MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vile vile, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini majibu kama haya si mara ya kwanza kuyasikia hapa Bungeni kwa sababu mwaka jana mwezi Aprili wakati Mheshimiwa Waziri akijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ngara aliyepita, alisema kwamba Serikali tayari ilikuwa katika hatua za mwisho za kumlipa mkandarasi ili kazi ianze kufanyika. Sasa leo, majibu ni kama yale yale ya mwaka jana. Sasa ningependa kupata kauli ya Serikali katika maswali yangu mawili.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, ni lini sasa kazi rasmi ya ujenzi itaanza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, katika eneo la Keza ambalo amesema ndiyo ujenzi utaanza; wanaanza kutoka Keza kwenda Nyakahura au Keza kwenda Murugarama kwa sababu Keza ni katikati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, miradi yetu inachukua muda mrefu na ndiyo maana bado hatujasimamisha, tunaendelea na utaratibu wa kuijenga. Pia, kama nilivyosema kwamba barabara hiyo itajengwa, itaendelea kujengwa na bajeti yake imeshakamilika na ndiyo maana tayari tumeshapata mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, barabara hiyo tutajenga kuanzia Keza – Nyakahura kwa hatua ya kwanza wakati tunasubiri lot ya pili kutoka Keza – Rulenge – Murugarama. Ahsante.