Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mecktridis Fratern Mdaku (2 total)

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Malinyi lina Miradi ya Maji katika Kijiji cha Misegese – Ihowanja na Mtimbira na miradi hii imekaa muda mrefu zaidi ya miaka mitatu sasa bila kukamilika. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha miradi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, ni Mbunge mahiri, na pia ni Mjumbe katika Kamati yetu ya Maji na Mazingira, tunaendelea kutambua mchango wake mkubwa sana katika kuishauri Serikali na kuisimamia. Katika kuwatetea wananchi wake, sisi tutaendelea kumpa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo madai ya wakandarasi ndani ya Jimbo lake, na tayari yameshaletwa na yameshafika kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu, wanayafanyia kazi. Tunaamini kabisa kwamba ndani ya kipindi cha miezi miwili mitatu hii, tutapeleka fedha ili wakandarasi hawa walipwe ili miradi hii ambayo imekaa kwa muda mrefu iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali, siyo hiyo miradi pekee, miradi yote inayoendelea kutekelezwa nchini tunayo maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba tunakamilisha kwanza hii miradi ambayo imeishaanza badala ya kuanza miradi mipya ili kuhakikisha kwamba tunaanza kupata matokeo kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya. Ninakushukuru sana.
MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Malinyi lina mtandao wa mita chache za lami. Je, ni lini sasa Serikali ina mpango wa kuongeza kupitia programu ya kuboresha Halmashauri za Wilaya au Makao Makuu ya Wilaya kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, Mheshimiwa Mecktridis amelifuatilia suala la Barabara za Malinyi mara kwa mara. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tunaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe na pale inapowezekana kuendelea kujenga barabara kiwango cha lami na tutahakikisha kadri fedha zinapopatikana tunatoa kipaumbele cha juu kabisa kwa ajili ya Mji wa Malinyi.