MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira vijana wanaojitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Edward Mwakyembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, Toleo la Pili, ikisomwa pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 na Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma wa Mwaka 2025, ajira katika Utumishi wa Umma hupatikana kwa ushindani na uwazi. Kujitolea katika Utumishi wa Umma huwezesha vijana kujipatia ujuzi wa ziada pamoja na kuwapa uzoefu na uwezo wa kushindana pindi ajira zinapotangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vijana wote wanaohitimu vyuo wanapata fursa ya kujitolea katika Taasisi za Serikali hivyo, utaratibu uliopo wa ushindani unatoa fursa sawa kwa vijana wote wanaojitolea na ambao hawajapata fursa ya kujitolea. Ahsante.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Edward Mwakyembe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kugharamia ulipaji wa madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2025/2026, shilingi bilioni 700 zilitengwa ambapo hadi Februari, 2026 jumla ya shilingi bilioni 477.6 zimetolewa. Kadhalika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 800 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kugharamia ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa suala la madeni ya wakandarasi na wazabuni linadhibitiwa, Serikali inaendelea kutoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kupitia waraka mbalimbali za utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti katika mwaka husika. Maelekezo ya Serikali ni kama yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafungu kutenga bajeti kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi, lakini pia Maafisa Masuuli kutumia mifumo ya kudhibiti matumizi hali kadhalika kuhakikisha kuwa mchakato wowote wa ununuzi unaanzishwa baada ya kujiridhisha uwepo wa bajeti na uhakika wa upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha ninaomba kuwasilisha. (Makofi)