Supplementary Questions from Hon. Dr. Regina Christopher Malima (6 total)
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
kwanza kabisa nishukuru kwa majibu mazuri ya Wizara, na
niipongeze Serikali kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa sana
umefanyika katika sekta ya elimu. Kuna mikakati mingi imefanyika
na Serikali ya Awamu ya Sita, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na miradi
hii ya kimkakati kutoa ajira kwa vijana, je, Serikali ina mpango wa
kuweka Sera au miongozo itakayolazimisha miradi yote ya uwekezaji kutenga asilimia maalumu ya ajira za kitaalamu kwa
wahitimu hawa wa vyuo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO): Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakubaliana na mwuliza swali 100% kuwa miradi ya kimkakati
imeonesha uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira. Hata hivyo, Sera za
Ajira zinaelekeza ajira zitolewe kwa ushindani bila kutoa
upendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira, na Mahusiano inaendelea kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Na.1) ya
Mwaka 2015, ambapo pamoja na mambo mengine inaelekeza
wafanyakazi wa kigeni yaani wataalamu kurithisha ujuzi kwa
wazawa katika ajira za kitaalamu ili pale kibali cha kazi cha
wageni kitakapokwisha, mzawa aweze kuchukua nafasi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali itaendelea kutoa
kipaumbele kwa wafanyakazi wazawa katika miradi ya kimkakati
kwa nafasi za kazi ambazo utaalamu wake siyo adimu katika soko
la ndani ya ajira. (Makofi)
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nina swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na Bandari ya Nansio katika Kisiwa cha Ukerewe. Bandari hii pia, imechakaa, imechoka, haijawahi kufanyiwa ukarabati tangu uhuru. Wakati mwingine hali ya hewa ikiwa ni mbaya meli pia zinapata shida kuweza kupaki. Kwa hiyo, ninaomba kujua, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Bandari hii ya Nansio katika Kisiwa cha Ukerewe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka anapoingia madarakani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2021, takribani bandari 80 zilikuwa zinatambuliwa na kurasimishwa. Kutokana na umuhimnu wa sekta ya bandari, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo maalumu na mahususi kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wizara ya Uchukuzi kwanza, tufanye urasimishaji. Tumekamilisha urasimishaji na bandari zimeongezeka mpaka 142.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni kuanza kutafuta fedha, kuboresha bandari moja baada ya nyingine. Namwomba Mheshimiwa Malima awe na Subira, Bandari ya Nansio ni moja kati ya bandari muhimu kwenye Taifa letu. Tutakwenda kuifikia pindi fedha zitakapokuwa zimepatikana.
MHE. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaunganisha wahitimu wa vyuo vikuu na fursa za mikopo hii ya 10%, ili na wao waweze kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mbunge ni swali muhimu sana, lakini Serikali ilishaanza kutekeleza. Ninakumbuka miaka miwili iliyopita nilifanya ziara katika Halmashauri ya Nyamagana ambapo vijana wahitimu walijiunga pamoja, wakaanzisha kituo cha afya na wakapewa mkopo wa 10% na wakaendelea kuendesha kituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Dar es Salaam imefanya hivyo, wapo walimu ambao wamekopa, wamefungua tuition center na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa hiyo, Serikali inawapatia fursa kupitia dirisha la mikopo ya 10% kwa vijana kupitia Halmashauri zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwahamasisha vijana wahitimu kote nchini kwamba waunde vikundi vyao, waende kuomba mikopo kwenye Halmashauri kulingana na taaluma zao, waanzishe shughuli zao kwa sababu dirisha lipo wazi kwa ajili yao, na lina faida kubwa kwa sababu wao wenyewe wanapata ajira, na pia wanaajiri vijana wengine katika maeneo hayo.
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini swali langu dogo ni kwamba, wakati Serikali ikijipanga kuwa na mipango endelevu kwa ajili ya kuwasaidia wahitimu hawa wanaojitolea katika kufundisha vyuo vyetu, je, mna mpango gani wa haraka wa kuhakikisha mnawalipa posho na motisha wakati wakifanya kazi hii kwa uaminifu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Regina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali kwa kuona kwamba inawezekana kuna watu wanajitolea katika taasisi nyingi, lakini katika shule zetu, katika vituo vya afya na wakati mwingine malipo au posho zile zinasuasua, Serikali imeleta mwongozo ambao unaeleza kiwango ambacho anatakiwa kulipwa na ndiyo maana katika mwongozo ule ambao umetolewa wa mwaka 2025 utaeleza utaratibu namna ya kuwapata wale vijana ambao wanakwenda kujitolea. Mwongozo unaeleza stahiki za yule mtumishi ambaye anakwenda kujitolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutoe hofu kwamba utekelezaji wa mwongozo huu utatupeleka kwamba watumishi wote wanaojitolea watapata haki zao za msingi kila ambapo wanajitolea katika taasisi zetu lakini na katika maeneo yetu, ahsante.
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi. Ni jambo la kushangaza kuwa wananchi wa Kisiwa cha Ukerewe kinachozungukwa na Ziwa Victoria hawana majisafi na salama, ikiwemo Kijiji cha Busagami Kata ya Namilembe. Nini kauli ya Serikali juu ya hali hii, na ni hatua gani za haraka zitachukuliwa kuhakikisha wananchi wa kisiwa hiki wanapata huduma ya majisafi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu kwamba kiu ya Mheshimiwa Mbunge ni kuhakikisha wananchi wake wa Ukerewe wanapata huduma ya majisafi na salama kwa 100%, lakini mpaka sasa upatikanaji wa maji ndani ya Kisiwa cha Ukerewe ni zaidi ya 65%.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaamini kwamba kiu yake ni kwamba tuongeze ili wananchi wengi zaidi wakiwemo katika Kijiji ambacho Mheshimiwa amekitaja, nikuhakikishie Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza, tayari wanafanya tathmini ya kujua ukubwa wa tatizo ili waweze kufanya usanifu na tuweze ku-establish gharama za kwenda kutekeleza miradi ambayo itatatua changamoto ya maji katika Jimbo la Ukerewe. Ninakushukuru sana.
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kwa niaba ya vyuo na vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti kuna changamoto ya baadhi ya vyuo vilivyoko kando kando ya Ziwa Victoria, lakini pia shule za sekondari especially kwenye Majimbo ya Mwibara na hata Jimbo la Ukerewe.
Je, Serikali iko tayari kufanya uhakiki wa shule hizo na zenyewe kuingia katika mpango wa huu Mradi wa Ziwa Victoria? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Regina kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la msingi sana ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliongelea na kwa sababu Watanzania wote kwa mujibu wa Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 Toleo la mwaka 2025 ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya maji safi na salama hususan katika maeneo haya ya chuo, tutakaa na wenzetu Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu lakini pia Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, kwa upande wa shule za sekondari na msingi ili tuweke mkakati wa pamoja namna ya kwenda kushughulika na changamoto zilizoko katika vyuo, sekondari pamoja na shule za msingi. Lengo ni kutimiza azma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anakuwa na access ya maji safi na salama. Nakushukuru sana.