Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii kuweza kuongea ndani ya Bunge hili Tukufu kwa mara yangu ya kwanza nikisimama hapa kama Mbunge wa Viti Maalum kupitia kundi la wafanyakazi kutokea Mkoa wa Mjini Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sana kuwashukuru Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa UWT ukiongoza na Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Taifa UWT, Mama Mary Pius Chatanda. Wajumbe hawa walisababisha mimi kuonekana na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua na kuniamini kuona ninaweza kuungana na Wabunge kupitia Bunge hili la Kumi na Tatu ili niweze kuwawakilisha wanawake wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sana pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wake wa kishindo wa 97% kupitia Chama Cha Mapinduzi. Pia ninapenda kumpongeza Spika ambaye yuko ndani ya Bunge hili pamoja nawe Naibu Spika pamoja na Wenyeviti, Waheshimiwa Wabunge wote waliomo ndani ya Bunge hili kwa ushindi wa kishindo mlioupata na kuhakikisha mmeteuliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Kumi na Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Dkt. Emmanuel Nchimbi, Msaidizi wa Mama Samia Suluhu Hassan, Msaidizi wa Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu ambaye aliteuliwa na kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Mtendaji Mkuu wa Serikali. Ninawapongeza pia Mawaziri na Waheshimiwa Manaibu Waziri wote ambao wanamsaidia Rais katika kufanya kazi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa upekee kabisa, ninapenda kuwapongeza sana Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ambaye aliwasilisha Mpango Elekezi wa Maendeleo wa muda mrefu, muda wa kati na Mpango pia wa mwaka 2026/2027. Pia, ninapenda kumpongeza kaka yangu Khamis Mussa, Waziri wa Fedha naye aliwasilisha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 – 2028/2029. Ninapenda sana kupongeza kwa weledi waliotumia katika kuwasilisha mpango huu pamoja na bajeti hiyo ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uwasilishaji wa mwongozo huo pamoja na bajeti hiyo, ninaomba kujielekeza katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni sekta ya utalii ambapo kwenye sekta ya utalii tumeona imeendelea kuwa nguzo muhimu kwa uchumi wa Taifa na kuchangia 27% ya pato la Taifa kwa mwaka 2024. Mafanikio makubwa hayo, yametokana na ongezeko kubwa la idadi ya watalii kutoka watalii milioni 1.8 mwaka 2023 na kufikia milioni 2.14 kwa mwaka 2024. Mapato pia kuongezeka kutoka dola za Kimarekani bilioni 3.37 kwa mwaka 2023 na hadi kufikia bilioni 3.9 kwa mwaka 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kuendeleza uchumi wa Taifa kufikia malengo ya muda mrefu. Kamati pia ya Bajeti imechambua shabaha mbalimbali na ikapendekeza Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vidogo vya ndege katika maeneo yenye vivutio vya utalii na kurahisisha usafiri wa watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapenda kumpongeza sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa makusudi kabisa na kwa uthubutu wake mkubwa, aliamua kutengeneza filamu ya “The Royal Tour” katika kuongeza, kuinua uchumi wa Nchi hii ya Tanzania kutokana na sekta hiyo ya utalii. Pia ninaomba kumpongeza Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuwa bega kwa bega katika kumtia moyo na kumwongezea nguvu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutengeneza filamu hii ya ‘The Royal Tour’.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona viongozi hawa waliitengeneza filamu hii, Dkt. Samia aliitengeneza filamu hii akiwa ardhini, akiwa angani, akiwa baharini kwa kushirikiana na Dkt. Hussein Mwinyi ambapo nilifurahi sana nilipowaona wakiwa baharini, walifikia hatua ya kuvutia kivutio hiki cha utalii kwa kuvua samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemwona daktari huyu uthubutu wake ulivyo mkubwa, walimtoa samaki kwenye maji wakamleta juu; ni Rais wa pekee ambaye alifanya tukio hilo, mimi sijawahi kuona. Tumpongeze sana Daktari Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema nini katika eneo hili? Katika eneo hili ninaendelea kusisitiza kwamba, Serikali ihakikishe utekelezaji wa mikakati wa kukuza na kuhamasisha aina mbalimbali za utalii ikiwemo utalii wa picha, michezo, matibabu, mikutano, fukwe za bahari, utamaduni na urithi wa kihistoria ambao haujatumika ipasavyo. Vilevile, jumuishi za hifadhi na wanyamapori ziendelee kuimarishwa ili kuongeza thamani ya vivutio vya utalii. Hatua hizi zitasaidia kuongeza idadi ya watalii, mapato ya kigeni na mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuligusa ni la wakandarasi wazabuni pamoja na watoa huduma. Tumeona katika uwasilishwaji wa mpango huu umeguswa uimarishaji wa mifumo ya kidigitali. Sasa hapa katika uwasilishwaji nimeona changamoto moja kubwa inayoikabili Serikali; ni malimbikizo ya madeni ya wakandarasi; wazabuni na watoa huduma. Changamoto hizi zinatokana na mambo kadhaa ikiwemo ucheleweshaji na uhakiki wa madai, ukosefu wa fedha za kutokana na mapato ya ndani yasiyo thabiti pamoja na urasimu katika utaratibu wa malipo. Hali hii imekuwa ikidhoofisha uwezo wa wakandarasi na wazabuni kuendelea kutoa huduma bora na wakati mwingine kusababisha kusimama kwa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sikusimama tu kwa miradi ya maendeleo; tumeona vijana wetu wengi wamekuwa wakipata ajira kwenye eneo hili. Wazabuni na wakandarasi wanapofanya kazi basi wao wanakuwa msaada mkubwa wa kutoa ajira kuisaidia pia Serikali kuwapa vijana wetu ajira. Pale tunapokosa kuwalipa kwa wakati; kumbuka wanajaribu kulipa, wanalipa, lakini mwisho wa siku na wao wanashindwa kuwafanyia malipo vijana. Vijana wanalalamika huko mitaani. Wanapolalamika mitaani inasababisha kuonekana kuwa tatizo kubwa ni kiongozi wa juu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba kwenye upande huu kwanza mifumo ya uhakiki wa madai iimarishwe katika teknolojia ya kidigitali ili kupunguza urasimu na kuongeza uwazi; Serikali ihakikishe kuwa bajeti ya miradi zinatengwa kwa uhalisia na fedha za kutosha zinapatikana kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo; kuwe na utaratibu wa kipaumbele katika malipo ambapo wakandarasi na watoa huduma wanahusika na miradi ya mkakati ya kijamii watalipwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. (Makofi)