MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninapenda tu kumkumbusha kwamba chuo hicho cha Singida kimeanza muda mfupi uliopita kikiwa na wanafunzi 39, lakini hadi leo tunapoongea wapo wanafunzi 450, mwitikio ni mkubwa.
Mheshimiwa Spika, chuo kina ekari 41 kama alivyosema, lakini tayari wamefanya usanifu. Kinachosumbua sasa ni gharama kubwa za uendeshaji. Pale ukumbi wa Bonde wameshahama, wamepanga eneo ambalo wanalipa shilingi 150,000,000 kwa mwaka.
Myheshimiwa Spika, kutokana na ongezeko la wanafunzi, chuo pia kimeongeza program za mafunzo kutoka programu mbili hadi nane. Mpaka ikifika Oktoba mwaka huu chuo kinakusudia kupokea wanafunzi 1,500. Kwa maana hiyo, eneo lile walilopo sasa halitatosha, lakini pia gharama za uendeshaji zitaendelea kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, naomba commitment ya Serikali, chuo hicho ni kikubwa na bado wanafunzi wanapata shida kupata masomo hayo, na ukizingatia chuo hicho sasa kinatoa mafunzo yanayofundishwa na VETA, kwa hiyo, idadi ya wanafunzi itaendelea kuwa kubwa. Naomba majibu mazuri ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninamshukuru sana Mheshimiwa Yagi kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya. Kikubwa zaidi, kwa muda mfupi kabisa ameelewa kazi kubwa inayofanywa na vyuo vyetu vya maji hususan katika hiki Chuo cha Maji Singida. Kiuhalisia, alichokiongea Mheshimiwa Mbunge ni ukweli kabisa kwamba tulianza na wanafunzi wachache, na sasa wanafunzi wamezidi kuongezeka. Hii maana yake ni kwamba, imani ya Watanzania katika chuo hiki imezidi kuwa kubwa na uhitaji wa majengo umekuwa mkubwa.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Serikali kupitia Wizara ya Maji, tumeamua kuweka kwenye Mpango na kwenye bajeti ya mwaka 2026/2027 ili kuhakikisha sasa tunaanza ujenzi ili kuweza ku-accommodate wanafunzi ambao watakuwa wanadahiliwa katika chuo hiki ili kuepusha chuo kuingia kwenye gharama za kupanga majengo ambayo yatasababisha hasara, badala ya kujikita katika kuboresha huduma ya utoaji wa mafunzo.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumepokea na ninakushukuru sana.
MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Singida wana hamu sana ya kupata usafiri wa anga. Pamoja na kuchagiza shughuli za kiuchumi, usafiri na usafirishaji Singida ni katikati ya nchi. Singida ni jirani na Dodoma, ikitokea rubani akashindwa kutua Dodoma, mji wa karibu kutua ni Singida; lakini kwa sababu, Singida ni Katikati, itakuwa kiungo kizuri cha usafirishaji ndani ya nchi. Ninaomba kauli ya Serikali, ni lini sasa Singida watajengewa uwanja wa ndege? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Singida Mjini na Mheshimiwa Mstahiki Meya Mstaafu kwa ufuatiliaji wake wa uwanja huu mzuri na muhimu kwa Taifa letu. Kama alivyoeleza yeye mwenyewe, uwanja huu ulijengwa miaka ya 1950 na Serikali imekuwa ikiutumia, lakini kwa kweli, kiwango chake kiko chini ni wa changarawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maombi ya Waheshimiwa Wabunge na wakati mwingine viongozi, Serikali imepokea kilio hicho na imeanza kufanya usanifu. Ninamhakikishia, tunakwenda kujenga Uwanja wa Singida na mwaka wa fedha 2026/2027 tunaingiza kwenye bajeti. Tunaenda kuongeza runway kutoka 1,000 mpaka 2,000, tunaweka lami pamoja na kuhakikisha kwamba, tunaweka taa, ili uwanja utumike mchana na usiku.
MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitaishukuru Serikali kutokana na historia ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa Mji wa Singida. Hata hivyo, bado lipo tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Singida wananchi wanahitaji lita milioni 24 kwa siku ilhali upatikanaji ni lita milioni 11 kwa siku; utaona ni chini ya 50% ya mahitaji ya wananchi. Mradi huu wa miji 28 anaousemea Mheshimiwa Naibu Waziri ni mradi ambao umechelewa sana. Mkataba ulisainiwa Juni, 2022 lakini mradi ukaanza Aprili, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuamini mpaka leo bado wanachimba visima, hakuna matanki yaliyojengwa wala mitandao haijatandazwa. Hii inawasababishia wananchi adha ya maji, na hivi ninavyoongea, kuna mgawo mkali wa maji katika mji wa Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Viko vijiji 12 na mitaa kumi ambayo haijawahi kupata maji ya bomba tangu vijiji hivyo vimeanzishwa. Vijiji hivyo ni Uhamaka, Mwampafa, Isomia, Mwachichi, Unyamikumbi A, Unyamikumbi B, Ikhade, Ugauga A, Ugauga B, Ikenga, Isasida A, Isasida B, Unyambwa A, Unyambwa B, Mtamaa A, Mtamaa B, Kimai, Mtaa wa Mtisi, Mwinyutuka na vijiji vingine. Wananchi hawa hawajawahi kufungua bomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba commitment ya Waziri, na ikibidi, akikubali, basi tutafute muda tuongozane mimi na yeye akaone hali halisi huko ndani. Wananchi wanachangia maji na wanyama katika enzi hizi ambazo Rais ana nia nzuri ya kuwatua wanawake ndoo kichwani…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, umeeleweka.
MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yagi Maulid Kiaratu, Mbunge mahiri kabisa kutoka Jimbo la Singida Mjini na kwa namna ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba ni kweli tunayo mitaa ambayo bado haina maji, lakini pia tunavyo vijiji kwa sababu jimbo lake lina vijiji na mitaa, katika mitaa 53, mitaa 40 ina maji, mitaa mitatu ina maji ambayo kidogo hayatoshelezi, lakini mitaa 10 ndiyo mitaa ambayo haina maji kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vijiji 19, tunavyo vijiji saba ambavyo vina maji ya kutosha, pia tuna vijiji takribani vitatu ambavyo maji yake hayatoshi. Vijiji vingine vilivyobaki tunakiri kama Serikali, kwamba bado maji hayajafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu hizi, Serikali mpaka sasa imeshafanya kazi kubwa sana kwa sababu hadi sasa Jimbo la Singida Mjini upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama umefikia zaidi ya 76%. Tunatambua kuwa bado kuna kazi kubwa ambayo tunaendelea kuifanya, lakini kwenye suala la mradi huu wa miji 28, dhamira ya Serikali siyo kuchelewesha miradi, bali kukamilisha miradi ili itoe matokeo, na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la mradi huu wa Singida ni kwamba visima ambavyo vilikuwa vinachimbwa, scenario hii ni sawa na kule Chunya, kwamba wanachimba, lakini visima vinamomonyokea ndani kiasi kwamba wanachimba, lakini bado kunakuwa na changamoto ya kukiendeleza kwa sababu udongo unarudi ndani. Mkandarasi alipata shida sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeamua kumtumia mkandarasi aliyechimba Nzunguni, Zuzu, na Nala, sasa tunamhamishia ili aende na vifaa vyake akachimbe katika Mradi wa Miji 28 Singida Mjini ambapo mpaka sasa tumeshachimba visima vitatu. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imejidhatiti na iko makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kutengeneza mradi ambao hautakuwa na matokeo, na hatuwezi kutengeneza mradi ambao baada ya muda mfupi unakuwa umebaki kama white elephant. Kwa hiyo, tuko makini kufuatilia ili utakapokamilika, utoe matokeo yaliyokusudiwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake la Singida Mjini ili kujionea hali halisi ya maendeleo ya miradi mbalimbali ndani ya jimbo lake.