MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA K.n.y. MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza Miradi ya TACTIC iliyopangwa kutekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali na Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ni miongoni mwa halmashauri za miji 45 zinazotekeleza miradi ya TACTIC nchini. Halmashauri ya Mji wa Ifakara ipo kundi la tatu la utekelezaji lenye jumla ya miji 18 ambayo imetengewa kiasi cha shilingi billioni 13.25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa TACTIC umekamilisha usanifu wa miradi ya kundi hili la tatu ikiwemo Mji wa Ifakara wenye Barabara za NBC - Mangwale - Msikitini (km 1.29), Simba Oil - Mark Guest (mita 520), Uhuru Roads (km 1.08), Kilosa - Kalifornia (mita 70), Kituo cha Afya - SACCOS (mita 570), Junction - Katrini - Mlenge (mita 370), Vibaoni - Hospitali (mita 330), Stendi - Sokoni (mita 420).
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi zina urefu wa jumla ya km 4.65. Aidha, utekelezaji wa mradi huu utajumuisha mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi katika Kata ya Kibaoni na Soko Kuu katika Kata ya Ifakara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha usanifu wa miradi hii ya kundi la tatu, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inaendelea na taratibu za maandalizi ya kuanza utekelezaji wa miradi katika kundi hili ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Ifakara.