Supplementary Questions from Hon. Edibily Kinyoma Kazala (4 total)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, bado nina swali moja la nyongeza la kuiomba Serikali kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari tuambatane naye kuelekea jimboni akaone na kujidhirisha namna zoezi lilivyotekelezwa na kusaidia kutatua migogoro inayoambatana na kitalu hiki cha Makere Forest Reserve Uvinza Open Area.
Mheshimiwa Spika, kitalu ambacho kinasabaisha mgogoro wa wananchi; wananchi kufyekewa mazao, kupigwa na kuna mgogoro wa kimapato na halmashauri kwa mfano kwa DCC ripoti tuliopata wanapata kama 1,900,000 tu. Pia kuna mgogoro wa Kacheri na Luguvu Relini ambao nao wameambiwa kuhamishwa, kuna mgogoro wa wananchi wenyeji nao wamechukuliwa maeneo yao na wakati walikuwepo pale tangu miaka ya 70.
Mheshimiwa Spika, pia kuna mgogoro wa TFS na wananchi wa kimpaka, wananchi wamewekewa beacon mpaka katikati ya vijiji. Ninaomba ikiwezekana Mheshimiwa Waziri aambatane nami twende jimboni kupunguza changamoto zinazokabili jimbo langu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi niko tayari hata tukimaliza Bunge twende kwa wananchi wetu kuweka tabasamu kuondoa migogoro ambayo inawakabili. (Makofi)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kuna baadhi ya majibu hapo naona kama si sahihi ikiwemo shilingi milioni 166 ambazo ziligaiwa kwenye halmashauri kwenye huduma ya macho, DMO amekataa kwamba hizo fedha hazijawahi kufika. Pia hivyo visima sita vinavyotajwa hapo, kati ya hivyo visima sita vipo viwili tu na kimoja ndicho kinachofanya kazi vizuri, lakini pia baadhi ya hizo shilingi milioni nne zinazotajwa hapo nazo zinaonekana baadhi ya vijiji bado wanakiri kutokupokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu…
MWENYEKITI: Maswali Mheshimiwa.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niulize; mwekezaji huyu amekuwa akiwa na changamoto nyingi kwa jimbo langu la Kasulu Vijijini ikiwemo kufyeka zaidi ya hekari 200, kuzuia wananchi kuvua kwenye Mto Malagarasi na kuzuia wananchi kuweka mizinga kwenye miti.
Je, Serikali haioni haja ya kuleta mwekezaji mwingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa mwekezaji amekuwa akigombana sana na wananchi wa Jimbo langu la Kasulu Vijijini; je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kukikata kipande kile ambacho kipo mwekezaji anapopakana na wananchi kimilikiwe na halmashauri ili iongezee mapato na kuepusha migogoro ya Serikali na wananchi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mbunge, ameomba kupelekewa mwekezaji mwingine kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la kitalu cha Makere Uvinza Open Area lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambako Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya Baraza la Madiwani. Sisi kama Wizara tulipokea ombi kutoka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuhusu kutenga eneo hili kwa ajili ya eneo la uhifadhi na utalii. Hivyo, mamlaka haya yapo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Kama watakaa chini na wakaamua tena kama Baraza la Madiwani sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii hatuna kipingamizi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la kumega eneo na kuwa sehemu ya halmashauri, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya swali lake la nyongeza la kwanza, eneo hili lipo chini ya miliki ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na wao ndio waliotuomba sisi kama Wizara tuweze kutoa miongozo ya jinsi ya kuendesha eneo hili kwa ajili ya uhifadhi na utalii. Hivyo kwa kuwa eneo hili lipo chini ya miliki ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ninaomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge arejee kwenye Baraza la Madiwani na waweze kuketi kuona jambo gani wanaweza kufanya kwa maslahi mapana ya halmashauri yake ya Kasulu. (Makofi)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kumekuwa na wimbi la vijana kufanya interview nyingi na kwenye aptitude test wanapata asilimia za juu mpaka 90%, lakini wanakuwa hawapo selected. Je, Serikali haioni ipo haja ya kuweka cutting point, ili kuepuka vijana kufanya interview 10 hadi 20 na hawapati kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wanapokwenda kwenye mitihani ile ya awali, yaani aptitude test, kwanza tunapata waombaji wengi sana ambao ajira ikitangazwa wanajitokeza kuomba ajira hizi. Kwa hiyo, wanapokwenda kwenye usaili wanafanya mtihani wa written, kwenye ule mtihani wa written kunakuwa na alama ambazo zinamfanya yule msailiwa aweze kufikia zile alama na waliofikia zile alama wanachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, wengi wanafaulu na kwa kuwa kiwango ambacho labda Serikali imepanga kwa muda huo ni watu 10,000 na wanaohitajika labda ni watu 5,000 kwa hiyo, cutting point ya alama zile zinazotakiwa lazima itapanda kulingana na wingi wa watu kufaulu kwenda kwenye mtihani wa written. Hii ni kwa sababu, tunazingatia Sheria ya ILO ambayo inatuelekeza kwamba, nafasi moja itashindaniwa na watu watatu.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini pia Mheshimiwa Naibu Waziri amekuwa Mkurugenzi kwenye Halmashauri yetu anafahamu umuhimu wa hizi barabara. Je, Serikali haioni haja ya kutenga fedha kwenye hii bajeti kuhakikisha barabara hizi zinajengwa kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali la pili, barabara hizi zimepita karibu na SGR, mahali ambapo SGR inajengwa kuelekea Burundi. Je, Serikali haioni iko haja ya kuzijenga barabara hizi kwa haraka ili wananchi waweze kunufaika na fursa za SGR kabla SGR haijamalizika kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze na Barabara ya Uvinza - Kasulu. Barabara ya Uvinza - Kasulu nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, kimsingi ndiyo tunayoita T Number Nine ambayo inatoka Tunduma – Mpanda – Uvinza - Kasulu hadi Nyakanazi. Nakubaliana naye kwamba ni kipande hicho tu ambacho kwa sasa kinatafutiwa fedha ili kiweze kujengwa na tukamilishe barabara yote Nyakanazi – Kasulu - Mpanda, Sumbawanga hadi Tunduma. Kwa hiyo, nakubaliana na wewe na Serikali inalijua hilo. Kwa hiyo, tunafanya kila jitihada tutafute fedha kuanza kuijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Barabara ya Makere - Nyarugusu kwenda Kitanga, Mheshimiwa Mbunge anakubaliana nami kuwa hiyo barabara ilikuwa inahudumiwa na wenzetu wa TARURA, ndiyo imepandisha hadhi na nadhani ndiyo kwanza tunataka tuitengeneze iwe katika mfumo wa TANROADS, wakati tunaendelea kutafuta fedha ya kuisanifu ili kwa kweli iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, kwa sababu inaenda sambamba pia na SGR, pia inaenda mpakani, nchi ya Burundi. Kwa hiyo, tunalifahamu hilo, ndiyo maana tumeipandisha na tunaitafutia fedha kuisanifu ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante