MHE. MOSES C. BUJAGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya ujenzi wa Vituo vya Afya Walla, Mwambomba, Mwagi, Mhandi na Mwamala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Moses Charles Bujaga, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025 Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini, zikiwemo Kata za Isunga, Kadashi, Kikubiji na Hungumalwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Disemba, 2025 Serikali ilikuwa imekamilisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya 898 ambavyo vinatoa huduma ngazi ya kituo cha afya ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa kujenga vituo vya afya katika Kata za kimkakati ikiwemo Kata ya Walla ambayo imetengewa jumla ya shilingi milioni 250 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Utekelezaji utaendelea kwenye Kata zitakazokidhi vigezo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kadiri fedha zitakavyopatikana. (Makofi)
MHE. MOSES C. BUJAGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Malya – Nyambiti (kilometa 58) ili kuboresha usafirishaji katika Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moses Charles Bujaga, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Malya – Nyambiti, kilometa 58 kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kufahamika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.