi bilioni 200, lakini naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengine wote ambao wamesema kwamba zile shilingi bilioni 200 zimeenda tofauti na vile ambavyo sisi vijana tulikuwa tumetarajia, zimeenda katika maeneo mengine mengi ambayo wengine hatuwezi kukajua huku kuna kiasi gani wala utatuma kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kipindi hiki ambacho bado tunasubiri Benki ya Vijana ianze, tumeshuhudia majanga mbalimbali ambayo yametokea kwenye nchi yetu, tumeshuhudia sehemu nyingi ambazo zimekuwa na changamoto, Serikali imepeleka ruzuku. Kwa hiyo, changamoto ya ajira kwa vijana, changamoto ya ukosefu wa kipato kwa vijana sasa hivi tunaomba Serikali basi ichukulie kama ni suala la dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikichukulia kama ni suala la dharura, ina maana hata ile shilingi bilioni 200 ambayo tumepewa, ambayo imeenda katika maeneo mengine tofauti, Serikali tunaomba ituongezee sisi vijana. Tunaomba Serikali itukopeshe twende tukapambane kutafuta fedha, tutarudisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo Serikali inapeleka ruzuku ili mambo fulani yafanyike vizuri, lakini sisi hatutaki ruzuku, ninaomba mtukopeshe hizo fedha, na tutengenezewe mazingira mazuri ya kuzirejesha. Vilevile ninaomba tutengenezewe mazingira mazuri ya sisi kukubalika tuweze kukopesheka, kwa sababu changamoto kubwa ambayo inatukabili vijana ni kwamba ukienda utaambiwa njoo na dhamana, au vitu mbalimbali ambavyo lazima upeleke kwa ajili ya kupata mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikitudhamini yenyewe, Serikali ina watu mpaka ngazi ya kijiji, mpaka ngazi ya kitongoji ina watu ambao ni wasimamizi. Kwa hiyo, nikiomba mkopo, itajulikana Dotto anakaa sehemu fulani, Mwenyekiti wake wa Mtaa ni fulani, Mtendaji wa Kijiji ni fulani. Kwa hiyo, siwezi kutoroka na hizo fedha hata kama sina dhamana, lakini niaminiwe kwa kitambulisho cha NIDA, kwa vyeti vyangu vya shule, kwa uongozi wa Serikali ambao uko pale. Mniamini mnikopeshe ile fedha halafu mwone baada ya muda mrefu kama sitakuja kurejesha. Tukirejesha na wenzetu watapata; na mkitupatia, changamoto ya ajira itabaki ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama leo mwanafunzi ambaye amemaliza chuo kikuu anaweza akaenda Kariakoo pale, akaongea na mtu mwenye duka akamwambia naomba tisheti 10 niende nikauze nikishauza nitakurejeshea fedha yako nami nipate cha kwangu, mtu mwenye duka anamwamini yule mwanafunzi, kwa nini Serikali isituamini sisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani tuliyonayo kwa Serikali yetu ni kubwa sana na haya mambo ambayo tunayaomba, tunayaomba tukiamini kwamba yanawezekana. Tumesikia fedha ambazo zimeenda sijui content creators, sijui nini, kila sehemu ambazo fedha zimeenda unaanza kuona watu wanakuwa wengi katika lile eneo. Siyo kwamba watu wanafanya vile vitu, lakini ndiko wameona ambako kuna fedha. Kwa hiyo hata zile fedha shilingi bilioni 200 zingebakizwa kwa vijana, sisi vijana ndiyo tunajua tunataka tufanye nini? Msitulazimishe kwenda sijui kufanya hiki, kufanya hiki, au kufanya hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wangepeleka kwa vijana pale, sisi tutajua zile shilingi bilioni 200, Mheshimiwa Joel atajua yeye na vijana wenzake tuzigawane vipi twende tukafanye kazi tuweze kurudisha marejesho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, changamoto kubwa ambayo inatukabili sisi vijana, ni kuwa walalamishi. Tunakuwa walalamishi kwa sababu kuna kikundi kidogo cha watu ambao wamejipa usemaji wa vijana kwamba wao ndio wasemaji wa vijana, lakini kile kikundi siyo kikundi sahihi, ni kikundi ambacho hakina suluhisho la vijana lolote. Ni kikundi ambacho kinatufundisha sisi vijana kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kuongea na vijana wenzangu Waheshimiwa Wabunge. Vijana wenzangu Tanzania, tusikubali kuingizwa kwenye huo mkenge wa kuwa walalamishi kwa sababu ya watu wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tayari ameshaonesha mwanga kwamba matatizo ya vijana yanawezekana. Tusikilize sauti zinazotoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kijana mwenzetu ambaye ameaminiwa, huyo ndiye awe msemaji wetu vijana. Tusikubali wahuni wengine wakabeba ajenda ya kutusemea sisi vijana wakati sisi vijana tupo, na tunajua kwamba matatizo yetu yanatafutiwa ufumbuzi kwa jinsi ambavyo Dira imeoneshwa na Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kuwaasa vijana wenzangu Wabunge pamoja na vijana wenzangu kote kule walipo, tukatae wahuni, tumsikilize Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri wetu. Hao ndio wamebeba maono ya Sekta ya Vijana na siyo mtu mwingine yeyote yule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)