MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha kimkakati ndani ya Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Viwanda na Biashara naomba nijibu swali namba 10 la Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunafanya kazi, na tumeandaa mpango wa ujenzi wa Viwanda nchini katika kuongeza thamani ya bidhaa zetu ikiwemo Mji wa Tarime ambapo itazingatia uongezaji wa thamani katika mazao ya kilimo, mifugo na madini ambayo yanapatikana huko.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje katika ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vyenye mkakati kupitia Taasisi za TISEZA na SIDO. Wakati huo huo tunahamasisha balozi zetu, wadau mbalimbali na wananchi wote wa Tanzania kwa pamoja kutangaza rasilimali na vivutio ambavyo vipo katika Mji wa Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla ili hamasa hiyo iende sambamba na kutoa vivutio vya kikodi na visivyo kikodi ambavyo vinaendelea kutolewa chini ya Taasisi ya TISEZA.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -
Je, lini Mradi wa Maji Ziwa Victoria utakamilika na kutoa huduma ya Maji kwa Mitaa yote 81 ndani ya Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa Maji wa Miji 28 wa Rorya - Tarime uliopo mkoani Mara kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 134. Kazi zinazotekelezwa kupitia mradi huu ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) katika Ziwa Victoria lenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 29 kwa siku; ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, (treatment plant), wenye uwezo wa kutibu maji lita milioni 28 kwa siku; ulazaji wa mabomba umbali wa kilomita 110; ujenzi wa matanki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita milioni kumi; sanjari na ujenzi wa kituo kimoja cha kusukuma maji, (booster station).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu umefikia wastani wa 16% na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027 kulingana na upatikanaji wa fedha, ambapo unalenga kunufaisha zaidi ya wananchi 460,000 waishio katika Wilaya za Rorya na Tarime, ikiwemo mitaa 81 iliyopo kwenye kata nane za Tarime Mjini.