Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. David Mwakiposa Kihenzile (3 total)

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa; lakini nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza; ninaomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge na Watanzania kuhusu mafanikio ya ATCL tangu Serikali ianze kuwekeza fedha.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni upi mpango wa ATCL kushika soko la kimataifa likawa kama mashirika mengine makubwa ya duniani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, sisi kama Wabunge na Watanzania tuna mengi ya kujivunia kwa ATCL. Tumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa kuamua rasmi kuliboresha shirika letu la ndege la Tanzania. Katika miaka hii mitatu au minne ambayo Mheshimiwa Rais ameamua kuwekeza tumeona mabadiliko mengi. Kwanza, idadi ya ndege imeongezeka. Mwaka 2016 tulikuwa na ndege moja, ilipofika mwaka 2021 tukawa na ndege tisa. Mheshimiwa Rais ameongeza ndege ziko 16 ikiwemo na ndege kubwa ya mizigo; na hivyo imepelekea mzigo unaosafirishwa kuongezeka kutoka tani 1,290 hadi tani 6,900, haijawahi kutokea. Hata idadi ya abiria imeongezeka mara dufu kutoka abiria 537,000 sasa wako abiria 1,100,000.

Mheshimiwa Spika, hata mtandao wa ndege umeongezeka, hapo awali tulikuwa tunakwenda vituo vichache na leo ninapozungumza Air Tanzania inakwenda vituo takriban ukanda wote wa kusini; inakwenda takriban mikoa yote Tanzania ambapo viwanja imekamilika. vilevile Inakwenda kwenye maeneo ya kimataifa kama Guangzhou, Mumbai na Dubai; hayo yote ni mafanikio. Fedha za kigeni zimeongezeka zaidi kutoka takriban fedha iliyokuwepo mwanzoni dola milioni 43 hadi 157. Kwa hiyo, tunayo kila sababu na sifa ya kujivunia maboresho makubwa ya shirika letu la Air Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, ametaka kufahamu, kwamba je, ni mipango gani ambayo shirika inayo ya kuhakikisha kwamba linakuwa competitive na kushindana na mashirika makubwa duniani. Kwanza kabisa ni kuongeza idadi ya ndege. Ukimsikiliza Mheshimiwa Rais alipokuwa anahutubia Bunge na mara kwa mara akizungumzia sekta hii ya uchukuzi, anataka kuongeza ndege. Ukisoma Dira 2050 na Ilani ya CCM kwa umoja wake ifikapo 2030 zitaongezeka zaidi ya ndege nane hadi 10 ukilinganisha na zilizopo sasa hivi. Pili, pamoja na kuongeza ndege ambazo pia tunakwenda kuongeza vituo vya kimataifa, sasa hivi tuna vituo vitatu kama nilivyosema, ATCL ina mpango wa kuongeza vituo vingine saba na kwenda juu ili iende Ulaya, Asia na maeneo mengine ya dunia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, ATCL iliyojipanga kufanya majukumu yake kibiashara inakwenda kukodi ndege. Mashirika mengi duniani pamoja na kumiliki inakodi ndege zingine ili kuweza kushika soko la kimataifa; na sisi tunatengeneza balance sheets zetu vizuri ili tuongeze ndege nyingi zaidi, twende duniani kote tuweze ku-compete kama mashirika kwa mengine yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, tulikuwa na changamoto ya wataalam, sasa hivi tunamiliki ndege 16 lakini changamoto kubwa ni marubani. Tuna upungufu wa marubani 61 pamoja na wahandisi, (professional engineers). Ni nini tunakifanya kama shirika? Kwanza ni kuhakikisha tunajenga Chuo Kikuu cha Anga pale KIA ambacho kitajengwa hapo baadaye. Pili, kuboresha chuo chetu cha NIT. Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi ili marubani wapate vifaa na utaalam wa kutosha. Kama hiyo haitoshi, tunatoa rai kwa Watanzania kupeleka vijana wetu kwenda kusoma kwenye kada ya urubani pamoja na uhandisi wa ndege kwa sababu huko hawatoshi, tunahitaji wengi waende huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi ni kuimarisha diplomasia yetu. Kama ambavyo Wabunge wanafahamu, Mabalozi wetu katika dunia hii wanafanya kazi nzuri sana na ninatumia nafasi hii kuwapongeza sana kwa sababu ndio ambao wametupatia masoko. Hivi ninavyozungumza mwezi huu tunakusudia kuongeza kituo kingine Accra, Ghana. Hii ni kazi nzuri ya wanadiplomasia wetu wanayoifanya huko duniani. Kwa hiyo, kote huko tutakwenda kufika na hii yote inafanywa na wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tunakamilisha uwanja wa Msalato. Uwanja huu ni wa kimataifa, maana yake unapoongeza viwanja vya kimataifa shirika lako la ndani linapata nguvu na uwezo wa kuongeza scope ya kutoka hapa na kwenda kwenye maeneo mengine. Kwa hiyo, mipango ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya anga hususan kuboresha shirika letu la ATCL ni mikubwa, tumwombee Rais wetu afya njema ili maono yake yaweze kutimia. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, lakini pia kuna usafirishaji mkubwa wa makaa ya mawe kutoka Nyasa na Mbinga kwenda Mtwara; lakini pia tunategemea Mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma. Katika majibu ya msingi ya Naibu Waziri amesema kwamba upembuzi yakinifu wa kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa SGR kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay umeanza kutekelezwa. Je, itachukua muda gani kukamilisha upembuzi yakinifu na mradi huo ukaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu swali hili linagusa takriban Wabunge wote wa Kusini; na pengine wangesimama kutaka kuuliza reli ya kusini itaanza kutekelezwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe maelezo kwa ufupi sana. Serikali inatambua umuhimu wa reli ya kusini, kwanza kama kiunganishi cha Bandari ya Mbamba Bay na Bandari ya Mtwara, kwa sababu hizi mbili zikiungana unarahisisha usafirishaji; na nini kimekifanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua za awali Serikali imekwishaanza kujenga Bandari ya Kisiwa Mgao pale Mtwara bandari ya pili ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya kusafirisha dirty cargo; yaani cement, makaa ya mawe na kadhalika; zaidi ya bilioni 435 zimeelekezwa pale. Pia ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay ambao utagharimu zaidi ya bilioni 70, ni hatua muhimu kuelekea kwenye jambo hilo. Tatu, fidia imelipwa kule Ludewa kwa wananchi waliopo kwenye maeneo ya Liganga na Mchuchuma, hiyo ni hatua pia. Nne sasa, tumekwishafanya usanifu. Kama nilivyosema, tunatafuta wawekezaji binafsi ambao tutashirikiana nao ili tuanze kujenga. Ninatoa rai tena kwa watu wote wa ndani na nje ya nchi ambao wapo tayari kushirikiana na Serikali, twendeni tukajenge reli hii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini ninaomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ninaomba kufahamu, huo upembuzi yakinifu unahusisha kitu gani na utakamilika lini? Kwa sababu tarehe 28 Machi, 2024, Serikali ilisaini mkataba na mkandarasi anayeitwa Taifa Civil Mining Limited, mkataba ambao ulikuwa na zaidi ya thamani ya bilioni 29.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Serikali, wananchi wa Nyamagana, nikiwemo mimi mwenyewe kama mwakilishi wao, ninapata mkanganyiko wa nini ambacho kinaendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu, ilhali Serikali tayari imekwishasaini mkataba.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; toka Serikali isaini mkataba huo, haijawahi kupeleka hata senti tano. Hivi ninavyozungumza, kwa taarifa nilizonazo, mkandarasi ameanza kuondoa vifaa vyake site. Ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili mkandarasi aweze kuendelea na kazi ya ujenzi wa uwanja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Nzilanyingi kwa ufuatiliaji wake wa karibu kwenye uwanja wetu huo wa Mwanza, lakini yeye Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla. Kiko kilio kimoja ambacho wamekuwa wakikitoa kwa muda mrefu, ni lini uwanja wa Mwanza utapewa hadhi ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia maombi hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan, amepokea kilio hicho na amefanya usanifu, ametuelekeza kama sekta chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa tumefanya tathmini ya kina na kubaini kuwa, iko haja kubwa ya kuufanya uwanja kuwa wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, sasa mambo mazuri yanahitaji pia subira, nini kinafanyika kama nilivyosema? Mambo matatu; la kwanza Jengo lilopo kwa sasa, linatosha abiria karibu 400,000 – 500,000. Tunataka tufanye usanifu ili tuweze kujenga jengo kubwa litakaloweza kubeba abiria zaidi ya milioni mbili na laki tano. Ili ndani ya jengo, tuweze kuweka taasisi zote muhimu ambazo ni sifa na takwa muhimu kwenye uwanja wa kimataifa; Uhamiaji, Afya, pamoja na Maliasili na vitu vingine vingine. Mbili, runway; ili uwanja uweze kuwa wa kimataifa, ule upana wake hautoshi. Tunaongeza kutoka meta 45 mpaka meta 60 na ku-maintain urefu uliopo wa takribani meta 3,800.

Mheshimiwa Spika, la tatu, ni taa. Ule uwanja uliopo awali tulifikiri pengine zile taa zingetosha, lakini baada ya tathmini ya kina, inaonekana kabisa kwamba zile taa hazitatosha kwa sababu zilijengwa miaka ya 1970. Hivyo basi, tunataka tubadilishe taa zilizopo na kuweka za kisasa. Kwa sababu hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wote waweze kuwa na subira.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameuliza kwamba Serikali haikupeleka fedha ni kweli na jengo lililopo linafanya nini? Jengo lililopo sasa ambalo tulikuwa tumeshaanza ujenzi ambao tunashirikisha sekta binafsi tutalitumia kwa ajili ya general aviation. ndege ndogo, wale watu wa premium, ukiwa na ndege yako, utatumia jengo hilo. Lengo ni jema tu, kuhakikisha kwamba tunaupa hadhi ya kimataifa na inayostahili uwanja huo ambao unasafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nchini kwetu minofu ya samaki, maliasili pamoja na utalii, kwa maana ya utalii kwa ujumla na kadhalika. (Makofi)