Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Madini, Wizara ambayo ni muhimu kabisa katika utekelezaji wa Dira yetu ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 – 2050 kwa sababu, inabeba uchumi wa Taifa letu na inaajiri Watanzania wengi ambao wako katika sekta hii. Tunajua tumeweka 70% ya Private Sector kuhakikisha kwamba, tunafikia Dira yetu ya 2050.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote, kwa kuhakikisha kwamba, wamewekeza na kuhakikisha wanawavutia wawekezaji. Tumeona hata katika hotuba yake ameainisha kabisa kwamba, tumeweza kuchangia 11.9% kwenye pato la Taifa kupitia madini haya. Ni kwa sababu, wameongeza uwekezaji na mapato ya Serikali yameweza ku-double mpaka about a trillion na mauzo nje yamefikia almost 14 trillion kwa mwaka, lakini pia, kwenye export earning wametuainishia kwamba, ni 52.7%.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo ukienda kwenye Ibara ya 46 umeainisha hapa kwamba, alitoa vibali takribani 8,635 vya kusafirisha madini ghafi kwenda nje, dhahabu, almasi, ameainisha madini ya bati, madini ya shaba, pamoja na makaa ya mawe. Hili ongezeko ambalo tunaliona ni kwa sababu ya madini ghafi. Sasa, umefika wakati pamoja na mikakati yote ambayo Waziri ameiweka, aone kuna umuhimu wa kuongeza thamani kwenye madini, tuweze ku-process hapa nchini ambapo tutatoa ajira za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ongezeko ambalo tunaliona ni kwa sababu ya madini ghafi, sasa imefika wakati pamoja na mikakati yote ambayo Waziri ameiweka haoni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza thamani kwenye madini, tuweze ku-process hapa nchini ambapo tutatoa ajira za kutosha. Katika tafiti ambayo nimepitia kama tungeweza kuchakata hapa nchini na kuongeza thamani kwenye haya madini tu ambayo amesafirisha, hivi vibali alivyovitoa, tungeweza kutoka kwenye trilioni 14 ambazo tumepeleka kama mauzo nje ika-range kati ya trilioni 18 mpaka trilioni 30. Kwa hiyo, tuone kwamba ni wajibu sasa hivi tuweze kufanya hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitia ukiangalia alivyoeleza kwenye Ibara yake ni dhahiri kabisa kwamba critical minerals na strategic minerals hazijaweza kuhusika kuhakikisha zinachangia kwenye mapato ya Taifa letu. Tanzania ni takribani katika nchi 10 tajiri zenye madini haya, ambayo madini haya tukiyatumia kimkakati yatatusaidia sana kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna hiyo strategic gap, kwa kuhakikisha kwamba tunawekeza zaidi, hapo umeainisha tu kwamba umetoa leseni 454 za madini haya lakini hizi leseni sasa kwa sababu tunaanza, tunatakiwa tuwe na mpango mkakati. Ninampongeza kwenye ile mining vision yake ya 2030, tuwe na mpango mkakati wa kuweka road map hata ya ten years. Sasa hivi katika nishati safi nchi nyingi by 2040 zinaondokana kabisa na magari ya petroli, zinawekeza kwenye magari ya umeme and the like.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia huu mpango, haya madini Tanzania ya graphite, nickel, cobalt na hizi rare earth elements tunazo nyingi sana Tanzania, ambazo ni madini, they call geopolitical minerals, ni madini ya kimkakati, tukiyatumia tunaweza kuwa na usalama wa uchumi wetu, tukawa na nguvu ya kishawishi kimataifa, lakini pia yakasaidia kuhakikisha tuna-win masoko pale ambapo tutayageuza kuweza kuchakata nchini, tuite wawekezaji wa ndani na wa nje, waweze kuchakata nchini na kubadilisha kuwa bidhaa katika teknolojia ya kisasa ambapo yanatengeneza simu, computer, runinga, magnetic hizi na mambo mengine, pia mpaka umeme wa upepo na magari kama nilivyosema. Kwa hiyo, tuziangalie sana kuhakikisha kwamba tunawekeza katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine kuhakikisha kwa kweli tunapovutia wawekezaji wanakuja, kama hizo leseni 454 umezitoa lazima tuweke masharti ambatanizi. Unavyompa leseni ahakikishe kwamba anakuja pia kuhakikisha kwamba anakuwa na kiwanda au anakuwa na chain kuhakikisha kwamba anachakata na kutengeneza hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, nilikuwa najaribu kulinganisha hii rare mineral elements na nchi nyingine za kimataifa kwa mfano China, wenyewe wanazalisha almost 70% ya hii rare earth elements, wanazalisha lakini wanachakata 85% ya hizi rare zote za dunia. That means, karibia asilimia 20 mpaka 25 ambazo wanachukua malighafi kutoka nchi nyingine ikiwepo kwetu Tanzania wanaenda wanachakata kule na baadaye wanatuuzia bidhaa zenye thamani kubwa. Kwa hiyo, we are just exporting jobs halafu tunanunua bidhaa teknolojia kwa bidhaa kubwa sana, wakati Mwenyezi Mungu ametubariki haya tuweze kuyafanya hapahapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda na kengele imelia nilikuwa nataka tu kushauri nini tufanye. Kama nilivyosema awali, kuwepo na mandate value addition kwa wawekezaji wote wanaokuja hapa Tanzania, kuhakikisha kwamba wanaweka thamani kwenye madini yetu. Pia tuanzishe special economic zones za barite minerals na tunajua tunatakiwa tuhame kwenye nishati, nilichangia juzi graphite, nickel, lithium tuweze kuhakikisha tunatengeneza, tukishakuwa na hii industrial zone tutavutia wawekezaji lakini tutatengeneza bidhaa kama nilivyosema na kuongeza thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuvutie strategic partnership, wasiwe tu just wawekezaji kuja kuchukua vitalu na kuchimba na kupeleka. Waje watuletee ujuzi, waje wahakikishe kwamba walete teknolojia hapa Tanzania ili tuweze ku-benefit kama Taifa. Pia katika hizi natural critical minerals na strategic minerals tuhakikishe tunaziainisha kama ambavyo Waziri amesema mapema kabisa, ili tujue zipo ngapi ili tuweze kuwekeza kwa uthabiti, lakini pia tuziwekee sasa kwa mpango mkakati, if it is five years kama alivyosema kwenye vision yake au it’s ten years ili sasa kuhakikisha kwamba tunakamata soko la kimataifa na tunanufaika nazo hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho tuhakikishe sasa, ninaona sasa it’s high time kwa sababu ya haya madini ya kimkakati na madini muhimu, Serikali iangalie uwezekano wa kuunda kamisheni ambayo itakuwa ina-deal na haya madini muhimu, yaani ikiwepo kamisheni kabisa muhimu ambayo ita- deal na haya, iweze kuratibu, uweze kuvutia wawekezaji na iweze kuona ni vipi tunakwenda. Maana yake haya madini tukiyaweka, sasa hivi hivyo tu nimesema madini jadi ndiyo yanatuletea hizi fedha zote, dhahabu, almasi, tanzanite, rubi and the like. Tukiwekeza huku kwingine kwenye madini muhimu na madini ya kimkakati, tutaenda mbali na tutafikia uchumi wa dola trilioni moja kama ambavyo tumejiwekea kwenye Dira ya 2050.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutahakikisha per capital income ya Mtanzania inakuwa seven thousand dollars kwa mwaka na tutahakikisha tunakuza GDP yetu kama ambavyo tumeweka kwenye mpango wetu kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni hayo ambayo nilikuwa ninataka nishauri leo, kwa sababu ya muda mengine nitaandika kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)