MHE. CLAYTON R. CHIPANDO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia wakandarasi wanaochelewesha miradi kama Mradi wa Delta ya Mto Luiche unaoendelea kwa kasi ndogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya kutokukamilika kwa wakati kwa baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa umwagiliaji wa Delta ya Mto Luiche. Mradi wa Luiche wenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 65.16 unajumuisha ujenzi wa bwawa na miundombinu ya mashambani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, mwaka 2025 ilifanya mapitio ya usanifu wa mradi husika ili kuendana na mahitaji ya sasa na hivyo kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi hadi mwaka 2027. Baada ya mapitio hayo, mradi umeanza utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi wa Delta ya Mto Luiche kutanufaisha eneo la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 3,000 na kunufaisha wakulima zaidi ya 9,620 katika Vijiji vya Kagera, Matiazo, Mungonya, Kamala, Kasuku na Simbo.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mtandao wa Barabara za lami Kigoma Mjini kwa kuongeza bajeti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Clayton Revocatus Chipando, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji hadi mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa inapokea Bajeti ya Matengenezo ya barabara na madaraja jumla ya shilingi bilioni 1.6 kwa mwaka. Kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka 2025/2026, bajeti iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 3.2 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa TACTIC Awamu ya Kwanza inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Barabara za kilometa 9.4, Mitaro Mikubwa ya Maji ya Mvua kilometa 5.4, Soko kuu la Mwanga pamoja na Soko la Samaki la Katonga katika Manispaa ya Kigoma Ujiji. Utekelezaji wa mradi huu utaongeza mtandao wa Barabara za lami Kigoma Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuujengea uwezo wa kibajeti wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini ili uweze kutekeleza Ujenzi wa Barabara za tabaka la lami kwa awamu kote nchini ikiwemo katika Manispaa ya Kigoma.