Contributions by Hon William Kafiti Kafiti (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue nafasi hii kuchangia hotuba muhimu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kusimamia Dira yetu ya 2050 katika kuhakikisha wanakuza uchumi na kuzalisha ajira nyingi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na vilevile kwa ziara yake ambayo ameendelea kuifanya katika mikoa mbalimbali ambayo imeleta tabasamu kubwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo, kupitia ziara zake, ninapenda kutoa rai kwa watendaji walioko maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu amepita, basi wasisubiri kwanza Waziri Mkuu aje ndiyo wananchi waweze kusikilizwa kero zao. Kwa hiyo, ninaomba sana waendelee kuwasikiliza wananchi, ili waendelee kupata tabasamu ambalo ameahidi Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua tena fursa hii kuwapongeza Mawaziri wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya, Mheshimiwa Deus Sangu na Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Profesa Shemdoe, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ninaomba nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maeneo mbalimbali, hasa nitajikita katika maeneo mawili, lakini kubwa nitaongelea zaidi katika eneo la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba, Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa ambayo ina makusanyo makubwa na inachangia kwa kiwango kikubwa kwenye pato la Taifa. Zaidi ya asilimia 7.2 ya pato la Taifa yanachangiwa na Mkoa wa Mwanza, nyuma ya Dar es Salaam. Kwa maana hiyo, Mkoa wa Mwanza, pamoja na kuwa ni mkoa wa kimkakati na sisi kama Wabunge, tunalo jukumu la kuhakikisha tunaendeleza yale mazuri ambayo Mheshimiwa Rais ametaka kuyafanya katika Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Wilaya ya Ilemela, ambayo mimi ndiye Mbunge wa jimbo hilo, ni wilaya ya kimkakati. Ukiangalia katika Mkoa wa Mwanza ni wilaya ya pili ambayo inaongoza kwa makusanyo. Wilaya yetu ya Ilemela ukiangalia miundombinu yake ya barabara kiukweli inasikitisha na tunatakiwa tupewe kipaumbele kikubwa na Mkoa wa Mwanza kwa sababu, ndiyo hub ya kiuchumi ya Ukanda wa Maziwa Makuu. Tunaomba sana Serikali iendelee kuweka jicho la pili kuhakikisha tunarekebisha sana miundombinu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ambapo tumesikia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba sasa TARURA wanakwenda kuongezewa fedha na sisi tunaamini, kama wawakilishi wa wananchi, tutaendelea kusimamia na kuhakikisha miundombinu hii inarekebishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwa sasa hivi barabara nyingi, hasa za Jimbo langu la Ilemela, zimekuwa ni changamoto kubwa. Barabara zimeharibiwa na mvua, tunafahamu pamoja na kuwa mvua ni baraka, lakini barabara nyingi zimeharibika. Kwa hiyo, ninaomba sana ndugu zangu wa TARURA kuangalia barabara za wakazi wangu wa Jimbo la Ilemela na wananchi wote kwa ujumla, kuhakikisha barabara hizi ziweze kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo ninaomba niongelee Barabara yangu ya Ilemela ya kimkakati, Serikali naomba iiangalie kwa jicho la pili. Barabara hii ya Airport – Kayenze ni muhimu sana na kiungo kwa Wilaya hii ya Ilemela. Barabara hii endapo itafunguka, itahamasisha maeneo makubwa ya kiuchumi, hasa kwa wavuvi wanaopatikana Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Ilemela.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongelee eneo la miundombinu ya uwekezaji wa viwanda. Tunafahamu kwamba, nchi hii imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ina-promote uanzishwaji wa viwanda vingi. Kwa hiyo, naendelea kuipongeza sana Serikali na ndugu zetu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wakiwemo NSSF, PSSSF pamoja na WCF kwa kuwa, mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanaunga mkono juhudi ya Serikali kuhakikisha wanaimarisha uanzishwaji wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mfano, NSSF, Kiwanda chetu cha Mkulazi zaidi ya wananchi 10,000 wameajiriwa pale. Zaidi ya tani 50,000 zimeendelea kuzalishwa pale. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iendelee kutumia Mifuko hii kwa sababu, imeonesha kufanya vizuri. Hata watu wa PSSSF, ukiangalia Kiwanda cha Kilimanjaro Leather kinafanya vizuri katika utengenezaji wa viatu, lakini vilevile katika eneo hilo hilo bado tuendelee kuiomba Serikali iendelee kushika Mifuko hii, ili iendelee kufanya vizuri kwa sababu, mifuko hii ndiyo inasimamia maslahi ya wazee wetu ambao wanastaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo hilo, ninaomba nielezee yafuatayo kwa sababu, mifuko hii imekuwa ikileta tija katika jamii yetu. Mifuko hii imekuwa ikiongeza chachu ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali, basi tuiombe Serikali kwa madeni ambayo Mifuko hii inadai, iweze kuyamaliza na kuongeza mafao kwa wastaafu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo hilo ninaiomba sasa Serikali, kama itaridhia, Daraja la Kigamboni tunafahamu uwekezaji mkubwa umefanyika pale. Basi ni jukumu la Serikali iweze kulipa fedha zile pale na lile daraja liweze kurudi Serikalini na baadaye wananchi wa eneo hilo waweze kupita bila kuwa na kipingamizi cha aina yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni uwekezaji. Pamoja na mazingira mazuri ambayo Serikali imeyaweka kuhakikisha kwamba inalinda maeneo ya uwekezaji na wananchi kujikwamua kiuchumi, napenda kuipongeza sana TISEZA kwa juhudi inazofanya katika kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapatikana, kwa ajili ya uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Halmashauri nyingi na Waheshimiwa Wabunge watakuwa ni mashahidi hapa, asilimia nyingi zina maeneo mengi ya kuwekeza, lakini hazina uwezo wa kulipa maeneo hayo ya kimkakati, kwa ajili ya uwekezaji. Sasa ninaiomba Serikali, kupitia TISEZA, itafute yale maeneo strategic ambayo TISEZA inaweza ikalipa fidia kwa niaba ya Halmashauri, ili wawekezaji wanapokuja waweze kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yangu ya Ilemela tuna maeneo mazuri ya uwekezaji. Kulingana na uwezo wa manispaa yangu, haiwezi kulipa hizo fidia kwa ajili ya wakazi hao kuyaachia, kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali, kupitia TISEZA, itakuwa ni vizuri yale maeneo yote ambayo ni strategic, kwa ajili ya uwekezaji tuweze kuwatumia wadau hawa, ili waweze kuimarisha ajira na uanzishwaji wa viwanda vingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kuliongelea kundi ambalo nasema nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowaongelea ndugu zangu wa bodaboda pamoja na bajaji. Mimi nikiwa kama Rais wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Mwanza, ninalo jukumu la kuhakikisha kwamba, tunawajengea uwezo na kuwatetea, ili nao waweze kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu vijana wengi wamejiajiri na ni kundi kubwa. Ukiangalia katika wilaya yangu tu, ni zaidi ya vijana 12,000 wamejiajiri katika eneo hili. Kwa hiyo, ni wakati sasa kuiomba Serikali, kundi hili nalo tuweze kulirasimisha wawe Maafisa Usafirishaji kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba vilevile kusema kitu kimoja, katika eneo hili vijana wengi wanataka kujiajiri, lakini gharama za leseni kwao zimekuwa ni kero kubwa kwa vijana wetu. Watu wanataka kuendesha pikipiki hizi, lakini wanakosa uwezo wa kulipia hizo leseni. Ninaiomba Serikali hii sikivu ya Chama cha Mapinduzi katika eneo hili waweze kuangalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita, yalitolewa mapendekezo kwamba leseni iweze kushuka kutoka shilingi 70,000/= mpaka shilingi 30,000/=. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba sana, katika kundi hili la vijana ambao wengi wako huku na mimi siku zote nimekuwa nikihimiza kundi hili kwa sababu, ni kubwa ni lazima sasa, kama Serikali, tuwatoe sehemu moja kuwapeleka sehemu nyingine, ili waweze kujikwamua kiuchumi. Kwa hiyo, tuna mengi ambayo tunahitaji kuongea hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ninaomba sana Mfuko huu wa PSSSF uliwekeza katika eneo la Msamvu pale, ile Msamvu Bus Stand, ambalo kila mmoja tunapafahamu. Lile eneo limejengwa kwa fedha za wastaafu. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali itoe fidia kwa Mfuko huu wa PSSSF, ilipe lile eneo ili liweze kuachiwa katika Halmashauri ile ya Morogoro na PSSSF iendelee na mikakati yake ya uwekezaji maeneo mengine, ili kuweza kulinda mafao ya wastaafu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ninaomba niongelee eneo la vijana, hasa katika eneo la kilimo. Tunafahamu nchi hii kilimo ndiyo uti wa mgongo, kwa hiyo, vijana wengi tunahitaji wajiajiri hapa. Kwa hiyo, katika eneo hilo ninaiomba sana Serikali tuendelee ku-promote, ili vijana wengi waweze kuingia hapa na kufanya uzalishaji unaotokana na maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuendelea kutujaalia afya njema na kuwa pamoja hai katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee sana kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Ilemela kwa kuendelea kuniamini, nami kama kijana ninawaahidi kuendelea kuchapa kazi ndani ya Bunge na nje ya Bunge, kwa maana hiyo niwahakikishie kwamba wana jembe, mimi ni mtu wa vitendo na siyo mtu wa maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tena nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa. Ndugu zangu ninaomba tu niwajulishe kwamba dhamira ya Rais katika kuhakikisha inawainua vijana kiuchumi imeendelea kudhihirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa, Taifa lolote ili liweze kuendelea linahitaji nguvu ya vijana, kwa hiyo vijana pamoja na kuwa nguvu kazi, tunaamini vijana ni mtaji na si liability katika Taifa letu. Dira yetu ya 2050 inahitaji kuwaongezea ujuzi na uimara vijana wote katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, kama Serikali na kama nchi kwa ujumla tunashukuru sana kwa kuendelea kuwaamini vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza sana Rais hata ukiangalia Bunge hili, wengi asilimia kubwa ni vijana. Kwa maana hiyo Taifa hili sasa linaongozwa na vijana na vijana tuliomo katika Bunge hili hatuna budi kuhakikisha tunawasimamia vijana wenzetu ili waweze kujikwamua kiuchumi. Vijana tumekuwa tukilalamika kuomba nafasi na kupewa nafasi za uwakilishi. Sasa nafasi tumepewa, ni jukumu letu ni kuhakikisha tunaonyesha njia kwa vijana wenzetu kwa kuleta maendeleo thabiti katika Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze sana Waziri, kaka yangu Joel Nanauka. Rais hakukosea ametuleta Rais kijana, mzalendo, mchapakazi, muadilifu, mwenye hofu ya Mungu, tunamwamini na vijana tuko nyuma yake. Nasi tutampa ushirikiano wa kudumu na kuhakikisha yale matamanio ya Rais, matamanio ya Serikali, matamanio ya vijana wa nchi hii yanakwenda kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niongelee sasa mambo matatu leo nitaenda kusisitiza. Awali ya yote kwa sababu Rais amekuwa na nia thabiti ya kuwainua vijana. Wakati anafanya kampeni aliahidi kutoa zaidi ya bilioni 200 kwa vjijana wetu na bilioni 200 hizo zimeshaanza kutoka. Kwa hiyo, ndugu zangu ninaomba niwahakikishie kwamba vijana wote pesa hizi zilizotoka ni kwa ajili ya vijana wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hizi zilizotoka haziangalii itikadi ya chama, dini wala kabila, vijana wote wenye sifa watakwenda kukopeshwa pesa hizi. Nami nimhakikishie Waziri, vijana tuko nyuma yake kuhakikisha hizi bilioni 200, ambazo Serikali imetenga, ambazo Rais amezielekeza kwa vijana, basi zinakwenda kufanya kazi ya kuwainua vijana mbalimbali kwenye Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutimiza ahadi yake, leo Wizara ya Vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, tumeahidiwa kupata zaidi ya bilioni nane na mpaka saa hizi zaidi ya bilioni 2.5 zimeshatolewa kwa Wizara hii, pongezi kubwa kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo bado tunaamini hizi bilioni 200 bado zinahitaji kusimamiwa na Wizara hii ya Vijana. Tunafahamu pesa nyingi zimeweza kupelekwa katika Wizara Mtambuka, Wizara za Kisekta ili kuweza kukamilisha mahitaji kwa vijana. Tumeona kwamba kwa wale ambao vijana wana-deal na kilimo, pesa zao ziko Wizara ya Kilimo, wanao-deal na madini ziko Wizara ya Madini na sekta nyingine, lakini ninaomba tuwahakikishie kwamba vijana tutaendelea kutumia hii fursa na tuendelee kuitumia hii fursa kwa umakini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kumekuwa na malalamiko pesa hizi hazitoki kwa wakati, kumekuwa na malalamiko vijana hawapati pesa hizi lakini pesa hizi zimekuwa zikitoka japo ninaweza nikasema kwamba bado Serikali inatakiwa iongeze pesa hizi ili kila kijana aweze kunufaika na mikopo hii na pesa ambazo zimetolewa na Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuchangia Wizara hii, vijana tunajukumu kubwa la kuhakikisha ajenda ya maendeleo na dira yetu ya 2050 tunakwenda kuitekeleza. Ukiangalia hata sensa za 2022 vijana ndiyo asilimia kubwa zaidi ya 60%, Maana yake nini? Dira hii ya 2050 bila kuwaimarisha vijana haitoweza kutekelezeka. Nasi vijana ndiyo lazima tuchukue msingi huu, ni lazima tusimame pamoja kuhakikisha dira hii tunakwenda kuitimiza kwa wivu mkubwa, kuhakikisha kila kijana ananufaika na pesa hizi ambazo Rais amezitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutenga pesa kwa ajili ya maendeleo ya vijana, kupitia Wizara hii zaidi ya bilioni tano zimetengwa kwa ajili ya maendeleo ya vijana. Kupanga ni jambo moja na utekelezaji ni jambo lingine. Katika miaka minne iliyopita kabla ya Wizara hii haijaanzishwa, Wizara hii ilikuwa inatengewa bilioni moja wakati ule ni Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana, sasa hii Wizara inajitegemea, tunaomba hii bilioni tano kwa ajili ya maendeleo ya vijana iweze kutengwa na iweze kutolewa kwa wakati ili iweze kunufaisha vijana wetu. Kwa hiyo, katika eneo hilo ninaomba tuendelee kuiomba sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie wasaa huu vilevile kuomba sana vile Vyuo vya Maendeleo ya Vijana kwa maana Chuo chetu cha Morogoro cha Ilonga pamoja na Chuo chetu cha Songwe, Sasanda, Serikali iendelee kutoa pesa zaidi ya bilioni mbili zimeidhinishwa, sasa ninaiomba sana Serikali kuanzishwa kwa mafunzo haya ya muda mfupi yatakwenda kunufaisha vijana wengi katika maeneo ya kilimo, katika maeneo ya ujasiriamali, katika maeneo ya uzalendo kuhakikisha kila kijana ananufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine niombe tu kitu kimoja kwamba Serikali sasa ije na mpango wa kuwaandaa vijana wake, na hili nimekuwa nikichangia na nimekuwa nikiongea na Waziri wa Mipango, kwamba sasa ifikie wakati Serikali lazima ije na mpango wa kuhakikisha inawatoa vijana wake kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Mfano, vijana leo wa Form Four wakimaliza wale ambao hawajafanikiwa kufaulu wanakwenda wapi? Vijana wa Form Six ambao hawakufaulu wanakwenda wapi? Vijana wanaomaliza Chuo Kikuu nini mpango wa Serikali kuhakikisha unawainua kiuchumi vijana hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali ije na mpango huu, dira yetu ya 2050 itakwenda kutekelezeka kwa sababu tutajua mahitaji ya vijana hawa. Leo tumetoa bilioni 200 hatujafanya research je, ni vijana wangapi watakwenda kunufaika na kiwango hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine labda kwa kumalizia kwa sababu tuko kwenye Wizara hot ya vijana na wanatusikiliza nitaomba muda wako kidogo na mimi kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati hii vijana ndiyo kimbilio letu, kwa hiyo uniwie radhi kidogo tuna madini mazuri ya kuwaona kwamba vijana wengi wanakwenda kunufaika na Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la kilimo kupitia BBT tuendelee kuweka msisitizo, vijana wengi watakwenda kuajiriwa hapa. Tunafahamu tuna vijana wanatoka SUA, ni ajabu kumwona graduate wa SUA anakwenda kutafuta kazi wakati kuna nguvu kazi Serikali inaweza ikatoa mitaji na vijana hawa wakaenda kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vijana wanaomaliza mikataba JKT wakimaliza wanarudi mtaani, kwa nini tusiwaanzishie mashamba ya wao kujiajiri na kuweza kuchangia pato la Taifa? Kwa hiyo, tunafahamu tuna uhaba wa sukari, vijana waende tuwaanzishie mashamba na mitaji waende wakalime. Tunayo mahitaji ya alizeti, kwa maana ya kilimo kama nchi tuna mahitaji ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kumalizia tunapotoa bajeti hii ni lazima Serikali sasa ije na mpango kuhakikisha pesa zinazotoka zimekwenda kufanya nini? Zimesaidia vijana wangapi? Tuimarishe vitengo vya monitoring and evaluation ili kuona tija ya pesa hizi zinapotoka kweli zionekane zinawanufaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niombe Wizara hii imeanzishwa ni Wizara mpya, tunao vijana ambao walikuwa chini ya maendeleo ya jamii kule kwenye Halmashauri. Sasa tuombe watoke kule warudi kwenye Wizara yao ya Vijana kwa sababu sasa Wizara ya Vijana iko kamili na inaendelea na shughuli zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja, vijana tukae mkao wa kula, sasa ni wakati wetu wa kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Asanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii kutoka kwa Wizara hii ya muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Ilemela, kwanza kabisa nitoe pongezi sana kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa kwa kuhakikisha anamtua mama ndoo. Ninadhani wote ni mashahidi, Mheshimiwa Rais wakati anaingia alisema moja ya ahadi yake kubwa ni kuhakikisha anamtua mama ndoo na hili limedhihirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na wananchi wangu wa Jimbo la Ilemela kiukweli tulikuwa kwenye wakati mgumu, ukiona mtu anaulizia maji ya Ziwa Victoria na wewe upo hapo hapo, lakini hupati maji ilikuwa ni changamoto kubwa. Leo nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu sasa Ilemela inakwenda kung’ara, Ilemela inakwenda kuwa na maji ya uhakika. Kwa hiyo, nimpongeze sana Ndugu yangu, Mheshimiwa Aweso amefanya kazi nzuri sana yeye na wasaidizi wake; Mheshimiwa Kundo na Wizara nzima kwa kweli wanajituma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kutoa pongezi kwa dada yangu Nelly wa MWAUWASA anafanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, ninaomba sana kwa nafasi hii niliyopata nitoe pongezi kubwa kwa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu maji ni uhai lakini bila maji binadamu yeyote hawezi kuwa hai na ndiyo maana tunaamini kwamba suala la uwepo wa maji ni suala la muhimu sana katika jamii yetu. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, chanzo chetu cha Capri Point amekwenda kukipanua kutoka lita milioni 90 mpaka lita milioni 144, pongezi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaona Ilemela tulikuwa tuna shida kubwa sana ya maji, lakini kutokana na upanuzi huu wanaokwenda kuufanya katika chanzo chetu cha Capri Point, Wilaya sasa ya Ilemela tunakwenda kuondokana na tatizo la maji. Ninampongeza, mkandarasi aliniambia zaidi ya shilingi bilioni 4.5 tayari zipo Ilemela mkandarasi anaendelea na utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo bado ameendelea kusambaza mabomba. Tunafahamu kipindi cha nyuma Ilemela iliendelea kuwa na changamoto kubwa ya maji, lakini ninaamini kwa uwepo wako kwa bajeti na pesa ambazo tunakwenda kumuidhinishia Ilemela sasa tunakwenda kuwa salama katika eneo zima la maji. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, bajeti hii ni bajeti kubwa, lakini tumeweza kuangalia hapa bajeti hii kwa mapato ya ndani ni ya zaidi 30%. Sasa nimwombe kama hatutaongeza bajeti hii kwa kutumia vyanzo vya ndani nina mashaka utekelezaji wa bajeti hii. Kwa hiyo, niombe sana Mwenyezi Mungu aendelee kumtia nguvu atafute pesa nyingi zaidi kuweza kutekeleza hii miradi ambayo Watanzania wanaitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, sisi watu wa Ilemela tunashukuru ametuletea ule mpango wa maji taka kwa wakazi wale wa mlimani, ametupa zaidi ya shilingi 22,000,000,000 kwa ajili ya wakazi wa Lumala, Kiseke pamoja na Pasiansi. Hilo nimpongeze sana kwa sababu tulikuwa tunapata shida, wakati wa mvua tunasema tunafungulia koki watu wa mlimani, sasa Waziri amekwenda kuboresha maisha ya wakazi wa Jimbo la Ilemela, hilo nimpongeze sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile nimwambie tu na niendelee kumtia moyo, tunafahamu Idara hii wengi tulikuwa tunalia na kubambikizwa bili za maji lakini sasa unakuja kwako na mpango wa smart meter. Maana yake ni kwamba tatizo la kubambikwa bili za maji linakwenda kuwa historia. Kwenye hilo ninampongeza sana Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona wenzetu wa TANESCO sasa hatulalamiki kubambikiwa bili, kwa sababu sasa wameturahisishia. Kwa hiyo, katika eneo la maji, nimwombe sana Waziri aendelee kuweka mkazo huu wananchi waweze kufurahia huduma ya maji wanayoyapata bila kuwa na ubambikiwaji bili. Umbambikaji wa bili umeleta chuki kwa Serikali, umeleta chuki kwa wananchi, umeleta chuki kwa viongozi, kwa hiyo kupitia usimamizi wake tunaamini suala hili linakwenda kwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niendelee kuelezea suala lingine la upotevu wa maji. Tumekuwa tunapambana kwa kiwango kikubwa sana kuhakikisha kwamba tunaongeza speed ya usambazaji wa maji, lakini sijaona mikakati ya kudhibiti upotevu wa maji. Tumeona taasisi kama DAWASA inapoteza maji mengi sana, taasisi kama MWAUWASA inapoteza idadi kubwa ya maji. Kwa hiyo, hii ni hasara kwa Serikali, ni hasara kwa wananchi na inaongeza gharama kwa Serikali, kwa hiyo niendelee kumwomba Mheshimiwa Waziri katika eneo hili tuendelee kulipa mkazo mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni lazima tuwe sasa na mpango, tunasema tuwe na water budget kwa kumalizia. Ni lazima tujue mahitaji yetu ya maji ni kiasi gani, matumizi yetu ni kiasi gani. Kwa historia tunaambiwa kwamba Ziwa Victoria lilishawahi kukauka miaka 400,000 iliyopita. Sasa sisi tumejipangaje katika hili? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri niendelee kumpongeza Waziri, tupo tayari kuhakikisha tunapitisha bajeti yako ili kuleta ustawi wa maisha bora ya watu wa Ilemela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hiyo na ninaunga mkono hoja. (Makofi)