Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zuberi Yahya Mfaume (2 total)

MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza:-

Je, hatua gani zimechukuliwa za uchafuzi wa Mto Mfizigo na Mhuva zitokanazo na shughuli za madini na kubaini kemikali zilizopo na athari zake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, pili kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania, kwa dhamana kubwa aliyonipa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Ninaomba nimuahidi Mheshimiwa Rais kwamba nitafanya kazi kwa juhudi, maarifa na weledi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, sasa ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Yahya Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mito ya Mfizigo na Mhuva iliyopo katika Jimbo la Morogoro Kusini ni moja ya maeneo ambako hufanyika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini katika maeneo ya pembezoni mwa mito hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mito hiyo inatunzwa na kuzuia uchafuzi wake kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali mwaka 2025 ilichukua sampuli za maji ya mito hiyo kwa ajili ya kupima ikiwa kuna uchafuzi wa kemikali zitokanazo na uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Matokeo ya vipimo vya sampuli hizo vilionesha kuwa kuna kemikali za chuma na manganizi. Kemikali zilizobainika kuwepo zinatokana na miamba iliyokuwa inachimbwa na siyo kwamba zinatokana na matumizi ya kemikali za kuchenjua madini kama zebaki.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kuchukua hatua kulinda vyanzo vya maji na mito ikiwemo Mito ya Mfizigo na Mhuva katika mazingira ya Morogoro Kusini kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 na Sheria ya Rasilimali za Maji ya Mwaka 2009.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza:-

Je, lini Serikali itadhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mvuha, Selembala, Dutumi, Kisaki, Bwakila Juu, na Kolelo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Yahya Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini:-

Mheshimiwa Spika, kipindi cha kiangazi hutokea adha ya upungufu wa malisho maeneo mengi, ambapo hupelekea wafugaji kuanza kuhama kwa ajili ya kutafuta maji na malisho. Hali hii inasababisha wimbi la wafugaji vamizi kutoka nje ya Wilaya ya Morogoro kuleta mifugo mingi ambayo husababisha mwingiliano na uharibifu wa mazao.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na migogoro, ikiwa ni pamoja na kutenga na kutambua maeneo ya malisho kwa wafugaji kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, ambapo jumla ya vijiji 68 vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi kwa kutenga hekta 54,577. Watendaji wote wa vijiji na kata kutoruhusu wafugaji wageni kuingia kwenye maeneo yao bila kufuata taratibu, kuhamasisha uzalishaji wa malisho ili kuongeza upatikanaji wa malisho kwa wafugaji.

Mheshimiwa Spika, wizara za kisekta zimeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa elimu ya ufugaji wenye tija wa kuwa na mifugo michache.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama kufanya operesheni maalum ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Morogoro. Pia, Serikali inapopata tetesi ya mgogoro kwa wafugaji na wakulima, Viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya hufika kwa wakati na kuhakikisha migogoro inatatuliwa.