Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sara Msafiri Ally (2 total)

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupata kura nyingi sana kwenye Uchaguzi Mkuu. Nichukue nafasi hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mvomero kwa kunichagua kuwa Mbunge wa Jimbo la Mvomero kwa kura nyingi za kishindo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze katika kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, na niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kusema kwamba hotuba ile imeleta matumaini makubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninukuu maneno ya mwisho kabisa kwenye hotuba ile ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyazungumza hapa Bungeni, kwamba anatamani sana kipindi chake cha awamu ya pili anapokwenda kumalizia ngwe hii, basi akiondoka aache wananchi wa Tanzania wakiwa na tabasamu. Kwa kweli ukisoma ahadi zilizokuwa kwenye hotuba ile, hakika Watanzania wataachwa na tabasamu kubwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niipongeze sana Tume Huru ya Uchaguzi kwa kazi waliyoifanya hasa ya kuongeza vituo vya kupiga kura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge tunaotoka kwenye majimbo ya vijijini, majimbo yenye changamoto za kijiografia, zenye milima na miinuko mikubwa, majimbo ambayo wananchi wake ni wakulima, wafugaji, (wafugaji wale ambao wanategemea asubuhi wafungue maboma, watoe mifugo wakachunge jioni warudishe), wananchi ambao ni wajasiriamali wadogo wadogo, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu kitendo cha kuongeza vituo vya kupigia kura kimesaidia sana wananchi wengi wa makundi haya ambao iliwalazimu hata kama siku ilikuwa ni ya mapumziko ya kupiga kura, lakini wao ambao wamejiajiri sekta binafsi kuweza kutoka mapema kwenda kupiga kura, kurudi kufungua maboma yao kwenda kufanya shughuli za ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, wajasiriamali wadogowadogo, wakina mama wanaouza mbogamboga sokoni, mama lishe, bodaboda na wafugaji wote waliweza kupiga kura kwenye majimbo yetu ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee kabisa tunashukuru, wale ambao tumetoka kwenye majimbo yenye miinuko mikubwa (milimani). Jimbo la Mvomero kata 15 tarafa mbili zipo kwenye milima; wananchi wengi hasa wa makundi maalum: wakinamama, wajawazito, walemavu, na wazee walikuwa wanatamani sana kufanya takwa lao la Kitaifa kipindi cha nyuma kwenye michakato mingine ya uchaguzi, lakini walikuwa wanashindwa kwenda kupiga kura kwa sababu ya changamoto za kijiografia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile sasa vituo vya kupigia kura vilikuwa vya kutosha ndani ya Jimbo langu la Mvomero tulikuwa na vituo 711. Vituo vilikuwa kwenye maeneo ya makazi ya watu, maeneo yenye wafanyabiashara, na kwenye maeneo ya shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, wakinamama na makundi mengine waliweza kutumia fursa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kutokuwa na misongamano sehemu za kupigia kura kulihamasisha sana wananchi kujitokeza kupiga kura. Kipekee wamenituma wananchi wa Tarafa ya Mgeta, Tarafa ya Mvomero ambazo ni kata 15 na kata nyingine 10 za wafugaji kwamba Mheshimiwa Mbunge uende ukampongeze Mheshimiwa Rais na wananchi, nao wamefanya takwa lao la Kikatiba kwa mara ya kwanza kupiga kura nyingi. Kwa hiyo, tunashukuru sana Serikali kwa kuliona hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ndani ya siku 100 mambo aliyokuwa ameahidi kuyafanya kwenye hotuba hasa kwenye umeme vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha anakamilisha Bwawa la Mwalimu Nyerere. Amehakikisha vijiji vyote nchi hii vinapata umeme. Aliahidi kwamba vitongoji ambavyo havijapata umeme ataanza kutekeleza hiyo ahadi, na tunaona ndani ya siku 100 tumeenda kupata miradi ya vitongoji 9,000 ndani ya nchi hii na Jimbo la Mvomero tumepata vitongoji 93.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua bado vitongoji 13,000 ambavyo bado havijapata lakini tunaamini kwa speed na kasi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchi yote na vitongoji vyote vinaenda kupata umeme. Kama ndani ya siku 100 ametuletea vitongoji 9,000, tunaamini kabisa kwamba vitongoji vyote vinakwenda kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kwenye suala la maji wenzangu wameongea mambo mengi na tunatambua kazi kubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama vijijini na mijini. Huko nyuma tunaona kwamba 84% mpaka 91%, upatikanaji wa maji umeongezeka mijin, na 70% mpaka 85%, upatikanaji wa maji umeongezeka vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba maji haya yanapatikana kipindi kile kukiwa na mvua tu, kukiwa na kiangazi hali ya upatikanaji wa maji nchini inakuwa ni changamoto. Sisi tunaotoka kwenye maeneo ya wakulima na wafugaji, migogoro ya wakulima na wafugaji inakuwa mingi kwa sababu wafugaji wanahamia kutafuta maji, kwa hiyo tumekuwa na changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwenye Hotuba yake kwamba anakwenda kujenga ujenzi wa gridi ya Taifa ya maji, na maji haya sasa yatatoka Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, na Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, hatutatumia tena na kutegemea maji ambayo yanatoka kwenye mito ambayo yanategemea mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Ni kwamba sasa kwa miaka mitano hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakulima wanaenda kupata maji ya kutosha, wafugaji watapata maji ya kutosha, viwanda vitapata maji ya kutosha, matumizi ya majumbani maji ya uhakika, safi na salama yatapatikana. Kwa hiyo, hata wananchi wangu ambao wengi ni wafugaji, tutaenda sasa kuwekeza ile ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba wafuge kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutajenga majosho, tutaleta madume na mbegu bora za mifugo kwa sababu sasa tunaachana na biashara ya kuhamahama. Vilevile, wakulima nao watafanya kazi za kilimo na kujielekeza kwenye shughuli nyingine za uzalishaji mali kuliko ilivyokuwa sasa hivi wanashinda kwenye mashamba kufukuza mifugo. Kwa hiyo, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tuiunge mkono Serikali yetu ili haya ambayo Mheshimiwa Rais anaenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye masuala ya maji tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ameahidi kuongeza maeneo ya wakulima hasa kilimo cha umwagiliaji kutoka ekari milioni tatu mpaka milioni tano, na kupima maeneo ya wafugaji kutoka ekari milioni tatu mpaka milioni sita. Tunaamini kabisa utekelezaji wa jambo hili unaenda kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sasa Serikali yangu na Wizara na taasisi za Serikali, Mheshimiwa Rais ameahidi kuweka kongani za viwanda kwenye wilaya. Tunajua kuna suala la kibajeti, lakini kuna mambo ambayo hayahitaji bajeti, basi Serikali na taasisi zinazohusika zikamalize migogoro ya ardhi kwenye maeneo ambayo tumetenga kwa ajili ya kongani za viwanda ili tukiyasubiri hayo ya kibajeti, basi maeneo haya yawe tayari ili tunapopata wawekezaji maeneo hayo wayakute.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kupitia ahadi ya Mheshimiwa Rais kwa Wilaya ya Mvomero eneo la Dakawa kutujengea mradi wa umeme wa kilovolti 220 kwa ajili ya viwanda vya Turiani na maeneo ya Gairo na Kilosa. Tunaiomba Serikali ifanye hivyo ili wananchi hawa waweze kufaidika na kupata ajira nyingi kupitia uwekezaji wa viwanda, kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hii bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kipekee ninamshukuru sana Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri aliyoitoa yenye mipango endelevu ya kuongeza tija kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nitoe shukrani zangu sana kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge, ambayo inashughulikia masuala ya kilimo kwa ushauri mzuri sana ambao Mwenyekiti ameutoa kwenye mchango wake binafsi na kwenye hotuba yake hasa kuongeza masoko na kufanya utafiti kwenye mbegu, kwenye mbolea na namna ya viwanda vyetu vitakavyoongeza uzalishaji na kufanya tathmini kwa wale ambao wameshindwa kuendeleza viwanda, tuone namna nzuri ya kuwaondoa na kuweka wawekezaji wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ziara aliyoifanya ndani ya Jimbo la Mvomero akiambatana na Waziri wa Mipango na Uwekezaji. Walitembelea maeneo ya uwekezaji ya viwanda vya sukari na mashamba ya miwa, walipata fursa ya kuona changamoto za viwanda ambavyo vinazalisha kwa kiwango kikubwa zaidi ya malengo, lakini changamoto ipo kwa wakulima wa miwa, miwa yao haivunwi kwa wakati na hivyo wanapata hasara kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na masuala ya kuingiza sukari na Mheshimiwa Waziri kwa pamoja walisema watalishughulikia hili. Salamu za wananchi wa Mvomero wana imani kubwa na Mheshimiwa Waziri, ninaamini hakutakuwa tena na kuharibika kwa miwa ya wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali, Jimbo la Mvomero lina skimu za umwagiliaji 10 na skimu hizi 50% tayari Serikali imefanya usanifu bado fedha, lakini kwa kipekee tunashukuru kwamba zipo skimu ambazo Serikali imeshatoa fedha. Skimu za Lukenge, Mgongola, Misufini, mkandarasi amepatikana. Skimu ya Dakawa tayari hekta 3,000 zinafanya uzalishaji wa 100%, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye changamoto za kusuasua kasi ndogo ya uwekezaji kwenye miundombinu hii hasa kwenye skimu ambazo Serikali imeshatoa fedha. Tunayo Skimu ya Mgongola, skimu hii imeanza ujenzi tangu mwaka 2021, mkandarasi akaleta changamoto zake, mradi ukasimama wa shilingi bilioni 5.6, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupa fedha, mkandarasi akalipwa bilioni 1.7, akapotea akaishia mitini, kwa hiyo skimu ile ipo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha muda mfupi alichokaa ofisini kwake, ameweza kutoa ushauri wa namna ya kuachana na huyu mkandarasi, mkandarasi huyu sisi ametushinda. Serikali ya Wilaya, Serikali ya Mkoa, Tume ya Umwagiliaji wamehangaika naye imeshindikana fedha zetu amechukua 1.7 bilioni na fedha iliyobaki ni pungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ushauri alioutoa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, basi tuiombe Tume ya Umwagiliaji tuna Mkurugenzi Mkuu mchapakazi pale, masuala ya kisheria yamekwisha ili sasa tuachane na mkandarasi, tukamalizie. Nishauri kwa sababu muda umeenda ni zaidi ya miaka mitatu sasa tangu fedha zitolewe na Serikali na mradi umesimama, niiombe Tume ya Umwagiliaji ikafanye mradi ule kwa force account ili sasa wananchi wale wa Jimbo la Mvomero hasa eneo la Tulia ambapo kuna mafuriko waweze kunufaika na miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao pia mradi mwingine ambao Mheshimiwa Waziri ametuahidi, ni Mradi wa Lukenge ambao Serikali imewekeza 1.4 billion, mradi umekamilika kwenye miundombinu bado pampu. Mheshimiwa Waziri na Serikali wametuahidi kwamba tarehe 30 mwezi huu ambao ni keshokutwa watakuwa wametununulia pampu ya shilingi milioni 800 ili wananchi wale wakafanye uzalishaji. Sasa kwa sababu miundombinu imekamilika miaka miwili iliyopita, ilibaki pampu ambayo Mheshimiwa Waziri ametuahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niombe ndani ya skimu zetu za Jimbo la Mvomero, tuna hekta 41,883 uwekezaji uliofanywa na Serikali ni 19% tu sawasawa na hekta 8,002. Kama wenzangu walivyoongea na Wabunge na Kamati ya Bunge ilivyoshauri tunahitaji mapinduzi ya kilimo kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa sababu kinakopesheka, tuna uhakika wa kuvuna na tuna uhakika wa masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Benki ya Kilimo, Tume ya Umwagiliaji na Serikali wakae waone namna ya kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo hasa kwenye kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika ili sekta ambayo imeelekeza kwenye Jimbo langu kwenye 19% tu tuweze tukawekeze kwenye 100% ili tuweze kuzalisha kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mbolea wameongea wenzangu. Tunavyo viwanda vya ndani vya mbolea, Serikali ione namna ya kusaidia viwanda hivi vikopesheke viweze kuzalisha mbolea ya kutosha na ya uhakika ili wakulima wasipate tabu ya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)