Primary Questions from Hon. Mwamengo Ulimboka Baraka (3 total)
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Ibanda – Kiwira Port kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Baraka Ulimboka Mwamengo, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Ibanda – Kajunjumele – Kiwira Port yenye urefu wa kilometa 28 ulisitishwa baada ya mkandarasi aliyekuwepo kushindwa kutekeleza mradi kwa mujibu wa mkataba. Taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi mwingine zinaendelea. Ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza baada ya taratibu za manunuzi kukamilika.
MHE. SUMA I. FYANDOMO K.n.y. MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya Ipinda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Baraka Ulimboka Mwamengo, Mbunge wa Jimbo la Kyela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhitaji mkubwa wa magari ya kubebea wagonjwa. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI imepokea jumla ya magari ya kubeba wagonjwa 382 na magari 212 ya uratibu na usimamizi wa shughuli za afya. Magari hayo yamepelekwa kwenye mikoa na halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ilipokea gari moja la uratibu na usimamizi wa shughuli za afya na magari mawili ya kubebea wagonjwa ambapo gari moja lipo Kituo cha Afya Kilasilo na lingine Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Kwa sasa Kituo cha afya Ipinda kinahudumiwa na gari la wagonjwa lililopo Hospitali ya Wilaya ya Kyela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili kuendelea kununua magari ya kubebea wagonjwa na kuyapeleka kwenye halmashauri zenye upungufu ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO aliuliza: -
Je, lini Barabara ya Ipyana – Kasumulu – Ileje itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Baraka Ulimboka Mwamengo, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Ipyana – Kasumulu – Ngana – Ndembo – Ileje eneo la Isongole lenye urefu wa kilometa 114.3 ambapo kwa sasa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii imefikia 96%. Aidha, Serikali imeanza ujenzi wa barabara hii sehemu ya Isongole II – Ndembo pamoja na barabara ya kuingia Ndembo – Isoko yenye urefu wa kilometa 52 ambapo ujenzi umefikia 10.75%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu ya Ipyana – Kasumulu – Ngana hadi Ndembo kazi ya kufanya uthamini wa nyumba na mali kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaoathiriwa na mradi huo inategemea kuanza hivi karibuni.