Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. MAGRETH B. EZEKIEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuanza kwa kutoa shukrani ya dhati kwa ajili ya kupewa nafasi hii adhimu ya kuchangia maoni na ushauri kwenye Mpango wa Maendeleo wa Serikali, Dira ya Maendeleo 2020 – 2050, Long Term Perspective Plan pamoja na the Fourth and Fifth-Year Development Plan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii adhimu kwa unyenyekevu na moyo wa shukrani wa dhati kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai, pumzi na fursa ya kusimama katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa na kwa moyo wa shukrani na upendo, ninapenda kumshukuru mama yangu kipenzi changu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua na kunipa dhamana ya kuwa Mbunge wa Viti Maalum nikiwakilisha mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kuwemo Bungeni miaka 24 niliyonayo ni ushuhuda tosha kwamba Mheshimiwa Rais ana mapenzi makubwa na sisi vijana. Pia, kwa nafasi hii ninaomba vijana wote watumie nafasi yangu humu Bungeni kama ushuhuda kwamba tuna nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya Taifa letu la Tanzania na kwamba tuna Serikali sikivu inayotupa sikio la kutusikiliza na kutuwezesha katika yote tunayoyafikiri katika kulijenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi pia kumshukuru na kumpongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa uadilifu, kwa nguvu zake zote na kwa wivu mkubwa kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Waziri Mkuu na Baraza zima la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayofanya. Nimefanya utafiti wa kuwatembelea na kuwasalimia Mawaziri zaidi ya 70% na wote wameonyesha utashi wa kutaka kuwasaidia vijana kwa nguvu zao zote. Katika Mawaziri hawa, 40% ya Mawaziri walioteuliwa ni vijana. Kwa hiyo, dhahiri inaonyesha kuwa katika kila hatua Mheshimiwa Rais ameweka jitihada ya kutuinua, ya kutuwezesha na kutujengea uwezo, akijua kwamba kesho ya Taifa letu ipo chini ya mikono yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa ninapenda kuwashukuru wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wakiongozwa na mama yangu kipenzi Mary Pius Chatanda. Wanawake hawa ninawashukuru kwa kunilea kisiasa, kunibariki, kunikopesha imani na kunipa kura nyingi. Ninaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu na Watanzania kiujumla kuwa nitalitumikia Taifa kwa juhudi kubwa, kwa uadilifu, moyo wa dhati na wivu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini dhahiri, uzalendo mkubwa ni kulitumikia Taifa kuhakikisha amani na uchumi endelevu. Taifa hili linajengwa na mimi, Taifa hili linajengwa na wewe na Taifa hili linajengwa na sisi sote Watanzania na katika udongo huu tuliozaliwa ndiyo udongo huu tutakaozikwa na siku moja kuwarithisha watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa shukrani na unyenyekevu mkubwa ninapenda kuwashukuru wanawake wote wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuonesha wazi na dhahiri kwamba sisi wanawake tuna nafasi kubwa ya kuendelea kutenda kwa maadili mema, kwa uthubutu, na kuendeleza kuwalea mabinti na wanawake wengine katika nafasi za uongozi tukielewa kwamba kuwepo kwetu sisi inaleta chachu ya maendeleo kwa Taifa kiujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu pia nichukue fursa hii kutuma salamu za shukrani ya dhati kwa baba yangu Baraka Ezekiel kwa kuthibitisha kuwa uchimbaji ni kitu ambacho kinaweza kurithishwa na ni biashara kama biashara nyingine. Nimezaliwa kwenye familia ya uchimbaji, vile mnavyoniona, elimu yangu, afya yangu, mimi kuwepo humu Bungeni vyote vimechangiwa na rasilimali zilizotokana na madini na Sekta ya Madini kiujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninapenda kutuma shukrani nyingi za upendo kwa wachimbaji wote Tanzania kwa kunilea na hususan wachimbaji vijana milioni nne walionipa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wao katika Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa kuna mambo machache yaliyozungumzwa nami ningependa kuyachangia. Ninapenda kuipongeza Serikali kwa kuweka umakini na umuhimu kwa vipengele mbalimbali katika Sekta ya Madini ikiwa kwamba katika Bunge hili nimekuwa nikisikiliza mawasilisho mbalimbali na katika kila Wabunge 10 wanaosimama basi Wabunge sita au Wabunge wanne wanasimama kuiongelea Sekta ya Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Madini ni uti wa mgongo, ni kitovu, ni moyo wa uchumi wa nchi yetu. Ninaipongeza sana Wizara ya Mipango kwa sababu wameweka katika flagship projects zao, wameweka Dodoma Central Minerals and Innovations Hub. Hii Central Mineral and Innovation Hub italeta chachu ya kufanya tafiti na uangalizi kwamba ni namna gani madini yanaweza kutunufaisha sisi, pale ambapo tunalenga kupata uchumi wa shilingi trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Hatuwezi kufikia uchumi wa shilingi trilioni moja kama hatutatumia rasilimali zetu za madini kiukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea suala zima la National Sovereignty Wealth Fund, nilikuwa Saudi Februari ya mwaka uliopita na nimeona jinsi gani Sovereignty Wealth Fund zao zimefanikiwa. Leo Saudi inatoka kwenye mafuta inaenda kwenye viwanda, inaenda kwenye kutengeneza betri na magari, na kwenye uchumi mwingine wezeshi. Hii yote inatokana na uwekezaji kwenye Sovereignty Wealth Fund. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu issue ya Liganga na Mchuchuma; hakuna sekta itakayoendelea, si Sekta ya Viwanda, si sekta yoyote wezeshi ya uchumi bila chuma. Chuma ni kitu pekee ambacho kinaweza kukutengenezea viwanda zaidi ya 1,000 hadi 2,000. Hivyo, ninapongeza sana Liganga and Mchuchuma Iron Complex Centre. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaenda kwenye mada maalum na mada ambayo inatulenga sisi vijana. Dira ya maendeleo ya sisi vijana, mfano mimi Magreth leo nina miaka 24, inamaanisha miaka 25 nitakuwa na miaka 50. Kwa hiyo, ninapaswa katika miaka 25 yangu nielekeze nguvu zangu, akili yangu na rasilimali zangu katika kuhoji. Je, katika mpango wa maendeleo nina nafasi gani ya ku-play? Kwa sababu tunapoangalia sasa hivi kwenye dunia tumeingia katika vita kubwa ya uchumi na vita kubwa ya teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaongelea suala zima la Artificial Intelligence. Sasa, Artificial Intelligence tunaongelea kazi ambazo zinafanywa na binadamu kwa sasa hivi, ndani ya miaka mitano, ndani ya miaka 10 na ndani ya miaka 20 zitakuwa zinafanywa na robots. Mpaka sasa hivi Kampuni ya Elon Musk imetangaza by 2027 unaweza ukanunua your own human robot kwa dola za Kimarekani 75,000. Je, vijana hawa ambao sasa hivi tunaenda kusema tunawapa ajira tumewaandaa vipi katika global market competitiveness in Artificial Intelligence? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunaongelea mtu kwenda kupambana na robot, huwezi kupambana na roboti, huwezi kupambana na AI. So katika dividend ambayo tunaiongelea (demographic dividend) inaenda kuwa demographic bomb. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii demographic bomb ni kwa sababu gani? Kwa sababu kuna vijana wengi ambao wanategemea ajira. Ajira nyingi zilikuwa kwenye kilimo lakini sasa hivi vijana wengi hawataki kilimo kila mtu anataka desk work. Hivyo kwa mapendekezo yangu nilikuwa napendekeza mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia. Sisi kama Tanzania kwenye Mpango wetu wa maendeleo tuweke mkakati wa kuanzisha The Tanzanian Artificial Intelligence Framework pamoja na The Tanzanian Employment and Unemployment Desk ambayo itaweka National accountability kwa vijana kwamba, kwenye miaka 25 ya maisha yako, wewe una mchango gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaomba kuwasilisha. (Makofi)