Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon William Kafiti Kafiti (5 total)

MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, bado sisi kama Mwanza na kama wakazi wa Jimbo la Ilemela, tunahitaji kujua huo upembuzi yakinifu utakamilika lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ukamilishwaji wa uwanja huu...
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kafiti Mbunge wa Ilemela alikuwa anajaribu kukazia hoja ile ile ya uwanja wa ndege na kimsingi yeye pale kwake hoja kubwa ambayo anaizungumzia ni upande wa fidia au namna ya kuweza kuondoa wananchi wa pale. Serikali ina dhamira ya kuufanya Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa kimataifa. Ili uweze kuwa na sifa hizo, lazima kama kuna wavamizi waondolewe. Kwa hiyo, nimwombe tu awe na subira, tutamilisha muda siyo mrefu tutaanza kufanya kazi.
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza. Itakumbukwa tarehe 2 Juni, 2023 Wizara ya Utamaduni na Michezo mliomba eneo katika Wilaya ya Ilemela eneo la North Buswelu kwa ajili ya kuanzisha kituo cha ufundishaji wa michezo, lakini mpaka sasa hakuna kitu kinachoendelea. Je, ni lini Serikali itatimiza maombi yake juu ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la Mheshimiwa Kafiti, Mbunge wa Ilemela ni kwamba kweli Serikali tarehe 2 Juni, 2023 iliandika barua kwa ajili ya kuomba eneo kutengeneza Center for Sports Excellence pale Ilemela na mpango ule haujafa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu wakati najibu kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Amari, kwa sasa tumejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu itakayotumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON. Pia Serikali inaanzisha Taasisi ya Sports Infrastructure Management Agency ambayo kazi yake itakuwa pamoja na mambo mengine kutambua, kujenga, kukarabati na kusimamia, kwa maana ya kuendesha maeneo mbalimbali ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Ilemela halijatoka kwenye mipango ya Serikali, na nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Kafiti aendelee kuwa na Subira, litafikia muda wake na litafanyika tutakapomaliza programu hii ya ya AFCON.
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na sasa naomba niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na umeajiri wananchi wengi katika nchi yetu ya Tanzania, kwa hiyo suala la kinga ya bima kwao ni ulinzi mkubwa juu ya kilimo wanachokifanya, na kwa kuwa suala hili limeshachukua muda mrefu, sasa nini kauli ya Serikali juu ya ukamilishwaji wa kanuni hizi ili ziweze kusaidia wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nikiri, ni kweli kabisa kilimo ndicho kimeajiri Watanzania wengi sana ambao wanajipatia kipato na kulingana na umuhimu wake na ndiyo maana kiukweli tumechukua muda mrefu ili kujiridhisha kwamba hizi kanuni zitakuwa rafiki kwa wakulima na Watanzania wote ambao wanajihusisha na kilimo. Kwa maana hiyo, kama ambavyo nimeweza kujibu kwenye jibu langu la msingi, mwaka huu wa fedha utakaonza 2026/2027 ndipo tunaenda kukamilisha utafiti huu na kanuni hizo zitaanza kutumika. Naomba kuwasilisha.
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ilemela, ninaomba kujua, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Pasiansi Lumala – Kiseke, kwa sababu barabara hii ni muhimu kwa wakazi wa Jimbo la Ilemela na imechukua zaidi ya Kata tatu? Ni nini kauli ya Serikali katika hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Pasiansi katika Jimbo la Ilemela ambayo Mheshimiwa Kafiti ameifuatilia mara kwa mara na tunafahamu kwamba Serikali imeendelea kuweka kipaumbele kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa, kwa sababu ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa eneo la Ilemela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ipo kwenye mpango wa Serikali na hatua za utekelezaji wa barabara hizo zitafanyika ili kuhakikisha kwamba inakamilika kwa wakati na inakuwa na ubora unaotakiwa kwa manufaa ya wananchi wa Ilemela. (Makofi)
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ilemela ninapenda kuiuliza Serikali, ni lini itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi chenye hadhi ya wilaya katika Wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Kafiti Kafiti Mbunge wa Ilemela ambaye naye kama ambavyo walivyo Waheshimiwa Wabunge wengine, ameona umuhimu pia wa kuwa na Kituo cha Wilaya katika Jimbo la Ilemela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, kama nilivyotoa majibu ya msingi kwamba tayari tunao mpango ndani ya kipindi cha miaka mitano unaoanza 2026 - 2030 wa kuhakikisha kwamba vituo vyote vya Polisi vya ngazi ya Wilaya ambavyo ni 75 viwe vimejengwa. Hivyo, niwaahidi pia wananchi wa Ilemela kwamba kituo chao cha Polisi nacho kitakuwa katika mpango huo na tutaweza kutenga fedha kwa mujibu wa hali ya bajeti kuhakikisha kuwa tunajenga kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa sasa waridhie na waendelee kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga Kituo cha Polisi ambacho kipo katika eneo la Tunza Road ambacho ni kituo cha Daraja C ili kituo hicho kianze kutoa huduma na baadaye tuweze kujenga kituo cha ngazi ya Wilaya.