Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Silvery Luboja Salvatory (3 total)

MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa vijiji 16 vya Gukwa Buhunda, Mwagimagi, Kifune, Busongo, Nyambiti, Kabale, Buhingo, Seke, Songiwe, Mwasagela, Mbalama, Nyamayinza, Gulumungu, Ng’hamve pamoja na Itogwang’holo viko kwenye Mradi wa Maji wa Ihelele unaopeleka maji Mikoa ya Shinyanga na Tabora, na unaanzia kilometa zero kutoka kwenye chanzo cha maji; Tangu uzinduliwe mwezi Juni, 2009 wananchi hawa hawajawahi kupata maji ilhali maji yananyewa Sikonge. Je, sasa Serikali haioni ni wakati umefika wananchi hawa na wao waweze kupewa maji kwa haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa maji ni uhai, je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuwapatia wananchi hawa maji kwa haraka ili kuokoa afya zao? Ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salvatory, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwenye upande wa Misungwi Serikali imefanya kazi kubwa sana. Upatikanaji wa maji wa sasa wa Misungwi ni 68%, lakini Serikali imetekeleza zaidi ya miradi 15 na yenye gharama ya shilingi bilioni 15.6, lakini miradi inayoendelea kwa sasa ni nane yenye gharama ya shilingi bilioni 69. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Misungwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata huduma ya majisafi na salama, lakini kati vijiji 94 vyote tayari vina maji na vijiji vinane ndivyo ambavyo bado tunahakikisha kwamba mradi huu unaoendelea utakapokamilika pamoja na vile vijiji 16 vyote vitapata huduma ya majisafi na salama. Tunafahamu kwamba maji ni uhai, lakini maji ni uchumi. Tunafahamu kwa kuwawezesha wananchi wa Misungwi wataweza kufanya shughuli zao za kiuchumi, lakini pia wataweza kutumia majisafi na salama kwa ajili ya kunywa, ahsante sana.
MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninakubaliana na mpango wa Serikali wa kutengeneza barabara kwa awamu kwa sababu za kibajeti, lakini majibu ya Mheshimiwa Waziri ni tofauti kabisa na hali halisi iliyoko site kwa kuwa Serikali haijasema kweli. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea hizo 40% za ujenzi wa kilometa tatu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ninaomba Serikali sasa iwaambie wananchi wa Mwanangwa, Misasi, Buhingo, Busongo, na Nunduru, ni lini barabara yao itaanza kujengwa kiukweli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mkandarasi alishafanya kazi na ndiyo maana alishaomba hata malipo baada ya kufanya kazi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulichoandika hapa, niko tayari kwenda na Mheshimiwa Mbunge kuona kile ambacho kimefanyika, lakini huku Serikali ikiwa inaandaa malipo ya huyo mkandarasi ili aweze kuendelea na kazi.

Mheshimiwa Spika, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni dhamira ya Serikali na ndiyo maana tumeanza kuijenga kwa awamu tukisubiri kupata fedha nyingi ambayo tutakamilisha kuijenga barabara hiyo ya Misungwi mpaka Kahama.

Mheshimiwa Spika, tusingekuwa na dhamira ya dhati tusingeanza, lakini tumeona wakati tunapata fedha kiasi, basi tuendelee kupunguza kazi, lakini tutakapokuwa tumepata fedha yote, mpango wa Serikali ni kujenga barabara yote kutoka Misungwi hadi Kahama kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa kuna kila dalili ya kwamba mkandarasi amekwishapatikana na wakati wowote ataanza kazi. Je, Serikali iko tayari kuanza upanuzi wa barabara hii kutokea Usagara kuelekea Mjini ukizingatia ukweli kwamba eneo la Usagara halihitaji uhamishaji wa miundombinu kama vile mabomba na taa za barabarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa upanuzi wa barabara hii unaenda kufungua shughuli za kiuchumi. Je, Serikali iko tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami; Barabara ya Fulo – Nyambiti hadi Malya yenye urefu wa kilometa 73 kwani barabara hii inauhusiano mkubwa na dry port pamoja na SGR itakayokuwa kule Fela na itapita kwenye kata yangu ya Fela – Kolomije pamoja Kanyelele?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Mheshimiwa Silvery Luboja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana na nimpongeze sana kwa umahiri wake kwenye kufuatilia hoja za wananchi wa pale Misungwi ambazo ukizitazama zinabeba vilevile eneo lote la Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Usagara kwenda Mwanza Mjini ama Mwanza Mjini kuja Usagara kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi la awali, ni kwamba ni barabara ya kimkakati na ni barabara muhimu sana na kwa kweli kwa sasa ni barabara ambayo ina msongamano mkubwa hasa mara baada ya ukamilifu wa Daraja la Kigongo – Busisi kama lilivyotamkwa maarufu Daraja la John Pombe Magufuli. Msongamano umeongezeka sana kwa sababu ni daraja limeleta msisimko mkubwa wa shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tunatarajia pale Mwanza tutakuwa na kituo kikubwa cha SGR, kwa hiyo kitaongeza zaidi ule msongamano wa eneo lile, rai ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tusianzie Mwanza Mjini, tuanzie Usagara kuelekea Mwanza Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu kwamba ushauri huu na rai hii ya Mheshimiwa Silvery Luboja, Mbunge wa Misungwi nimeipokea na nitaifikisha katika jopo la watalaamu, tutaitathmini na kuona kwamba ni namna gani tunaweza kutekeleza either kuanzia Usagara kwenda Mwanza Mjini au kuanzia Mwanza Mjini kurudi Usagara, lakini kwa hakika ushauri wake nimeupokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; anasema kwamba kutokana na maendeleo haya mazuri yanayoendelea katika eneo hili yanapelekea umuhimu wa kuifungua Barabara ya kutoka Fulo mpaka Nyambiti mpaka Malya na ni kweli barabara hii ni muhimu ambayo itapeleka muunganiko mpaka Sengerema kwa Mheshimiwa Tabasam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba na yenyewe tunaikamilishia upembuzi yakinifu na mara baada ya kuwa tumekamilisha upembuzi yakinifu wake tutapata gharama halisi na katika lengo lile la kuondosha msongamano katika miji haswa Jiji la Mwanza, barabara hii na yenyewe ni muhimu kwa hivyo tutaipa umuhimu kwanza tukishapata hizo gharama, tukishajua hizo gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaingia katika mkakati wa kutafuta fedha na baadaye kutangazwa zabuni kumpata mkandarasi na hatimaye hatua kwa hatua kuanza kuitekeleza kwa kuijenga. Nikupongeze sana tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Silvery Luboja kwa maswali haya mazuri ya wananchi wa pale Misungwi na Jiji la Mwanza kwa ujumla wake, ahsante. (Makofi)