Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Wilson Charles Mahera (1 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili nami niweze kuchangia katika mpango huu. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwa kazi nzuri na maandalizi mazuri ya hizi nyenzo kwa ajili ya kuenda kutekeleza Dira ya 2050. Nimshukuru pia Waziri wa Fedha naye kwa mipango mizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa, ninaanza kwa kuipongeza Serikali; tayari imekwishakuja na hizi nyenzo kama tatu kwa ajili ya utekelezaji wa Dira yetu ya 2050, ambapo Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo wa Miaka Ishirini wa Tano una dhima kwamba tunataka kuwa na Taifa ambalo lina uchumi jumuishi na Taifa linalojitegemea; ambapo kipato chake cha mtu mmoja mmoja kitakuwa dola 7,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuweza kuyafanya hayo inaonekana Wizara pamoja na Tume ya Mipango wamefanya kazi nzuri ya kufanya mapitio ya mipango ile mitatu iliyokuwepo kwa ajili ya Dira ya 2025 na wamebaini baadhi ya changamoto ambazo zilipelekea baadhi ya malengo kutokuweza kutimia. Moja ya hizo changamoto inaoneka ni kwamba kulikuwa na matumizi machache ya sayansi teknolojia na ubunifu, pia uzalishaji mdogo viwandani na kilimo pia kilichangia kwa kiasi kidogo; pia kulikuwa na tatizo la kutokuwepo na ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa vile tunataka kwenda kwenye Taifa ambalo linajitegemea kuna mambo mengi mazuri. Pia ilikuwa inaonekana kwamba kulikuwa na upungufu wa fedha katika kutekeleza baadhi ya mambo ambayo walikuwa wamepanga kuyafanya. Pamoja na hayo mafanikio yapo, lakini hatukufanikiwa kwa 100%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi mazuri kabisa ambayo yako kwenye mipango na yameelekezwa. Changamoto inayokuja ni kwamba tunatakiwa tujitahidi sana kufanya kazi business as usual ili tutekeleze hayo ambayo tumeyaandika humu ili ndoto yetu iweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kizuri ni kwamba pia wamekwenda kujifunza kwenye zile nchi ambazo ziko upper middle-income countries, nchi zenye uchumi wa kati hadhi ya juu na tayari wameona ni nini walichofanya mpaka wakafanikiwa. Kwa hiyo, kama Taifa ni lazima na sisi tuzingatie hizo core values ambazo tummeziona na pia ni lazima tuzingatie misingi waliyokuwa nayo na zile drivers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna mengi tunakokwenda; moja ya mambo ambayo tunaya-aspire ni kwamba tunataka tuwe na Taifa la watu ambao ni educated na learned. Nitajikita tu kwenye suala la elimu, kwa sababu ili tuweze kufanikiwa kwa kweli ni lazima tuwekeze sana kwenye elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba hata bajeti sasa itaongezeka, kutoka trilioni 7.31 hadi 8.19, lakini ninadhani bado inabidi kwa kweli tuongeze Bajeti ya Wizara ya Elimu. Hii ni kwa sababu mambo yote haya tunayokwenda kuyafanya wananchi lazima waelimishwe. Kuna ujuzi mbalimbali ambazo unatakiwa, hivyo ni lazima wananchi wasome waweze kuelimishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kuwa na Taifa linalojitegemea tunaangalia; tangu mwaka 1974 wakati wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alielekeza; alikuwa na falsafa ya elimu ya kujitegemea ambapo hatukuweza kuwa nyenzo nzuri za kuweza kulitekeleza hilo hadi miaka ya 51 hapa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuja kuelekeza Wizara ya Elimu kupitia mitaala na ile mihtasari pamoja na maboresho ya sera na kuja na suala la elimu ya amali. Hii inaonekana itakuwa suluhisho katika kuchangia kuongeza pato la Taifa, lakini wananchi wa Tanzania kuweza kujiajiri wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi Profesa Mhongo amesema asubuhi kuhusu namna watakavyokwenda kupata fedha. Ukiangalia kwenye suala la VETA; ametoa mfano wa kujifunza kwa Nchi za China na India. China kwa mfano wao kwa mwaka watu milioni 13 wanaingia kwenye shule hizi za vocations, na watu milioni 10 wana-graduate. Katika watu ambao sasa hivi wanakwenda kwenye kuchangia katika ajira kwenye viwanda na mijini wengi wao, zaidi ya 70% China wanatoka kwenye hizi vocations.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Tanzania kwa sasa ninachoweza kushauri kwamba kwenye Wizara ya Elimu hivi vyuo vya VETA ambavyo vipo kwa kweli awamu ya kwanza tumeshajenga bado kuna awamu ya pili; na ukitaka kuwa na elimu ya kujitegemea ni lazima ufanye practical zaidi. Kwa hiyo, tunatakiwa Tume ya Mipango kushirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha tuwekeze fedha nyingi ili tuweze kukamilisha hivi vyuo. Vikamilike kwa hadhi ambayo inatakiwa pia tusomeshe watu wengi kwenye masuala haya ya vocations.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana pia; nimeona wakati wanafanya review kulikuwa na matumizi kidogo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Sasa tufanye kitu ambacho nadhani Tume ya Mipango iliwahi kusema ruleless prioritization. Ni lazima tuamue kwa makusudi kipaumbele kwamba, tuwekeze zaidi kwanza katika kuelimisha watu ili baadaye hawa watu ndiyo waje wachangie katika sekta nyingine hizo za nchi yetu ili kuweza kuleta mabadiliko. Kwa hiyo, ninashauri sana kwamba, tuwekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia VETA hizi bado ni chache, tunatakiwa tuongeze idadi ya VETA, pia tuongeze programs nyingi na shule za sekondari za amali; tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais; zimejengwa sasa hivi 103, lakini ninadhani bado zinahitajika; awamu ya kwanza ndiyo imekamilika. Ili tuwe na watu ambao watapata ujuzi unaohitajika ni lazima wafanye practical za kutosha. Kwa hiyo, tunaomba fedha ziongezwe tena Wizara ya Elimu ili kusudi awamu ya pili ya ujenzi wa hizo shule za amali uweze kuendelea. Karakana zikamilike ili kweli watu watakapotoka kwenye mfumo huo wa amali basi wawe na ujuzi mbalimbali ambao unahitajika. kwa hiyo, nilipenda nichangie hiyo kwenye sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende zaidi tena mpaka kwenye vyuo. Tunamshukuru pia Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mradi wake ule wa elimu ya juu kwa mageuzi, tuna kampasi kila mkoa. Tuzitumie zile campuses vizuri kwa ajili ya ujuzi mbalimbali katika particular areas huko zilipo hizo kampasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona China kwa mfano wamejenga VETA kwa kushirikiana na Local Governments za huko. Kwa hiyo, hata hapa kwetu tuangalie, zile halmashauri ambazo zina uchumi mzuri basi Wizara ya Elimu au Tume ya Mipango iweze kushauri huko kwenye hizo halmashauri basi waanzishe hizo VETA kwa ajili ya kupata ujuzi unaohitajika kwenye hayo maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija harakaharaka kwenye Sekta ya Afya kwa sababu tunataka tuwe na Taifa la watu ambao wana afya ya kutosha, ukiangalia kwenye Sekta ya Afya asilimia kubwa ya Watanzania wanatibiwa kwenye afya ngazi ya msingi. Kwa mfano 97% ya akinamama mwaka 2024 waliohudhuria kliniki walipata huduma katika vituo vilivyo chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Vilevile, 93% waliojifungua Tanzania hapa walipata huduma hiyo kwenye vituo vya afya, lakini idadi kubwa ya akinamama zaidi ya 75% ya waliofanyiwa upasuaji kwa ajili ya kujifungua walifanya pia kwenye vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunakwenda kwenye suala la Bima ya Afya kwa Wote, lakini bado tuna-operate kwenye Sera ya Mwaka 2007. Ninadhani ile Sera nayo inabidi ifanyiwe mapitio kwa haraka kwa sababu kuna mabadiliko makubwa sana tangu ilipoanza mwaka 2007 mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgawanyo wa fedha nao lazima uangalie. Hili suala lisiwe suala la Wizara moja, liwe ni suala la Kisekta. Ili tuweze kufanikiwa pia, ushauri wangu katika kutekeleza hii mipango ni lazima Wizara zikubali sasa kwamba tunakwenda kufanya kazi Kisekta zaidi badala ya kufanya kazi Kiwizara. Kwa sababu Wizara moja ikifanikiwa wakati Wizara nyingine hazijafanikiwa haina maana yoyote ile, lazima tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, tukishirikiana hata mgawanyo wa fedha utakwenda kule ambako fedha zinahitajika kwa wakati muafaka. Kwa hiyo, hayo yalikuwa ni mawazo ambayo nilikuwa ninashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano fedha, labda ifikie mahali tuweke sheria au formula kabisa kwamba fedha lazima ziende kule ambako ndiko watu wanakozihitaji na wanakozitumia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine walipofanya review ilionekana kwamba kulikuwa na poor linkage kati ya Vocational Education au Academic na industries. Sasa, tunashukuru Wizara ya Elimu tayari wamekuja na Mpango wa Industry Advisory Committee. Ninadhani hii tui-emulate kwenye maeneo yote ili tuweze kuhakikisha kwamba watu wetu wanakwenda huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye viwanda tuweke pia mwongozo au kanuni ya kuwabana hawa watu ili wawe wanakubali internship, kwa sababu wakishaenda kule ndipo ambapo tayari ubunifu utafanyika na baadaye tunaweza kusoma kiteknolojia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa malizia.

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.