Supplementary Questions from Hon. Zuberi Yahya Mfaume (11 total)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Morogoro Kusini ni miongoni mwa majimbo ambayo yako katika hali mbaya sana ya miundombinu kwa sababu, sehemu kubwa ya jimbo hili ni milima, na hivyo, inaathiri hata performance yetu katika elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu za ufaulu, tuko chini na hali ya afya tuko hoi. Tuna changamoto ya Barabara ya Dakawa – Bwakila Juu, ambayo kwa kweli haipitiki kabisa. Tuna changamoto ya barabara ya Kolelo – Lukange...
MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swali moja kwa moja.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, ni kwa kiasi gani tutapewa upendeleo maalumu kutokana na hali mbaya tuliyonayo, kwa ajili ya kuzikarabati barabara hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipokea hili, na Serikali, tutalifanyia kazi kwa kadiri ya ambavyo tutapata taarifa za wataalamu wetu tukimshirikisha Mheshimiwa Mbunge. Pia ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, shughuli hizi za madini ni shughuli zinazowaendeshea maisha wananchi wenzetu. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa sasa elimu ya utunzaji wa mazingira ili wananchi wenzetu waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba shughuli za madini ni shughuli muhimu kwa uchumi wa nchi yetu na wananchi na sisi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Wizara zote zenye nasaba na masuala ya mazingira na madini tutaendelea, kwanza kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa wananchi na wachimbaji wote wa madini kuzingatia sheria na taratibu za uhifadhi wa mazingira ili kuwa na uchimbaji wa madini na uhifadhi wa mazingira endelevu. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Spika, ninaomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kutokea katika swali langu la msingi.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; mpaka hivi sasa ninavyozungumza hapa bado kuna mifugo katika mashamba ya wakulima huko katika Jimbo la Morogoro Kusini. Nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa hivi ili iweze kutekelezwa na mifugo hiyo iondolewe katika mashamba ya wakulima?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara ina mpango gani sasa katika Jimbo la Morogoro Kusini kuongeza ujenzi wa majosho, malambo pamoja na kasi ya kuelimisha wafugaji juu ya ufugaji bora wa kisasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa maswali yanayogusa changamoto hizi za wakulima na wafugaji. Sisi Ofisi ya TAMISEMI tunashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo na wameendelea kutoa elimu wenzetu Wizara ya Mifugo na pia wanatoa mbegu za ruzuku kwa ajili ya malisho ili kuondoa migogoro hii kabisa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha mifugo inaondolewa katika maeneo ya wakulima wetu na baadae nitakaa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo ili tuweze kuyaangazia maeneo haya na kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kujenga majosho mengi nchini. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuweze kuainisha eneo ambalo hasa amelizungumzia ambalo halijapata majosho mpaka sasa ili tuweze kujenga majosho hayo.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza swali kwenda Wizara ya Ujenzi kwamba, ni lini daraja linalounganisha Kata ya Tawa na Kata ya Konde vitakwenda kutengenezwa kwa maana limeshavunjika na hakuna mawasiliano katika kata hizo mbili? Ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu kwa ufupi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, sijamsikia vizuri Mheshimiwa Mbunge, hilo daraja na…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge taja daraja hilo kwa sauti usikike.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Naibu Spika, daraja hilo ni Daraja la Mto Mfizigo ambalo linaunganisha Kata ya Tawa na Kata ya Konde, kwa sasa hakuna mawasiliano baina ya kata hizi mbili na hii ni Barabara ya Kiswila kuelekea Tawa, ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, labda ungetaja na jimbo maana kata na kata pengine kwa Mheshimiwa Waziri inaweza ikawa ngumu.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, katika Jimbo la Morogoro Kusini Barabara ya Msalabani kwenda Tawa katikati kuna Daraja la Mto Mfizigo ambalo linaunganisha Kata ya Tawa na Kata na Konde, daraja hili sasa hivi halipitiki kabisa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimpe pole Mheshimiwa Mbunge, lakini pia na wananchi ambao wamekumbwa na adha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu maelekezo kwa Meneja wa Mkoa wa Morogoro kwa sababu ni kweli katika kipindi cha mvua madaraja mengi yamekatika na yanashindwa kupitika, lakini pia hata maeneo mengine ambayo barabara zimekatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachofanya labda tu kwa ujumla ni kwamba tumeshatoa maelekezo kwa mameneja wote wa mikoa, kufanya tathmini na kila siku kuleta taarifa Makao Makuu ya TANROADS na Wizara ili Serikali wakati inatafuta hizi fedha za dharura, basi ziweze kwenda kurudisha mawasiliano kwa dharura tukiwa tunajipanga kufanya matengenezo ama ujenzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe maelekezo specifically kwa Meneja wa Mkoa wa Morogoro ahakikishe anafika eneo hilo, achukue hatua za haraka kwanza kurejesha mawasiliano ya muda wakati Serikali inatafuta fedha kulijenga hilo daraja kwa upya, ahsante.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Morogoro Vijijini kwa sasa ndiyo mzalishaji mkubwa wa karafuu. Wawekezaji kutoka Indonesia walionesha nia ya kutaka kuwekeza katika eneo letu. Je, Wizara ina mpango gani sasa wa kuendelea kuvutia wawekezaji ili wakaweke viwanda vya kusindika karafuu kule Morogoro DC? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mbunge kwa swali lake zuri la kutetea watu wa Morogoro, hususan kwenye suala la kilimo cha karafuu na haja ya kupeleka viwanda na wawekezaji Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, kipaumebele chetu ni kuvutia wawekezaji. Rais ameshatuagiza, lakini ninyi wenyewe ni mashahidi Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa kipaumbele katika kuvutia wawekezaji anapozunguka huko duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue suala la Morogoro kama kipaumbele, nasi tutaliweka kwenye mpango wetu wa kuhamasisha na kuvutia wawekezaji waje kuwekeza Morogoro. Ninashukuru.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini na wananchi wa Halmashauri ya Morogoro ningependa kujua, ni lini ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki utaanza? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bigwa – Kisaki, kilomita 78, mkandarasi ameshalipwa na ameshaanza kazi za awali kufanya site clearance ikiwa ni pamoja na kujenga zile kambi za mhandisi mshauri. Kwa hiyo, kazi imeshaanza Bigwa – Kisaki. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nimweleze kwamba kuna changamoto kubwa katika eneo la Bwakila Chini, kwa maana ya Kijiji cha Ngwade, Serikali imepima maeneo kwa ajili ya kuwamilikisha wananchi na wananchi wamelipa fedha zote, lakini hadi sasa hawajapatiwa hati zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Kijiji cha Msonge pia wananchi walijiunga katika kikundi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo, wakawa na makubaliano na Serikali ya kujenga zahanati katika eneo husika, wananchi hawa waliahidiwa kupimiwa viwanja na Wizara ya Ardhi na kumilikishwa na tayari wamefanya wajibu wao kwa kujenga jengo lile, lakini hadi sasa Serikali haijatimiza wajibu wake wa kuwapimia na kuwapatia hati ili waendeleze shughuli za kilimo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari sasa kuambatana nami jimboni kuwasikiliza wananchi na kujionea changamoto hizi ili aweze kuzitolea majibu? Ninafahamu Mheshimiwa Naibu Waziri kwa muda mchache aliohudumu katika ofisi yake ni bingwa wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza Morogoro Kusini kwa kweli wamechagua Mbunge ambaye anafuatilia changamoto mbalimbali za wananchi wake. Wakati ni mgeni kabisa katika nafasi hii alishawahi kunipigia na tuliwahi kuzungumza juu ya changamoto mbalimbali na hatma yake na leo hii ameleta jambo hili na anazidi kuwatetea kujua haki ambazo wanastahili katika maeneo hayo, hongera sana Mbunge na hongereni wananchi wa Morogoro Kusini kwa kupata mwakilishi mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji alivyovitaja na alivyozungumza kuhusu haki yao ya kupatiwa hati, huo ni wajibu wa Wizara kwa sababu tayari mpango ulishapangwa na upimaji umeshafanyika, ni suala la kutoa hati tu. Nikuahidi, nitaambatana na wewe katika ziara ambayo tutakubaliana, tutaenda maeneo husika na siku hiyo nikuhakikishie kama kutakuwa na hati ambazo wanastahili kupewa watu hao katika vijiji hivyo tutazitoa na wewe ukiwemo na wananchi wako wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Morogoro Kusini lina kata 17 na takribani katika kila kata tayari wananchi wameshajenga maboma ya madarasa na sasa wanasubiri pesa za kumalizia kutoka Serikalini.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa mtatuingizia pesa ili tuweze kumaliza vyumba hivyo vya madarasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mfaume, Mbunge wa Jimbo la Morogoro.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kwa kuweka nguvu zao na kwenda kujenga maboma hayo na ni maelekezo mahususi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kwamba kabla ya kuanza miradi mipya, tuhakikishe maboma yote tunayakamilisha na yanatoa huduma tarajiwa.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa jimbo, tunakwenda kukamilisha maboma haya ili kuhakikisha kwamba yanaanza kutoa huduma kwa wakati na tukielekea mwaka 2028 ambapo tutapokea double cohort ya wanafunzi darasa la sita na la saba wote watamaliza kwa pamoja, kwa hiyo, ni lazima tuhakikishe miundombinu hii tunaikamilisha kwa wakati ili ikatoe huduma kwa wananchi wetu. Naomba kuwsilisha.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Ni lini sasa barabara ya Mto Mbozi kwenda Tandali itajengwa? Ni kwa miaka mitatu sasa haijaguswa kabisa. Barabara hii iko katika Jimbo la Morogoro Kusini, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Morogoro Kusini amefuatilia mara kadhaa kuhusiana na barabara hiyo na tulikwishawasiliana na Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Morogoro na walishawasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa Serikali iko kwenye taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kufanya matengenezo ya barabara hizo, na barabara hizi nyingi zitatengenezwa baada ya mvua hizi ambazo zinaendelea kunyesha kukatika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini kwamba Serikali hii sikivu inatambua, na italifanyia kazi.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ahsante Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini ninakushukuru kwa kukiri kwamba kulikuwa na malipo ambayo yalichelewa. Kwa kweli tuna changamoto kubwa kwa vyama vya ushirika vya msingi katika kushughulikia uuzaji wa nafaka hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itarasimisha mfumo mbadala na mfumo shindanishi ambao utaleta tija kwa wakulima? La pili, Morogoro Kusini tumekuwa wazalishaji wa ufuta ambao una daraja la juu. Kuna changamoto kubwa ya vifaa vya kilimo pamoja na pembejeo. Ni lini sasa Wizara itapeleka vituo vya ukodishaji matrekta pamoja na kusambaza pembejeo ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza tena Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mheshimiwa Mfaume kwa kufuatilia sana wananchi wake mara kwa mara. Nimwondoe shaka tu kwamba, moja, Serikali ipo karibu sana na kuwasikiliza wananchi kero zao zinapokuwa zinatatuliwa, ndiyo maana katika wiki mbili zilizopita, nilijibu swali la namna hii hapa Bungeni, watu wakiomba tupitie mfumo ili kurekebisha ule upungufu. Kwa hiyo, Serikali tuko tayari kupitia, sisi pamoja na wadau na kuainisha yale maeneo yenye upungufu ili tuweze kuongeza ufanisi katika mifumo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Serikali tuko tayari muda wowote kufanya kazi pamoja ili tuweze kutengeneza mfumo mbadala na shindanishi ambao unaweza kuwasaidia wananchi hao. Kuhusu ni lini tutapeleka matrekta huko na pembejeo, mpango wa Serikali ni kuanzisha vituo vya zana za kilimo katika halmashauri zote nchini. Lengo la Serikali ni kuanzisha vituo 1000, na mpaka sasa hivi tumeshafungua vituo 79 katika halmashauri kama 25 hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mpango huu ni endelevu, na katika mipango inayokuja, Jimbo la Morogoro Kusini lipo katika mpango huo, ahsante sana.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Mimi ninatokea Jimbo la Morogoro Kusini, ningependa kujua Barabara ya Kilengezi, Kongwa hadi Lukooni lini itaanza kutengenezwa ipo kwenye hali mbaya sana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ziko barabara na hususani katika Jimbo la Morogoro Kusini ambalo lina neema ya mvua nyingi sana na kila msimu wa mvua barabara nyingi zinaathirika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mheshimiwa Zuberi, kwamba Serikali inaendelea kwanza tumeshafanya tathmini ya barabara zote zilizoharibiwa na mvua na tumeshapata gharama ya fedha ambazo zinahitajika takribani shilingi bilioni 300 na hivi sasa Serikali inaendelea na taratibu za kibajeti kwa ajili kuanza kupeleka fedha kwa utaratibu wa dharura, lakini pia utaratibu wa kibajeti ili kurekebisha barabara hizo.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa awamu tutahakikisha tunaendelea kufanya matengenezo katika barabara hiyo.