Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Esther Nicholas Matiko (12 total)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Tarime ni miongoni mwa maeneo ambayo yanapata mvua ya mara kwa mara, na hivyo kusababisha barabara kuharibika na kuathiri shughuli za maendeleo na uchumi za Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kujua, nini mkakati wa Serikali wa kulingana na mazingira ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ya mvua ya mara kwa mara, kujenga barabara ambazo zitastahamili hali ya hewa ya Mji wa Tarime ili wananchi wa pale waweze kupita muda wote kwenye barabara zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya Barabara za Tarime ni kama ilivyo hali ya Barabara za Mji wa Morogoro. Mpango ambao tumeuweka kwenye Mkoa wa Morogoro, vivyo hivyo tutau-extend kwenda Tarime. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Barabara ambayo inaanzia keep left inakwenda mpaka Mogabiri yenye kipande cha takriban kilometa 9.3 iliyopo Tarime Mjini imeharibika sana kiasi cha kupelekea ajali mbaya sana na wakati mwingine vifo. Hata hivyo, kwa sababu tayari mkandarasi yupo na yupo tayari kuanza kazi anasubiri tu malipo ya awali, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupeleka fedha hizi ambazo ni takriban shilingi bilioni 7.9 ili barabara hii iweze kutengenezwa na kuunganishwa na ile barabara inayoenda mpaka Nyamwaga ambayo tayari imeshakamilika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba kipande hicho ni kweli kimeharibika, kilikuwa na lami, lakini barabara ilitangazwa yote. Ilibidi tuanze mbele ili baadaye tuweze kufumua kipande hiki ambacho amekiongelea Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunajua kwamba hatuwezi tukatoka na barabara ya vumbi kutoka Tarime halafu tukaenda kuipata lami mbele. Kwa hiyo, nimhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tunaandaa malipo ili mkandarasi aweze kulipwa na kuanza kuikarabati, ambayo ni sawa na kuijenga upya hiyo barabara ambayo ina zaidi ya kilometa tisa. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tarime una Miradi mitatu ya TACTIC, ambayo ni Stendi ya Kimange, barabara za lami ikiwepo Barabara kutoka Lebu – Kebaga mpaka Biyambu, ambayo ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Tarime pamoja na Mradi wa Dampo. Ninataka kujua ni lini sasa miradi hii itaanza na kukamilika kwa manufaa mapana ya wananchi wa Tarime Mji? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tarime ni miongoni mwa miji inayokua kwa haraka. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoupambania huu Mji wa Tarime; tupo katika mpango wetu wa kutekeleza huu Mradi wa TACTIC Awamu ya Tatu na ngazi ya usanifu wa dhana, pamoja na usanifu wa awali tuko mwishoni kuukamilisha. Tutakwenda kutangaza zabuni, kuanza ujenzi mara moja. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao unakaribia kukamilika mwaka huu Septemba kuna wananchi ambao walipisha huo mradi. Sasa ningetaka kujua hawa wananchi waliopisha mradi huu mkubwa ni lini wanaenda kulipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge kwa kuendelea kuwapigania. Kwanza kuhitaji wa wananchi wapate huduma ya majisafi na salama, lakini pia wale ambao wanapisha mradi wahakikishiwe kwamba wanapewa haki yao ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali, kabla hatujalipa tunafanya tathmini na kujiridhisha wanastahili kulipwa kiasi gani? Yupi anayestahili kulipwa, na yupi ambaye hastahili kulipwa? Baada ya kujiridhisha, Serikali inakwenda kufanya malipo kulingana na haki ya kila mwananchi ambaye atakuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi ya maji.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kufuatia majibu ya Serikali, kwanza kabisa ningependa kusema wazi wawekezaji wengi hasa wale wakubwa wanapenda kuwekeza Mkoa wa Pwani, labda kwa sababu kupo karibu na Dar es Salaam. Huku pembezoni na kama ilivyo Mji wa Tarime, siyo rahisi sana kuweza kuvutia wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru Serikali imekiri kwamba kwa jiografia ya Mji wa Tarime, tuna upatikanaji mkubwa wa malighafi za kilimo, mifugo pamoja na madini. Pia, Mji wetu wa Tarime uko mpakani, na hivyo kuifanya Tarime Mji kuwa kituo kizuri tu cha kiwanda cha kuzalisha thamani.

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kujua kwa kuwa hasa bidhaa za ujenzi ni ghali sana kwa kule kwetu Mkoa wa Mara, na asilimia kubwa inatoa Kenya, Serikali haioni kwamba ni wakati mwafaka kuhakikisha kwamba inavutia wawekezaji wakubwa wa vifaa vya ujenzi kama uzalishaji wa mabati, nondo, vifaa vya maji ili waje kuwekeza kule ili kupunguza watu kwenda Kenya au kupata bidhaa Tanzania kwa gharama kubwa zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa malighafi za kilimo zinapatikana, na pia tungependa kupata mwekezaji mkubwa ambaye anaweza kuchakata na kuwa na Kiwanda cha Biskuti kwa sababu tuna viazi vingi sana vinasafirishwa kuja huko mikoani au crips ambazo zinatokana na ndizi. Serikali haioni pia kuna haja sasa ya kumleta mwekezaji huyu mkubwa kuacha wale wadogo ambao umeeleza kwenye jibu lako la msingi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, kwanza nikiri maelezo ya Mheshimiwa Mbunge. Tarime ni Wilaya ya kimkakati na hasa tunapozungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki iko mpakani na iko kimkakati, na ndio maana mkakati ambao tunao sasa hivi ni kuimarisha biashara katika mtengamano huu wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki na kutumia Tarime na mikoa ya mipakani kama maeneo ya kimkakati wa Tanzania ku-access masoko katika Jumuiya hiyo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Serikali inatoa rai kwamba tunatangaza vivutio ambavyo ni vya kikodi na visivyo vya kikodi hususan kwenye miradi ya kimkakati ambayo inaweza kuwekezwa katika maeneo maalum ya kiuchumi na hii ikiwemo misamaha na nafuu ya kikodi ili kuhamasisha wawekezaji kwenda nje ya maeneo ambayo tumeyazoea hasa katika mikoa ya Pwani ili ku-access soko kubwa zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tarime ambalo ni eneo la kimkakati ku-access masoko hayo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusiana na suala la kutafuta wawekezaji wakubwa. Kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Dira ya 2020-2050, lengo letu ni kuongeza thamani ya mazao, thamani ya madini yetu ambayo tunazalisha nchini, viwanda vya kimkakati ambavyo vinatoa ajira na kutuhakikishia pia uwepo wetu katika Jumuiya na ku-access masoko ya SADC pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Shule ya Amali ya Nyandoto iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime imeshakamilika miundombinu ya madarasa, ofisi, vyoo na nyumba ya Mwalimu, lakini shule hii ilijengwa nje ya mji, hivyo tunahitaji tupate fedha kwa ujenzi wa bweni na karakana, ili shule ianze. Sasa ni lini Serikali itapeleka fedha hizi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba, shule hii imejengwa awamu ya kwanza na tunafahamu kwamba katika mpango wa ujenzi wa shule zote 103 za amali mabweni, karakana na mitambo yote ya kihandisi ni sehemu ya ujenzi wa shule zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga awamu ya kwanza, zimeanza kutoa huduma kama shule za kutwa; awamu ya pili inakwenda kujenga mabweni, karakana pamoja na miundombinu yote ya uhandisi ili kuhakikisha shule hizo zinatoa huduma inayotakiwa. Kwa hiyo, tupo kwenye hatua za mwisho za kupata fedha kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu hiyo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Wananchi wa Mji wa Tarime wana adha kubwa sana ya maji, na tegemeo lao kubwa; na wanaishukuru Serikali kwa Mradi mkubwa wa Maji Ziwa Victoria wa shilingi bilioni 134 lakini mradi huu ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu. So far wamepeleka shilingi bilioni 24 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba hizi shilingi bilioni 110 zinaenda ili mradi huu ukamilike ndani ya muda na kuweza kupunguza adha ya maji kwenye Mji wa Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kabisa kwamba Mheshimiwa Esther Matiko ameendelea kupigania sana wananchi wake wa Tarime Mjini, na pia ameendelea kuhakikisha kwamba mradi huu anausukuma ili uweze kupata fedha na uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba mradi huu unaenda kuwa mwarobaini, lakini mkakati wa Serikali sasa wa namna gani mradi huu unaenda kukamilika, ni kupunguza utitiri wa kutangaza miradi mingi wakati tuna miradi ambayo bado haijakamilika na haijaanza kutoa matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa tunaenda kuhakikisha kwamba badala ya kutangaza miradi mingi na kuzigawanya fedha ambazo zingeenda kukamilisha miradi kama hii, sasa tunaenda kuweka hitimisho katika utaratibu wa namna hiyo, na mkakati wetu ni kumaliza miradi viporo. Tukishamaliza baadaye tutaendelea na miradi mingine ambayo tutaweza kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mradi huu ni kipaumbele kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na tuna uhakika mradi huu utakamilika na wewe mwaka 2030 utarudi, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na kwa niaba ya wananchi wa Babati Vvijijini pamoja na Tarime Mjini, maana mara kadhaa nimesikia ukilalamika pia, kuna watendaji na maafisa kilimo walioajiriwa kwenye idara ya afya na elimu wanajitolea sana lakini zikitolewa ajira hawapewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni kwamba iweke hiki kigezo kama added advantage, wale wanaojitolea wapewe priority kama wanavyofanya wenzetu wa jeshini? Waliopitia jeshini wanapewa kipaumbele. Wale unakuta wamejitolea kwenye taasisi za umma wapewe kipaumbele inapokuwa imetangazwa ajira wanachukuliwa wao kwanza halafu ndiyo wanaenda kwa wale wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema kwamba watu wa Tarime pamoja na wa Babati Vijijini ambapo na mimi ni mdau mkubwa, ni ukweli usiyopingika wako vijana ambao tayari wanajitolea, lakini kwa kuona hivyo ndiyo maana nimesema Serikali imeweka utaratibu mzuri kuhakikisha wale vijana wanaojitolea wanaingia kwenye mfumo ni lazima kuwepo na ushindani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivi, tukubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba ili kutenda haki kwa sababu siyo wote wanaopata nafasi ya kujitolea, lakini advantage ya yule anayejitolea, anapoenda kwenye ushindani tunaamini kwamba yule atafanya vizuri kwa sababu tayari ameishi katika maisha ya utendaji. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuweza kunipa fursa ya kuuliza swali na tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuweza kutoa utofauti kati ya madaraja yale mawili.

Swali langu ni kutaka kujua Serikali imejifunza nini kutokana na uendeshaji wa madaraja haya mawili ili kuweza kuongeza ufanisi kwenye miundombinu mingine ya kimkakati ambayo mnajenga nchini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishakuwa na private sector kwanza una uwezo wa kufanya miradi mingi kwa sababu private sector wanachangia na wewe unachangia na kwa maana hiyo ndiyo maana nadhani utaona hata kwenye maboma Serikali tunasema wananchi wakishachangia tunaweza tukajenga maboma 30 badala ya kujenga maboma 15 kwa sababu kuna nguvu ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ndiyo maana wenzetu maana yake hili siyo suala jipya labda sisi ndiyo tumeanza na wengine wanasema tumechelewa, ndiyo maana miradi mingi sasa hivi tunasema tutakwenda kwenye PPP na huo ndiyo mtazamo wa Serikali. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri tunakushukuru kwa kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Nilikuwaona Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo.

WAZIRI WA MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nataka nichukue nafasi kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri anavyojibu maswali kwa umahiri wa hali ya juu sana kwa sekta ambayo amei-master sana tangu awe Mheshimiwa Naibu Waziri katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nijibu swali na niweke maelezo ya msingi na swali la Mheshimiwa Matiko ni la muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya fundisho ambalo tunalipata tunapoelekea kwenye ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma, ni kwamba ni muhimu tutoe elimu mapema kwa wananchi juu ya nature ya mradi wenyewe. Mradi wa Daraja la Kigamboni kuanzia mwanzo ilikuwa ni kwamba huu ni mradi ambao utajengwa kwa fedha zitakazotolewa na NSSF na utakapokamilika ni kwamba fedha zitarudi kwa wananchi kulipa fee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Tanzanite tumelijenga kwa fedha za mkopo nafuu (concessional loan) na mule ndani mpaka ukupe concessional loan maana yake ni kwamba siyo business tungeweka tangu mwanzo kwamba wananchi watalipa isingekuwa concessional loan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ambacho tunajifunza hapa ni kwamba lazima sisi Serikali tutoe maelezo ya kina kuhusu mradi unapoanza. Hapa tunajiandaa kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tunajiandaa kutekeleza mradi wa PPP wa barabara ya Dar es Salaam - Chalinze kuja huku kwa PPP maana yake lazima tuambie wananchi kwamba mradi huu utajengwa kwa PPP na kwamba fedha ambazo zitajenga zitarudishwa kwa njia ya kulipa.

Kwa hiyo, watakapokuwa wanapita siyo tumejenga leo kesho wakasema ah! kwa nini tunalipia, kwa hiyo nadhani kitu kikubwa hapa ni kwamba ni elimu kwa umma na tutaongeza jitihada katika eneo hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Kimataifa la Mazao la Lemagwe ni muhimu sana kwa uchumi wa Tarime, Mara, na Taifa, na ujenzi ule wa Soko la Kimataifa unaenda sambamba na ujenzi wa ghala. Ninataka kujua, ni lini sasa unaenda kukamilika baada ya kuwa umesimama kwa muda na mmesainisha mwaka 2025 mkataba? Lini wananchi wa Tarime wanategemea Soko la Kimataifa linaenda kukamilika sambamba na ghala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwathibitishie tu wananchi wa Tarime kwamba, Soko la Lemagwe tulishasaini mkataba, ambacho kilikuwa kimechelewa ilikuwa ni fedha na tayari tulishaomba fedha Wizara ya Fedha na wametuthibitishia kutupatia kwa ajili ya kumkabidhi mkandarasi na kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatarajia kwamba mradi ule utakamilika kwa wakati, na kama utachelewa, basi kutakuwa na extension ya muda usiozidi miezi sita kabla ya ule mradi kukamilika.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa na mimi kuuliza swali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Tanzania tunatarajia kunufaika na uwepo wa AFCON na ukuaji wa utalii, na kwa kuwa wageni ambao watakuja kipindi cha AFCON watahitaji hoteli zenye hadhi ya nyota nne mpaka tano wengine.

Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuweza kufufua au kutafuta wawekezaji kwenye hoteli za umma ambazo zimetelekezwa kwa muda mrefu kama vile Motel Agip na Embassy ili ziweze kuongeza malazi, ajira na mapato ya taifa kuliko kuendelea kuwa liability kwa Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko, aliyeuliza kwa ujumla hoteli mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi kimsingi, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, nitajikita kwenye miradi iliyopo kwenye sekta yetu. Kama ambavyo nimeshaanza kumjibu Mheshimiwa Mgore, tunatambua maeneo mbalimbali, kwanza, kwa ajili ya kuongeza ajira, ukifufua hoteli unaongeza ajira kwa wananchi, lakini pili, unaimarisha utalii. Kwa maeneo ambayo ni ya kimkakati ambapo AFCON inakwenda kutumika maana yake pia inasaidia kuongeza accommodation, wananchi waweze kupata mahali au washiriki kwenye kombe hilo, waweze kushiriki.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ametuongezea msukumo mkubwa zaidi ya kutushauri na kutukumbusha Serikalini ili tuendelee kuona umuhimu wa kuweza kufufua maeneo hayo kwa maslahi ya Watanzania wote.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Mradi huu ulitarajiwa kukamilika Novemba, 2025, wakafanya extension kuja Septemba, 2026. Nimeuliza takribani mara 40. Bunge lililopita niliuliza takribani mara 26 na Bunge hili takribani mara 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa kuwa Mji wa Tarime una mitaa 81 una kata nane. Kata nne tu ndizo zinapata kama takribani 45% za maji; kata nne nyingine hazipati kabisa maji; na zile kata zina mitaa, lakini zina taswira kama ya vijiji. Ninataka kujua ni kwa nini sasa Serikali iweke mpango wa dharura wakati tukisubiri mradi huu ambao unachukua muda mrefu sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ione kuwa kuna haja ya kuchimba visima kwenye kata hizi, ili hii mitaa ambayo haina maji kabisa, hasa kwenye taasisi za shule na vituo vya afya waweze kupata maji wakati tukisubiria huu mradi wa Ziwa Victoria kama vile ambavyo wenzenu wa umeme wanafanya wanapeleka REA kwenye mitaa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi huu wakati unapita, kuna wananchi ambao ardhi zao zimechukuliwa kwa ajili ya kupisha mradi huu lakini mpaka sasa wananchi hawa hawajajua hatma yao lini watalipwa fidia zao. Ninataka nijue ni mkakati gani Serikali ilionao wa haraka kuhakikisha kwamba wanawalipa wale wananchi fidia waliopisha mradi huu ili kuendelea kupata baraka wakati wanajenga mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Esther Matiko kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya ya kuwasemea wana Tarime Mjini. Pia ninakiri, ukiachana na Bunge lililopita ndani ya kipindi hiki cha Bunge, nimejibu hili swali la Mheshimiwa Esther Matiko zaidi ya mara 10, ninatambua kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba mradi huu una maslahi makubwa sana kwa Majimbo ya Tarime Mjini, Tarime Vijijini, na Rorya; na Waheshimiwa Wabunge wote, akiwemo Mheshimiwa Waitara pamoja na Mheshimiwa Chege wamekuwa wakiuongelea mradi huu. Sisi kama Serikali tumesikia sauti ya Wanatarime, tumesikia sauti ya wananchi wake na sisi tutahakikisha kwamba tunaongeza speed ya kupeleka fedha ili mradi huu uende kwa kasi zaidi ili uweze kutoa matokeo kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na fidia, labda niseme hivi, kuhusu fidia ya wananchi tulikubaliana na wananchi wake. Sehemu ambapo bomba linapita Serikali haitalipa fidia, tulikubaliana na kwa maandishi. Maeneo ambayo tunalipa fidia ni eneo la chanzo cha maji, eneo la booster station na eneo la mtambo wa kutibu maji; na katika eneo hilo tayari tumeshalipa zaidi ya milioni 36. Orodha tunayo, Mheshimiwa Mbunge akiomba tutampatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunatambua kwamba tuna zaidi ya wananchi 20 ambao wameshalipwa. Eneo ambapo bomba linapita hatulipi fidia ya ardhi, tunalipa fidia ya uharibifu wa mazao. Tayari tumeshafanya tathmini, tunahitaji shilingi milioni 40 na tayari malipo yanaendelea. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tuko makini kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata haki yao kulingana na jinsi ambavyo wamejitolea ili mradi huu uweze kupita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hivi vijiji katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amesema, kata hizi changamoto yake kubwa ni kwamba, visima vinapochimbwa katika hizi kata baada ya kuweka pampu, maji yanakauka. Pia tatizo kubwa la Tarime Mjini vyanzo vya maji ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu kwamba umuhimu wa wananchi katika kata hizi tano ikiwemo Nyandoto, Nankende. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi kata tumemwelekeza MD aweze kufanya tathmini, iwapo katika kata nyingine kuna mradi ambao una maji ya kutosha, tufanye extension kwenda katika hizo kata ambazo zina changamoto ya maji wakati tukiwa tunasubiri utekelezaji wa mradi mkubwa wa Ziwa Victoria wa shilingi bilioni 134 ambao ni uwekezaji mkubwa sana wa Serikali ya Awamu ya Sita. Ninakushukuru sana.