Supplementary Questions from Hon. Sara Msafiri Ally (8 total)
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongea. Jimbo la Mvomero lina miradi sita ya maji inayoendelea ambayo imekuwa ikisuasua kutokana na changamoto za kifedha ikiwepo Mradi wa Maji wa Tandale - Homboza na Mradi wa Dakawa. Je, lini Serikali itapeleka fedha ili hii miradi sita ikamilike kwa wakati na wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la dada yangu Mheshimiwa Sara Msafiri, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara kwenye Jimbo la Mvomero na Mradi huu wa Dakawa pamoja na Tandale ni kweli kabisa kwamba ni mkombozi kwa wananchi wa Mvomero utakapokamilika, lakini kati ya miradi ambayo 878 inayoendelea yenye gharama ya shilingi trilioni 1.3 na hii miradi iko humu. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha miradi viporo vyote inaisha ili wananchi waweze kuona matokeo na maji yatoke kwa ajili ya matumizi ya maji safi na salama. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, na ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri na kwa mipango mizuri ya kuboresha barabara zetu hasa zilizopo chini ya TANROADS. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, barabara hii ni barabara ya kimkakati ya kiuchumi ambapo kuna shughuli za kiuchumi za uchimbaji wa madini, madini ambayo yanategemewa sana kwenye viwanda vya tiles, Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na Kituo cha Afya kikubwa kinachotegemewa na Tarafa mbili ya Mlali na Mgeta, lakini kuna soko kubwa la kisasa pale, barabara hii imekuwa ikikwamisha shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kutenga fedha kwa ajili ya kufanya feasibility study ili barabara hii ya kilometa 59 ijengwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa barabara hii imeenda mpaka ikaunganika na Kituo cha Kisaki cha Treni ya TAZARA na wananchi wa Tarafa ya Mgeta na Mlali ni wazalishaji wakubwa kama nilivyoongea kwenye swali la kwanza: Je, Serikali haioni kuchelewesha kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami ni kuwachelewesha wananchi kuboresha shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubali kwamba barabara hii ni ya muhimu sana. Kama alivyosema, kwamba kuna shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo madini, kituo cha afya, lakini pia kuna soko. Ndiyo maana tumesema kwamba tunahakikisha inapitika muda wote, na yale maeneo ambayo yamekuwa yanakwamisha, tunayaboresha kwa kuyajengea lami ama zege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika jibu langu la msingi, tumekiri kwamba tunatafuta fedha ili tuweze kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kuhusu kuunganisha na Kisaki, ninakiri kwamba hii barabara ndiyo inayounganisha hawa wananchi mpaka kituo cha TAZARA cha Kisaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna vipande viwili. Sisi Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tunaishia pale Kikeo na kutoka Kikeo kwenda Kisaki inahudumiwa na wenzetu wa TARURA. Kwa hiyo, tutawasiliana na wenzetu ili tuweze kuhakikisha kwamba, wakati hatujaijenga kwa kiwango cha lami, lakini barabara yote iweze kupitika kuanzia hapa ambapo inaanzia, Sangasasanga – Kikeo hadi Kisaki, ahsante.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini TARURA itatenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara za kiwango cha zege kwenye maeneo ya milimani kama ilivyo Wilaya ya Mvomero ambapo maeneo mengi yako milimani na barabara zinaharibika kipindi cha mvua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sara Msafiri, Mbunge wa Mvomero amefuatilia mara kadhaa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuhusu suala la barabara za Mvomero. Ni kweli, wote ni mashuhuda kwamba Mvomero imekuwa na mafuriko mengi sana na ya mara kwa mara, ikiwemo mwaka 2026. Matokeo yake barabara zetu nyingi za udongo zinazolewa na maji na tunakuwa tunaanza upya mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI tuko kwenye hatua za mwisho za kufanya design ya barabara madhubuti na imara zaidi ambazo zitajengwa kwenye maeneo yenye mafuriko, milima na mvua nyingi zaidi ili tuhakikishe kwamba barabara hizo zinadumu na zinahudumia wananchi kwa muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumhakikishie Mheshimiwa Sara Msafiri na wananchi wa Mvomero kuwa Serikali sikivu iko kwenye hatua za utekelezaji na tutahakikisha kwamba tunaboresha barabara hizo.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Wapo baadhi ya wawekezaji wamehodhi maeneo makubwa ya ardhi na wameshindwa kuyaendeleza kwa 100%, na wengine kubadilisha matumizi. Nini kauli ya Serikali katika kufanya tathmini na kurejesha maeneo hayo ili kupangiwa matumizi mengine Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mfumo ndani ya Serikali wa kuwezesha wawekezaji hawa wapatiwe ardhi, na ardhi yao ilindwe ili waweze kufanya shughuli ambazo wameombea. Tunashirikiana vizuri na hawa TISEZA na mamlaka nyingine kwa ajili ya kuwapatia ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na ninatoa tu angalizo kuwa maeneo haya yalitolewa kisheria na wanatakiwa wayatumie kulingana na walivyoomba. Ila Wizara ya Ardhi ina utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa kutekeleza matumizi ya ardhi waliyoomba kutokana na hati ambayo tumepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi pale tunapogundua mwekezaji ameshindwa kutimiza masharti ya upatikanaji wa ardhi hiyo na kuyaendeleza, huwa tunampata taarifa na kufuata utaratibu wa kuyachukua na kuweza kuwakabidhi watu wengine ambao wana mahitaji ya ardhi. Hivyo, Mheshimiwa Sara, kama ana mwekezaji ambaye ameshindwa, hivyo, tuwasiliane na Wizara ya ardhi ili tuweze kufuata utaratibu tuweza kuyachukua maeneo hayo.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingi zimekuwa zikiharibika kwenye Jimbo la Mvomero hasa maeneo wanayofanya shughuli za uchimbaji wa madini; kama Kata ya Mvomero, Kata ya Lubungo na maeneo mengine.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti kwenye maeneo hayo ya barabara ili ziweze kupitika kipindi chote cha shughuli za wananchi wanapofanya shughuli zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka sasa imeongeza bajeti ya TARURA kwa zaidi ya takribani mara nne na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara zetu zote za vijijini na mijini zinapitika ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa ufanisi mkubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Sara Msafiri, Mbunge wa Jimbo la Mvomero, kwamba Serikali inatambua changamoto na hususani ya Mvomero kwa hali ya hewa mvua nyingi mafuriko na shughuli nyingine za kiuchumi ambazo zinapelekea barabara nyingi kuharibika na majimbo mengine yenye sura ya aina ya Mvomero, Serikali imeweka mpango madhubuti kuhakikisha kwamba barabara hizo zinajengwa na kupitika vizuri. (Makofi)
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Mvomero kwenye Tarafa ya Turiani ambayo ni ya kimkakai ya kiuchumi haina miundombinu ya barabara wala masoko. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja ya kuiweka miradi hii kwenye mpango wa miradi ya TACTIC ili kuongeza uchumi wa wananchi wa Turiani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba Jimbo la Mvomero Tarafa ya Turiani ni moja ya maeneo ambayo yanakua kwa kasi kwa kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi na za kijamii na zinahitajika barabara, masoko, stendi na miundombinu mingine ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Sara Msafiri kwamba, kwa sasa mradi wa TACTIC unatekelezwa kwenye miradi ambayo ilishafanyiwa design kwenye miji 45. Kwa hiyo, tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya maeneo ambayo hayapo kwenye miradi ya TACTIC, ikiwemo Mvomero, kuhakikisha tunajenga barabara hizo kwa awamu, lakini pia kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu kama masoko ili wananchi wa Turiani na Mvomero kwa ujumla wapate huduma bora.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni ahadi ya Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi kujenga maktaba na maabara ya kisasa kwenye kila wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga maabara na maktaba ndani ya Jimbo la Mvomero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ni Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, na ni dhamira ya Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya maktaba na maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Sara Msafiri, Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Serikali inaendelea hivi sasa na ujenzi katika maeneo mbalimbali kote nchini, lakini kwa sababu uhitaji ni mkubwa, Serikali inaendelea kuratibu upatikanaji wa fedha na tutaendelea kujenga miundombinu hiyo kwa awamu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pia Jimbo la Mvomero litapewa kipaumbele.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza ninaishukuru sana Serikali kwa kutupa gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya cha Mziha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za kijiografia kwenye Jimbo la Mvomero bado tunahitaji Serikali itusaidie kuleta gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya cha Mlali, Mgeta na Kibati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, lini Serikali italeta magari hayo ili kusaidia huduma hii ya afya iweze kufanya vizuri kwa wananchi wa Mvomero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Mvomero na tulifanya ziara ile siku ya Muungano katika jimbo lake na wananchi wanampenda kweli kweli kwa sababu ikitokeza kwa wingi ili kushuhudia ile ziara na kutupa moyo watendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutenga bajeti ya kuongeza magari kadri ambavyo tunayapata kutoka Wizara ya Afya ili kuona namna gani tunaendelea kuwasaidia mama zetu, wagonjwa katika Jimbo la Mvomero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie ushirikiano kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kadiri ambavyo tunapokea magari na sisi tutaelekeza hasa kwenye halmashauri ambazo zina upungufu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.