Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Moses Charles Bujaga (3 total)

MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kuja Mji Mdogo wa Malya umesimama. Swali langu ni kutaka kujua, ni lini mkandarasi atalipwa fedha ili arudi kazini na kukamilisha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Moses Charles Bujaga, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mradi ule unaopita Hungumalwa – Malya kwenda kule Sumve, na pia mradi huu unaenda mpaka kwa Mheshimiwa Mashimba Ndaki. Mheshimiwa Mbunge tulishakaa pamoja na mkandarasi kwa pamoja tukakubaliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninaomba sasa nimhakikishie kwamba ule mpango wa kuhakikisha kwamba analipwa, tumeweka kipaumbele katika kipindi hiki cha miezi miwili ili mkandarasi aweze kulipwa na arudi site, kwa sababu tunajua kuna matanki ambayo tayari ameshayajenga, lakini kuna kilometa kadhaa za kulaza mabomba ili aweze kumalizia na kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanaweza kunufaika na huduma ya majisafi na salama. Ninakushukuru sana.
MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, ningependa kuongeza maswali madogo mawili. Kituo cha Afya Budushi kina daktari mmoja, Kituo cha Afya Kadashi kina daktari mmoja, na Kituo cha Afya Isunga hakuna daktari. Ningependa kujua Serikali ina mpango gani wa dharura kuhakikisha kwamba tunapata watalamu katika vituo hivi vitatu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kituo cha Afya Budushi hakina gari la kubeba wagonjwa inapotokea dharura ya kupeleka wagonjwa hao kwenye Hospitali ya Wilaya iliyoko kilometa 33. Je, Serikali itatupatia lini gari la kubeba wagonjwa Kituo cha Afya Budushi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza na ninaomba niyajibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu upungufu wa madaktari na ndiyo maana tulipata vibali vya kuajiri madaktari 5,000 nchi nzima na baadhi ya madaktari wameshafika maeneo yao ya kazi. Ninawaomba madaktari waliopangiwa kwenda kwenye vituo vyetu vya afya ili wafike kwa wakati, lakini kama haitoshi nimwelekeze Mkurugenzi kuendelea kutoa ajira zile za lazima hasa kwenye maeneo ambayo tuna upungufu kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya kubebea wagonjwa, tayari tulishapeleka magari zaidi ya 594 katika maeneo yetu kwa Halmashauri zote nchini, lakini pia tunaendelea kuomba magari. Kadiri tunavyoyapokea kutoka Wizara ya Afya, tutaendelea kuyaelekeza katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)
MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, barabara hii ya Fulo - Nyambiti – Malya ilitakiwa kukamilika huo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kufikia mwezi wa Aprili, 2026. Ningependa kufahamu ni kwa nini kazi hiyo haijakamilika mpaka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, barabara hii kwa sasa iko katika hali mbaya sana na ndiyo inayobeba uchumi wa Jimbo la Sumve, minada ya Bungulwa, usafirishaji wa mazao kama dengu na pamba ambayo ndiyo msimu wa sasa hivi utakuwa ni changamoto. Serikali ina mpango gani kuhakikisha barabara hii inapitika, ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na usafiri wa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Moses Charles Bujaga, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali napenda kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa ni mtu wa shukrani ya kutambua kazi nzuri ambayo inafanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye eneo lake, lakini pili, amekuwa ni mfuatiliaji makini, kwa huu muda mfupi wote tunashuhudia, anavyopigania barabara za jimbo lake na hata za mkoa wake kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, ameuliza kwa nini haijakamilika katika muda uliokuwa umepangwa; moja, mhandisi mshauri alikuwa ameshakamilisha ile kazi, lakini kama unavyofahamu, mahitaji yanazidi kuongezeka. Timu ya wataalam ikapitia na kubaini kwamba kuna mambo mengine ambayo yakiongezwa, yatakuwa na maslahi mapana zaidi kuliko walivyofikiria pale awali na kimsingi jambo hili ni jambo jema kwa sababu pengine barabara ya awali ilikuwa inakusudiwa, ilitazamiwa kwa mahitaji ya pale mwanzoni.

Kwa hiyo, wataalamu wakaona iko haja kufanya maboresho, ili barabara itakayofikiwa kuamuliwa kujengwa, iendane na ndoto na matamanio ya yeye Mbunge, wananchi na Taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, nimwombe awe na subira, kwa sababu baada ya hatua hii sasa, tumemwongezea mkandarasi muda, angalau mpaka kabla ya mwezi wa Agosti au kabla ya mwaka huu haujaisha ili kazi hii iwe imekamilika.

Mheshimiwa Spika, la pili; ameuliza kwamba barabara hii imekuwa ni mbovu ambayo kimsingi sisi Serikali tunakubaliana na yeye na tunampa pole kwa changamoto hiyo, kawaida barabara hii itakiwa ifanyiwe ukarabati mara mbili kwa maana mwezi wa 10 pamoja na mwezi Mei mpaka Juni. Mwaka jana mwezi wa 10 ukarabati mzuri ulifanyika, sasa kipindi kama hiki ambacho wakulima na wananchi wanakusudiwa kusafirisha mazao mbalimbali kama vile pamba, dengu na mazao mengine barabara hiyo kweli ni mbovu.

Mheshimiwa Spika, tayari taratibu zimeshaanza kufanyika ili mkandarasi huyu sasa aingie kazini hivi karibuni na namwelekeza kwa Niaba ya Waziri wa Ujenzi amenituma nimwelekeze Meneja wa TANROADS ili alisimamie jambo hili mkandarasi huyo aingie kazini, aanze kufanya kazi na aboreshe barabara hii ili wananchi wa Sumbe na Mkoa wa Mwanza na maeneo jirani kwa ujumla waweze kunufaika na barabara hii na kujenga uchumi wao.