Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Emmanuel Peter Cherehani (2 total)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali ipo tayari sasa kuleta timu ya wataalam mara baada ya Mkutano huu wa Bunge?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ipo tayari kutumia sasa Mradi wa Bukene pamoja na Mradi wa Isemela ambao bado unatekelezwa kuweza kufikisha huduma ya maji katika Vijiji vya Zobogo, Tinde, Nuru pamoja na Igulamya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Serikali iko tayari na kama nilivyojibu katika swali la msingi, Wizara inatarajia kuunda timu ambayo itaenda kule Itwangi na kwenda kufanya tathmini na kujiridhisha na hali halisi ya huduma ya upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi 3,714 ambayo Serikali iligharimu takribani shilingi trilioni 1.8, ndani ya Itwangi kulikuwa na miradi tisa iliyokamilika yenye gharama ya shilingi bilioni 12.7. Ndani ya Jimbo hili tunayo miradi inayoendelea miwili ambayo ina gharama ya shilingi bilioni 8.9 ikiwemo na kuhakikisha kwamba vijiji vilivyobaki katika eneo hilo ni vijiji 14 tu ambavyo vimebaki bila kuwa na huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, eneo la Tinde, pamoja na Didia, pamoja na Samuye yote yataingizwa katika utaratibu wa kupata huduma ya maji safi na salama. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Barabara inayotoka Kata ya Nyankende inapita Nyambeshi, Kata ya Bulungwa, Sabasabini, Kata ya Mpunze inayotuunganisha na Manispaa ya Kahama haipitiki kabisa na ndio inayolinda uchumi wa Halmashauri ya Ushetu.

Ni nini mkakati wa Serikali kuifanyia marekebisho ya dharura hiyo barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ziko barabara nyingi ambazo zimeathirika na mvua nyingi zilizonyesha msimu ulipita na tayari mkakati wa Serikali umeanza kutekelezwa ambao ni kutangaza zabuni, kupata wakandarasi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara zote zilizokatika na kuharibika zile barabara muhimu sana ambazo ni uti wa mgongo wa maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo barabara hiyo inaunganisha Ushetu na Kahama ni barabara muhimu na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tayari Meneja wa TARURA wa Shinyanga lakini pia wa Wilaya ya Kahama na Ushetu wameshatangaza zabuni, tutapata wakandarasi hivi karibuni kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye barabara hizo. (Makofi)