MHE. YAGI M. KIARATU aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha Maji katika Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Yagi Maulid Kiaratu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Maji ni Wakala wa Serikali ulio chini ya Wizara ya Maji ulioanzishwa Mwaka 1974 kwa lengo la kuzalisha wataalam wa maji pamoja na sekta nyingine zikiwemo umwagiliaji na ujenzi. Pamoja na majukumu mengine, chuo hicho kinatoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ya kozi zipatazo 25 kwa ngazi ya Stashahada, Shahada ya kwanza na Shahada ya Uzamili kupitia Kampasi zake za Dar es Salaam na Singida.
Mheshimiwa Spika, Makao Makuu ya Chuo cha Maji yapo Jijini Dar es Salaam na hutumia majengo yaliyopo Ubungo kwa ajili ya shughuli za kitaaluma. Upande wa Kampasi ya Singida, Chuo cha Maji kinatumia Majengo ya Bodi ya Maji ya Bonde la Kati Singida kutolea mafunzo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imepanga kuanza kwa awamu ujenzi wa majengo ya chuo kwa Kampasi ya Singida katika eneo lenye ukubwa wa ekari 41.5 lililopo katika Mtaa wa Mwankoko Manispaa ya Singida ili kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa mafunzo.
MHE. YAGI M. KIARATU aliuliza: -
Je, lini mradi wa maji unaotekelezwa katika mitaa 38 ya Manispaa ya Singida utakamilika ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yagi Maulid Kiaratu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa mitaa 88 katika Manispaa ya Singida ni miongoni mwa Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 17.7. Kazi zilizopangwa kutekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu 12, ujenzi wa matanki tisa yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 4.1, ulazaji wa mabomba umbali wa kilomita 58.7 sanjari na ujenzi wa kituo cha uendeshaji wa mitambo (pump station).
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu mingine unaendelea sambamba na utafiti wa maji chini ya ardhi ili kuweza kupata visima vitakavyoweza kukidhi mahitaji ya mradi huu ambayo ni lita za maji milioni 22.3 kwa siku. Aidha, visima vitatu tayari vimechimbwa na vina uwezo wa uzalishaji wa maji zaidi ya lita milioni 4.9 kwa siku. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha visima vyote vinavyohitajika vinachimbwa na mradi kuendelea na utekelezaji ambapo unatarajiwa, kwa mujibu wa mkataba, utakamalika ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027.