Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Moshi Selemani Kakoso (10 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema, Kituo cha Afya cha Kasekese na Kituo cha Afya cha Mwese kuna tatizo kubwa la ukosefu wa Jengo la Mama na Mtoto, Maabara na nyumba za watumishi. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha,ili iweze kukamilisha hivyo vituo vya afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kwamba, zaidi ya vituo 532 vimeishatengewa bajeti ya shilingi bilioni 102.08. Kwa hiyo, pamoja na vituo ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha vimo katika ukarabati huu mkubwa na kuweza kujenga majengo mengine ambayo yanahitaji, kama maabara, ili kuendelea kupata huduma kwa wananchi wetu.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua zilizonyesha zimeharibu barabara nyingi kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika, ikiwemo Barabara ya kutoka Kapanga – Bujombe – Kalia, je, ni lini Serikali itakwenda kufanya ukarabati kwa barabara nyingi zilizoharibika kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika jimbo la Tanganyika, kama ambavyo ipo katika majimbo takribani yote kote nchini, kumekuwa na uharibifu mkubwa wa barabara zetu za TARURA. Serikali imeshafanya tathmini ya mahitaji ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linafanyika sasa, kwanza maeneo mengi bado mvua zinaendelea kunyesha kwa hivyo, siyo rahisi kufanya matengenezo ya uhakika katika kipindi hiki cha mvua. Tunasubiri kwanza hali ya hewa ikae vizuri, mvua zipungue, na baada ya hapo, taratibu za fedha zinaendelea kufanyika ili tuendelee kujenga barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso kwamba suala hilo liko kwenye pipeline na tutakwenda kuhakikisha kwamba tunajenga barabara hizo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa wilaya ambazo hazina kituo cha Polisi na halmashauri ya wilaya ilianzisha ujenzi, na mimi kama Mbunge, nimechangia kwenye hicho kituo; na Serikali iliahidi kutoa shilingi milioni 20, lakini mpaka sasa ni mwaka wa tatu. Ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tanganyika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Selemani kwa swali lake la msingi na ninawapongeza sana kwa kuchangia fedha kwenye ujenzi wa vituo vya Polisi ambao ni uhitaji mkubwa kwa usalama wa raia na mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Selemani, nimjibu tu kwamba vituo ambavyo havijamalizika nilitoa maelezo ya jumla hapa kwenye maboma 77 na nimeeleza kwamba tutaendelea kusaidia ili kukamilisha vituo hivyo kikiwemo kituo chake Mheshimiwa Selemani na tumhakikishie tu kwamba tutajitahidi mwaka wa fedha 2026/2027 tuweze kumsaidia na kukamilisha hiyo fedha ambayo tumeahidi kutoa ili tuweze kukamilisha kituo hicho. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa kuleta maji kutoa Ziwa Tanganyika kuyaleta Mpanda Mjini. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo ili wananchi waweze kunufaika?

SPIKA: Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kama sijamsikia vizuri kwenye hilo.

SPIKA: Unaweza ukarudia tena Mheshimiwa Kakoso swali lako?

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuleta maji kutoka Ziwa Tanganyika kuyaleta Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi Mpanda Mjini. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, katika mpango mahususi wa ujenzi wa gridi ya Taifa ya maji, moja ya maziwa na vyanzo vya uhakika ni pamoja na Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, pamoja na mito mingine mikubwa mikubwa kama Malagarasi, Momba, Pangani na mingineyo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba maji tunayatumia kwa kuyapeleka katika makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari imeshampata mtaalamu mshauri kwa ajili ya kuanza kufanya feasibility study ya kuyatumia maji ya kutoka Ziwa Tangayika ili yaende Kigoma, Mpanda, mpaka Rukwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaunganishwa na huduma ya maji yenye vyanzo vya uhakika, likiwemo Ziwa Tanganyika. Nakushukuru sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Kijiji cha Kamsanga ni kijiji ambacho kimejenga zahanati kwa kutumia nguvu za wananchi, zahanati nzuri na ya kisasa na ina zaidi ya watu 25,000. Ni lini zahanati hii mnaipandisha hadhi ili kiwe kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yana zahanati, lakini idadi kubwa ya wananchi zaidi ya 15,000 sera yetu ya afya inaelekeza kuwa na vituo vya afya. Kwa hiyo, eneo hilo la Zahanati ya Kamsanga ambayo ina idadi ya wananchi zaidi ya 25,000 ina sifa ya kuwa na kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wetu ni kwamba halmashauri wanaainisha kama eneo hilo lina ukubwa unaotosheleza kujenga kituo cha afya, lakini pili wanapeleka maombi yao Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ili tathmini ifanyike na iweze kuingizwa kwenye mpango kwa ajili ya ujenzi.

Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Kakoso, sisi tutawasiliana na Halmashauri ya Tanganyika ili tuweze kuweka utaratibu wa kupata taarifa kwa ajili ya kufanya tathmini na kuweka kwenye mipango yetu kwa ajili ya kupandisha hadhi zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa juhudi zilizofanywa na Serikali zimeonekana na tunashukuru kwa kazi kubwa ambayo imefanyika, lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa tatizo la vyumba vya madarasa, sambamba na ukosefu wa nyumba za walimu. Nini tamko la Serikali kumaliza tatizo hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ina shule ambazo zina tatizo kubwa na upungufu mkubwa wa madawati na vyumba vya madarasa kwenye Kata ya Kapalamsenga na Kata ya Kamsanga. Ni lini Serikali itapeleka fedha hizo kwa ajili ya kutatua kero ya uhaba wa vyumba vya madarasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Mbunge Kakoso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha na imeendelea kuainisha mipango thabiti kwa ajili ya ujenzi wa madarasa pamoja na nyumba za watumishi. Katika Bunge lako Tukufu nilikwishaeleza mpango mahsusi ambao tulienda nao pale Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuhakikisha kwamba sasa tunaenda kuanza kwa awamu ujenzi wa nyumba za watumishi 2,000 ambazo tutashirikisha sekta binafsi ili kuhakikisha kwamba nyumba hizi tunazikamilisha kwa wakati na watumishi wetu wapate nyumba hizi, ili waweze kufundisha watoto wetu kwa utulivu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya madawati na kujenga madarasa, na mpango uliopo, madarasa ya sasa yakijengwa lazima yawe na madawati angalau 45 ili kuhakikisha kwamba watoto wetu wanaanza kupata huduma.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kufanya juhudi hizi ili kuona kwamba tunajenga madarasa ambayo yanakuwa na madawati ili watoto wetu wapate mahali salama pa kujifunzia. Naomba kuwasilisha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kata ya Ikola na Kata Isengule hazina mawasiliano kwa sababu ya kuvunjika madaraja; na Kata ya Sibwesa inayounganisha Kata ya Katuma ina hali kama hiyo. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuzifanya hizo kata ziweze kuwa na mawasiliano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zote ambazo zimeathiriwa na mafuriko na kukatika kwa maana ya madaraja, ma-culvert na barabara zenyewe, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tumeshatoa maelekezo kwa Mameneja wa TARURA mikoa yote na Mameneja wa TARURA wilaya zote kwamba kwanza wanatakiwa kufika kwenye maeneo hayo mapema kufanya tathmini na kuona yale ambayo yanaweza kutengenezwa yatengenezwe kwa haraka katika hali ya dharura ili yaweze kupitika wakati tunasubiri matengenezo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso kwamba tutalifanyia kazi suala la madaraja hayo. Ninafahamu Tanganyika bado mvua zinaendelea kunyesha, kwa hiyo, yapo matengenezo ambayo yanawezekana na yapo ambayo yatasubiri mvua zikae sawa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Barabara ya Kapanga - Bujombe - Kalia inayounganisha na Wilaya ya Uvinza Mkoa Kigoma, ina hali mbaya baada ya mvua kunyesha na Serikali iliahidi kutoa fedha za kuiunganisha hiyo barabara kwa shilingi bilioni 1.5. Ni lini Serikali itatoa fedha hizo ili iweze kujenga hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara ambazo zimeathiriwa sana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha kote nchini, ikiwepo barabara ambayo Mheshimiwa Kakoso ameisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumetoa taarifa kadhaa kwa Wabunge, tayari Serikali katika kipindi cha miezi hii miwili iliyopita imepeleka katika Majimbo yetu zaidi ya shilingi bilioni 21.4 kwa ajili ya kufanya shughuli za dharura za kutengeneza barabara ili ziweze kupitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunaendelea na tathmini za mwisho kwa sababu bado kuna maeneo mvua zinaendelea kunyesha. Kwa hiyo, tunafanya tathmini za mwisho za gharama za fedha zinazohitajika kwa ajili ya kwenda kufanya marekebisho na matengenezo ya barabara hizo, na mpaka wiki mbili zilizopita tulikuwa tuna takribani shilingi bilioni 98 zinahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso, mara baada ya kukamilisha tathmini hiyo, tutaanza kupeleka fedha za dharura kwa ajili ya kurekebisha barabara hizo na tutahakikisha pia barabara hiyo inapelekewa hiyo shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya matengenezo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Tarafa ya Mwese na Kituo cha Afya cha Mwese, Katuma hakina gari ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itapeleka gari kwenye tarafa hiyo ili kuokoa wananchi ambao wanapata shida na adha kwenye vituo hivyo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kupeleka magari kwenye halmashauri zetu hasa zile ambazo zina upungufu mkubwa wa magari na awamu hii inayofuatia tutaendelea kupeleka magari hasa kwenye zile halmashauri ambazo hazikupata kwa awamu iliyopita ili kuona namna gani zinaendelea kutoa huduma kwa mama zetu hasa wale wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kutoa taarifa na tunaendelea kuwapa wakurugenzi wetu lakini pia ma-DMO kuendelea kutumia ile huduma ya M-Mama ambayo Serikali inashirikiana na Vodacom kuhakikisha kwamba unaweza ukapata gari binafsi na likaenda likabeba ugonjwa wetu hasa kutoka ngazi ya afya ya msingi au katika kaya na kuwapeleka katika vituo vyetu vya afya na halmashauri zimekuwa zikilipa magari hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba tutaendelea kuangalia upungufu hasa katika maeneo ya halmashauri ambazo zina upungufu wa magari na kuziongezea magari hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi yamelifanya Ziwa Tanganyika kuwa na mwelekeo tofauti uliosababisha wananchi wa Kata ya Ikola, Isengule, na Karema kukosa makazi baada ya ziwa hilo kuvamia makazi ya wananchi. Je, ni lini Serikali itaenda kujenga tuta kwenye maeneo ya kata hizo tatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, Serikali kupitia Mradi huu wa Mabadiliko ya Tabianchi tunatekeleza mradi huu kwa awamu kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itakapopata fedha, wananchi hao tutakwenda kuwahudumia kwa kujenga kuta kwenye eneo hilo kama ambavyo tumefanya kule Mikindani na kule Sepwese Pemba.