Supplementary Questions from Hon. Thomas Maganga Kampala (5 total)
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kulingana na umuhimu wa chuo hiki, je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kabla sijaja Bungeni, nilitembelea mradi huo wa ujenzi, mradi huo hauridhishi. Je, Waziri yuko tayari kwenda kujionea halisi ya mradi na kutoa msukumo ili mradi ukamilike kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako ninaomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa ufuatiliaji wake juu ya maendeleo ya Chuo hiki cha Mlele, lakini pia nimpongeze nimepata taarifa kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Wabunge wapya katika Bunge hili. Kwa hiyo nimpongeze kwa nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya awali, kwamba kati ya bilioni 1.6 ambazo zilizotengwa, bilioni 1.032 tayari zimeshatumika. Kwa hiyo bakaa iliyobaki siyo kubwa sana na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kumalizia vyuo hivi na kuanza ujenzi pia wa vyuo vingine. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Maganga kwamba, fedha zitaenda na chuo hicho kitamalizika katika awamu ya pili. Ahsante
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, niko tayari kwenda na kuangalia maendeleo ya chuo hiki.
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo, mkataba unatarajiwa kukamilika Juni. Kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, mpaka sasa mradi uko 10%, je, Serikali ina kauli gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza kwa ufuatiliaji wa karibu sana wa utekelezaji wa mradi huu; na pili, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu utekelezaji huu unaenda sambasamba na kukagua huu mradi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulichelewa kwa sababu ya changamoto ya kifedha, na sasa Serikali imeshatatua changamoto hiyo. Baada ya kuwa wamepelekewa fedha, wakandarasi wameanza kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Spika, tutatendelea kufuatilia kwa ukaribu sana, na vyombo vyetu vya usimamizi viko kule vinasimamia vizuri, wataalamu wetu, watendaji wakuu, Mheshimiwa Waziri pia anaendelea kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati na wenye thamani halisi ya fedha, kwa kuhakikisha kwamba ubora wake uendane na mahitaji halisi ili wananchi wa Jimbo la Mheshimiwa Kampala wapate huduma ya maji iliyokusudiwa.
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuja na mkakati wa kuzitambua shule zote kongwe na chakavu. Swali langu; je, ni lini mpango huo utakamilika kwa sababu shule nyingi ikiwemo Shule ya Msingi Masigo zina hali mbaya sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini tayari ya idadi ya shule ambazo ni chakavu na hivi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tumeshawasilisha andiko na mapendekezo kwa Wizara ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ili tufanye tathmini na kuona uwezekano wa wa kupata vyanzo vya mapato kwa ajili ya kuanza kupata fedha hizo na kuanza ukarabati wa shule hizo 10,595 kwa awamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeshachukua hatua tunaendelea na taratibu na mara taratibu zitakapokamilika tutaanza ukarabati wa shule hizo katika maeneo mbalimbali kote nchini.
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, Wabunge wengi wanazo takwimu sahihi za watumishi na walimu wanaojitolea kwenye majimbo na halmashauri zetu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi kushirikiana na Wabunge, ili kupata takwimu sahihi za watumishi na walimu wanaojitolea kwenye majimbo yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ya watu wanaojitolea kwa sasa ofisi haijapata takwimu kamili kwa sababu, kwanza watu wamekuwa wakiingiza watumishi kwa namna ambayo, kama nilivyosema kwamba, watu wanapojitolea wakati mwingine wanaingizwa kwa upendeleo na wengine wanaingia kwa kujuana. Serikali imeendelea kupanga mkakati kuhakikisha tuna mwongozo na mfumo ambao utakwenda kufuatilia kwa karibu wale vijana ambao wamepata nafasi ya kujitolea baada ya kutumia mwongozo huu ambao tumeutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watumishi watakapoingia kupitia mwongozo huu, Serikali itapata urahisi wa kupata data kamili ya vijana wa kujitolea, lakini pia, mwongozo ule unaeleza masharti na vigezo ambavyo vitatumika, ili watu hawa waweze kujitolea. Kwa hiyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tunauchukua, ili kuendelea kupata data kamili kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Wilayani Sikonge ulisainiwa Juni, 2023 na chuo kingekamilika Disemba, 2023, lakini kutokana na changamoto mbalimbali mpaka tunavyoongea hivi sasa hicho chuo bado hakijakamilika. Je, ni nini sasa tamko la Serikali kuona kwamba chuo hiki kinaenda kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu ya jumla kwamba Serikali iliahidi kujenga vyuo hivi nchi nzima kwa zile Wilaya ambazo hazina vyuo hivi. Tayari tulishapokea shilingi bilioni 82 kama 82% ya shilingi bilioni mia moja ambazo tumepewa, lakini pia tumeshapokea asilimia ya fedha zilizobakia na nimuahidi Mbunge kwamba fedha hizi tutaenda kuzigawa hivi karibuni na vyuo vyote hivi vitakamilika. (Makofi)