Primary Questions from Hon. Edibily Kinyoma Kazala (4 total)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia Wananchi wa Kitongoji cha Katoto waliopisha Mradi wa Kitalu cha Makere Forest Reserve?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya wananchi wa Kitongoji cha Katoto kuhama yalitolewa mwezi Oktoba, mwaka 2022 na Kamati ya Mawaziri Nane wa kisekta baada ya kubaini kuwa wananchi hao walikuwa nje ya mipaka ya Kijiji Mama cha Kagera. Serikali ilifanya tathmini ya kaya na makazi na kugawa eneo la ukubwa wa Hekta 4,446 katika Kitongoji cha Nyantuku, Kijiji cha Kagerankanda ambapo kila kaya ilipewa eneo la kujenga la ukubwa wa mita 32 kwa 64 na hekari tatu kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali kupitia Kamati ya kisekta ya Mawaziri Nane, wananchi wa Katoto waliohamishwa walishapatiwa fidia ambayo ni ardhi kwa ajili ya makazi, kilimo na mifugo ikiwa ni pamoja na Serikali kuwapatia usafiri wa mali zao kipindi walichokuwa wanahama. Hadi kufikia mwezi Oktoba, 2025 uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kasulu ulifanikiwa kuhamisha wananchi wote kutoka Kitongoji cha Katoto na kwenda Kitongoji cha Nyantuku, Kijiji cha Kagerankanda.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza: -
Je, ni kwa kiasi gani wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini wananufaika na uwepo wa mwekezaji wa Kitalu cha Makere Forest Reserve?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini wameendelea kunufaika na uwepo wa mwekezaji katika Kitalu cha Makere Forest Reserve kwa kupata mgao wa fedha za maendeleo ya jamii kiasi kisichopungua shilingi milioni 12 kila mwaka kinacholipwa na mwekezaji na kugawanywa kwa vijiji ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya vijiji husika. Mathalani, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Vijiji vya Kagera Nkanda, Chekenya na Kabulanzwili vililipwa shilingi 4,356,435.67 kila kimoja kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii. Vilevile, mgao wa fedha zinazotokana na 25% ya ada ya wanyamapori wanaowindwa katika kitalu husika kwa mujibu wa kifungu cha 137 cha Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 zinalipwa na Serikali kwa halmashauri husika. Asilimia 60 ya fedha hizo hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo na 40% shughuli za uhifadhi katika vijiji vinavyozunguka kitalu husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na manufaa yaliyotajwa, katika kipindi cha mwaka 2024/2025 na 2025/2026 mwekezaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania wamechangia miradi ya jamii yenye thamani ya shilingi 166,475,000. Fedha hizo zimetumika kufadhili kambi ya huduma ya matibabu ya macho katika Halmashauri ya Kasulu, madawati 100 ambapo katika Shule ya Msingi Chekenya wamepata madawati 25, Shule ya Msingi Nyakasanda walipata madawati 25 na Shule ya Msingi Nyantuku ambao wamepata madawati 50. Vilevile na uchimbaji wa visima vya maji sita katika Shule za Msingi Kamganza, Kasasa, Mwitiri, Chekenya na Nyantuki pamoja na Kituo cha Afya cha Kagerankanda. (Makofi)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Uvinza – Kasulu na Makere – Nyarugusu Kitanga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edibily Kazala Kinyoma, Mbunge wa Kasulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Uvinza hadi Kasulu na Barabara ya Makere – Nyarugusu hadi Kitanga ni barabara za mkoa zinazohudumiwa na TANROADS Mkoa wa Kigoma. Kwa sehemu ya Uvinza hadi Kasulu yenye urefu wa kilometa 56.8, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika, na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, kwa sehemu ya Makere – Nyarugusu hadi Kitanga, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante
MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza changamoto ya Mawasiliano kwa kujenga Minara Kata za Heru Ushingo, Kagerankanda na Asante Nyerere - Kasulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Edibily Kazala Kinyoma, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote – UCSAF ilikamilisha ujenzi wa Mnara Mwaka 2014 kupitia Kampuni ya Honora au (Yas Tanzania) kwa ajili ya kuhudumia Vijiji vya Seruhemebe na Heru vilivyopo katika Kata ya Heru Ushingo. Aidha, katika Kata za Kagerankanda, UCSAF ilijenga Mnara mwaka 2021 katika Kijiji cha Mvinza kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika Kata ya Asante Nyerere, UCSAF ilikamilisha ujenzi wa mnara mwaka 2025 kupitia Kampuni ya Vodacom Tanzania katika Kijiji cha Sogeeni Kwiliba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada nilizozitaja awali, Serikali kupitia UCSAF itatuma wataalamu kwenda Kasulu Vijijini katika Kata husika kufanya tathmini ili kujua mahitaji halisi na hatimaye kuviingiza vijiji vyote vyenye changamoto ya mawasiliano katika miradi itakayotekelezwa na UCSAF hususan katika Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Minara wa Mwaka 2025 – 2030.