Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Musa Godfrey Mbuga (1 total)

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Kwa kuzingatia kwamba Jimbo la Kisesa hasa Kata za Mwasengela na vijiji vyake, Sakasaka na vijiji vyake, Mwakisandu na vijiji vyake na Mbugayabanghya ni lango la tembo kuingia katika makazi ya watu. Kwa muda mrefu sasa Serikali imekuwa inaahidi kuwapelekea gari kwa ajili ya kufanya doria Wananchi wa jimbo la Kisesa hususani kata nilizotaja, lakini haijawahi kutekelezwa kwa muda mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka gari kwa ajili ya lindo, kwa ajili ya Jimbo la Kisesa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana nami Jimboni Kisesa ili ajionee madhara yanayosababishwa na tembo pamoja na uharibifu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musa, ninaomba kwanza nimpongeze sana kwa namna anavyofuatilia changamoto za wananchi wake. Niwaambie Wana-Kisesa wamechagua mtu sahihi, kwa wakati sahihi na kwa nafasi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna changamoto ya gari, lakini ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mapema tu ndani ya mwaka huu wa fedha, Serikali itapeleka gari kwa ajili ya kutoa huduma katika jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni suala la wajibu kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda katika eneo lake na kukagua na kuangalia changamoto zilizopo ili tuzipatie utatatuzi wananchi wetu waendelee kuwa na furaha ya uwepo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ahsante sana.