Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Moses Charles Bujaga (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi hii, na mimi kipekee kabisa, ninapenda nianze kumpongeza Waziri kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa jana. Ninawapongeza watendaji wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ndugu Gerald Mweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri kwa sababu ameonesha wazi kwamba yuko tayari kuweka mwendelezo kwenye sekta hii ya kilimo. Sekta ya Kilimo inahitaji uwekezaji wa muda mrefu. Matokeo ya uwekezaji katika Sekta ya Kilimo hayatokei ndani ya muda mfupi. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu, katika hotuba yake ameonesha jinsi ambavyo ataendeleza programu za maendeleo ambazo zimeanza chini ya Kesho Iliyo Njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, ameonesha ni namna gani ambavyo bajeti yake imejikita katika Dira ya Maendeleo 2050. Jambo moja la msingi sana ambalo bajeti ya Mheshimiwa Waziri imesema ni kwamba, ameangalia mpango na bajeti, mpango kabambe wa mageuzi ya kilimo 2050. Tanzania Agricultural Masterplan haijawekwa wazi kwetu, kwa hivyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri asiweke mpango huu kwenye shelf za ofisini kwake. Mpango huu uwe ndiyo kipimo cha namna gani kilimo chetu kinafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa sababu, ameonesha umuhimu wa kuendeleza miradi ya umwagiliaji, miradi ambayo kwa namna fulani imesimama kwa muda mrefu, lakini Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba, itaendelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, miradi ya umwagiliaji ambayo iko Wilaya ya Kwimba, hususan Jimbo la Sumve, ipewe kipaumbele kwa sababu, sasa hivi wananchi wa Jimbo la Sumve ni wazalishaji wakubwa wa zao la mpunga. Katika Wilaya ya Kwimba peke yake tunazalisha zaidi ya tani 60,000 hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 120.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri ni kwamba, ametambua umuhimu wa kuongeza tija kwenye mazao ya kilimo. Tatizo la wakulima wetu limekuwa ni ongezeko ama uduni wa uzalishaji na ameonesha kwa uwazi kwamba, tija ndiyo mwelekeo, lakini jambo moja ambalo Mheshimiwa Waziri hakulisema sawasawa, ameongelea tu ukuaji wa uzalishaji wa mazao asilia, hajaongelea ni namna gani tija itaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema 2025 mazao ya biashara asilia tulizalisha tani 1,600 tunatarajia sasa 2026 tuzalishe tani 2,118, lakini Mheshimiwa Waziri hajatuambia ni kwa namna gani zao la pamba, kwa mfano, ambalo tija yake mpaka sasa hivi tuko 20%, tunapanda vipi kufikia kilo 1,000 kwa hekta. Kwenye zao la korosho tuko 18%, tunapanda vipi kutoka kilo nne na nusu kwa mti, kwenda kilo 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku tunafanya vizuri, tuko 77%, tunazalisha kilo 1,400 kati ya kilo 1,800. Sasa, kilimo ni takwimu, tunahitaji numbers kuona namna gani tunatoka kwenye uzalishaji duni, ili wananchi wetu ambao amesema ni wawekezaji (kilimo ni biashara na mkulima ni mwekezaji), ni namna gani wanatoka kwenye uzalishaji duni, ili wazalishe kwa tija na tuwaondoe katika umaskini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ndugu yangu, Mheshimiwa Mbunge kutoka Kwimba amezungumzia jana. Mkoa wa Mwanza tunazalisha 20% mpaka 25% ya mazao jamii ya mikunde. Wakulima wa Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Magu, Wilaya ya Kwimba, Wilaya ya Sengerema na Wilaya ya Misungwi wanapanda kwa nguvu zao, wanalima kwa nguvu zao, wanatafuta mbegu kwa nguvu zao; wanapovuna wanakuja watoza ushuru. Anapovuna tunamwona COPRA na TMX.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wanachajiwa shilingi 230 kwa kilo moja ya choroko, kwa kilo moja ya dengu. Sasa tunataka hawa watoza ushuru wajue kuwekeza kwa wakulima wetu ili unapokuja wakati wa mavuno washiriki nasi katika ulimaji, na upandaji, ili waweze kufaidika na kile tunachokivuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anasema zitanunuliwa mashine 100 za kusafisha, kuchambua na kupanga madaraja ya zao jamii ya mikunde na zitasambazwa kwa AMCOS, kwenye mikoa mingine, lakini Mwanza haimo. Tunataka Mheshimiwa Waziri anapokuja kufanya majumuisho jambo hili aliseme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la agriculture financing structure. Sasa hivi mifuko mingi ya mazao ipo kwa ridhaa ama kwa utaratibu wa Waziri peke yake. Ninapendekeza Mfuko kama wa Pamba CDTF, Mfuko wa Korosho Export Levy, Mfuko wa Maendeleo ya Sukari Agriculture Development Fund, itengenezewe legal framework, ili iwepo kisheria, isiwe tu kikanuni.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)