Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lucy Edward Mwakyembe (5 total)

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ni utaratibu gani unaotumika kwa kutumia mkongo wa Taifa katika kupeleka mawasiliano kule Zanzibar ili kufikisha huduma kwa wateja kwa haraka sana na kwa maeneo ambayo hayafikiki?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaotumika katika kupeleka mawasiliano Zanzibar kupitia mkongo wa Taifa, huwa kwanza inafanyika tathmini, kuangalia uhitaji wa maeneo husika, ikishafanyika, Shirika la Mawasiliano Nchini hupeleka mawasiliano hayo kulingana na uhitaji wa eneo husika.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Tanzania imepata bahati mwaka 2027 kuendesha michezo ya AFCON katika upande wa Bara na Zanzibar, ninataka kujua, kwenye upande wa utalii, wafanyabiashara ndogo ndogo na wajasiriamali nao ni sehemu ya fursa ambayo wameipata kwa ugeni utakaoingia. Je, ni elimu gani imetolewa mpaka sasa, au Serikali imejipanga vipi kutoa elimu kwa wafanyabiashara ndogo ndogo pamoja na wajasiriamali, hususan wanawake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imejipanga vya kutosha kupokea mashindano hayo ya AFCON. Hivi ninavyokwambia, wataalamu wetu wako site, wameshaanza mafunzo na taratibu mbalimbali za wajasiriamali wetu ili kusudi waweze kupokea vizuri, na wanapokuja watu kutoka nje kwa ajili ya michezo, wasiwe wameondoka tu na michezo, bali waende kwenye vivutio vyetu na wajasiriamali wetu nao wawe wanufaika kupitia mashindano hayo ya AFCON.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninamshukuru Naibu Waziri, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, ndugu yangu, Mheshimiwa Regina Ndege, kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira ya Mwaka 2008, Toleo Namba Mbili pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 na Mwongozo wa Kujitolea wa Mwaka 2025. Ninaomba nitoe ushauri, Mwongozo huo wa Mwaka 2025, basi ufike haraka katika Taasisi za Serikali, pamoja na Taasisi za Sekta Binafsi ili watumishi hawa wa kujitolea wanapopata huduma hii iwe katika uwiano katika taasisi tofauti. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Lucy kwa namna anavyoendelea kuwasemea watumishi na vijana wa nchi hii. Ushauri wake tumeupokea. Hata hivyo, ninapenda kulihakikishia Bunge lako kwamba, utaratibu tuliouweka, kama Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni kwamba, mwongozo tayari umetoka. Hatua iliyobaki ni kuhakikisha mwongozo huo unasambazwa na kufika kwenye taasisi zetu za umma na kwenye idara na Wizara mbalimbali, ili uanze kutumika, kwa ajili ya kuwapata vijana ambao wapo tayari kujitolea katika utumishi wa umma. (Makofi)
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninamshukuru sana Naibu Waziri kaka yangu Mheshimiwa Munde kwa majibu mazuri ya Serikali pamoja na mikakati ambayo imewekwa kwa ajili ya ulipwaji madeni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Serikali inaendelea kutekeleza upatikanaji wa ajira milioni nane ambazo zimeainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi mpaka kufikia mwaka 2030 na pia niwapongeze sekta binafsi ambapo zinavyoongeza kuongeza ajira za vijana wa kike na kiume katika kutekeleza Ilani hiyo ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza. Serikali ina mpango gani katika kusimamia madeni hayo yasiongezeke hasa ya wazabuni na wakandarasi wazawa ili kuendelea kulinda mitaji yao na wao hao kuendelea kulinda ajira za vijana wa kike na wa kiume, lakini pia na kuhakikisha madeni ya watumishi yanalipwa na madeni ya watumishi hayaongezeki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Edward Mwakyembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli madeni ya wazabuni na wakandarasi pamoja na watumishi ni kero ambayo Wizara imeipata, lakini pia kupitia Wabunge mbalimbali jambo hili limekuwa likiongelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuliona hilo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kesho siku ya Jumatano, tarehe 20 Mei itakutana na Wizara ya Fedha katika kutafakari na kuhakikisha kwamba madeni hasa hasa ya wazabuni na wakandarasi wa ndani yanaweza kulipwa ili uchumi uweze kuzunguka lakini pia vijana ambao wamefanya kazi kwenye miradi hiyo waweze kupata kujikimu na kuinua vipato na uchumi wa mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)

MHE. LUCY EDWARD MWAKYEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali kwa ajili ya uanzishwaji wa bima hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo ndiyo suluhisho la kumkomboa Mtanzania katika ajira, wakiwemo vijana, je, Serikali inaonaje kuongeza kasi ya utafiti katika kukamilisha na kutumika bima hiyo hasa kwa upande wa bima ya mazao, mvua nyingi, ukame, wadudu kwenye mimea, pamoja na dhoruba. Matukio haya yanasababisha wananchi kupata majanga ya asili ambapo bima ikianza kwa haraka walau itampunguzia maumivu mwananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri la nyongeza, kwanza bima hii ya kilimo, nikiri kabisa kwamba imeanza kama miaka miwili au miaka mitatu huko nyuma. Kwa maana hiyo, katika hali ya kawaida kulingana na maoni ya wadau ambayo tumeendelea kuyapokea mpaka sasa hivi, jambo hili na utafiti huu ulitakiwa uchukue muda mrefu zaidi wa miaka hii miwili au mitatu ambayo sisi kama Wizara ya Fedha tunaweza kutumia.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, yeye ameuliza kwamba kuona namna ya kuweza kuharakisha; kwanza sisi kama Wizara ya Fedha tumeharakisha na kwa sababu hiyo, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, uharakishwaji huo na ndiyo maana tunaenda kutekeleza zaidi, kanuni hizi katika mwaka wa fedha 2026/2027 kuanzia Julai 1, 2026.