MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Mheshimiwa Waziri ameshafanya tathmini ya kujua ukubwa wa tatizo la matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari kwa nchi nzima na kupanga mkakati wake? Ninataka nijue, ni sahihi katika karne ya sasa Wabunge wa Tanzania, kuendelea kujadili na kuuliza maswali kila mwaka ya matundu ya vyoo, meza na viti na watoto kukaa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara kwamba Serikali inatambua umuhimu wa shule zetu zote kuwa na matundu ya vyoo yanayotosheleza na yenye viwango na ubora unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba watoto wetu wanasoma katika mazingira bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila mwaka tumekuwa tukifanya tathmini ya matundu ya vyoo yaliyopo, upungufu na kuweka mikakati katika kila bajeti kutenga fedha kupitia mapato ya ndani ya halmashauri na pia kupitia Serikali Kuu kwa ajili ya kujenga matundu ya vyoo. Kwa hiyo, tuna tathmini ya kila mwaka, tunajua kiasi gani tunayo, kiasi gani tunahitaji na Serikali imeendelea kutenga fedha na kujenga ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ni dhamira ya Serikali kwamba tuondokane na changamoto ya matundu ya vyoo kabisa na ndiyo maana tumeendelea kutenga fedha kila mwaka. Kwa mujimu wa taarifa za Benki ya Dunia ambayo assessment imefanyika hivi karibuni, tunahitaji kwa ujumla katika shule yenye wanafunzi 400 tunahitaji wastani wa matundu ya vyoo 12 (sita ya watoto wa kike na sita ya watoto wa kiume) na sisi kwa kiasi kikubwa baadhi ya shule tumeshazidi kiwango hicho. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha tunaboresha kwenye yale maeneo mengine ambayo yana uhitaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuhakikisha tunajenga matundu ya vyoo, lakini zoezi hili ni endelevu kwa sababu tutaendelea kujenga shule, population ya watoto itaendelea kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hakuna siku tutasema tumemaliza, hatujengi vyoo kabisa, kwa sababu population ipo na shule zitaendelea kujengwa na zitahitaji kujenga vyoo. Kwa hiyo, ni zoezi endelevu. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba zile shule ambazo zina upungufu tunaondokana na changamoto hiyo. (Makofi)